Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

MATAKWA YA MOLA KWA MITUME NO.1

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
MATAKWA YA MOLA KWA MITUME NO.1
Allah (s.w) amewapa Mitume yake nyadhifa mbali mbali, miongoni mwa nyadhifa hizo ni kufikisha ujumbe wake kwa waja wake, ujumbe huo waliopewa Mitume na Mola wao kuufikisha kwa walimwengu ni kwa ajili ya kumuongoza mwanaadamu na kumpatia saada ya duniani na Akhera.
kwa sababu hiyo basi Mitume walitumia njia zote tatu katika kufikisha ujumbe wa Mwenyeezi Mungu kwa watu. Ili kufahamu zaidi tutazielezea njia hizo moja baada ya jengine:
1. Hekima
Hekima ni elimu ambayo inamuwezesha mwanaadamu kudiriki na kupambanua uhakika wa mambo bila ya kuzidisha au kupunguza.
Vile vile hekima ni elimu ambayo inamfanya mwanaadamu kutenda mambo kutokana na akili, na kuyafanyia amali ya matendo aliyoamrishwa na Mola wake.
Mwenyeezi Mungu Mtukufu baada ya kubainisha hukumu zake katika jamii, hukumu ambazo zinamfanya mwanaadamu awe na itikadi nazo na kuzifanyia amali, hii inaonyesha kukua kwa akili ya mwanaadamu. Kama anavyosema Allah (s.w):-

ذٰلِكَ مِمَّا اَوْحَي إِلَيْكَ رَبُّكَ مِنَ الْحِكْمَةِ وَلاَ تَجْعَلْ مَعَ اللهِ إِلَهاً آخَرَ فَتُلْقَي فِى جَهَنَّمَ مَلُوماً مَّدْحُوراً[1]
Haya ni katika hikima alizo kufunulia Mola wako Mlezi. Wala usimweke pamoja na Mwenyezi Mungu mungu mwengine, usije ukatupwa katika Jahannamu ukilaumiwa na kufurushwa.
2. Mawaidha

Mawaidha ni njia inayotumiwa kubainisha mambo kwa elimu na ujuzi au mwenendo mwema, kiasi ya kwamba pindi mwanaadamu anaposikia mawaidha hayo humletea athari moyoni mwake, na huingiwa na shauku ya kutekeleza yale aliyoamrishwa kuyafanya.

Uzuri wa mawaidha ni kwamba, yule anayenasihi awe ni mwenye kuyafanyia amali yale anayowawaidhi watu, na vile vile yale anayonasihi yawe yanawiana na yale ambayo msikilizaji wa mawaidha hayo anayahitajia, kama alivyosema hadharati Luqmani kumwambia mtoto wake, :-

وَإِذْ قَالَ لُقْمَانُ لِابْنِهِ وَهُوَ يَعِظُهُ يَا بُنَيَّ لاَ تُشْرِكْ بِاللهِ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ[2]

Na Luqman alipo mwambia mwanawe kwa kumpa mawaidha: Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu. Kwani hakika ushirikina bila ya shaka ni dhulma iliyo kubwa.

*Huyu Luqmani ni katika mabwana wakubwa wema kabisa waliokuweko ulimwenguni, lakini Mwenyeezi Mungu hakutwambia – wala haikusihi katika hadithi ya Mtume – kuwa alikuwa wa kabila gani wala mahala gani.


3. Majadiliano mazuri

Majadiliano mazuri yaani : wakati wa majadiliano ni lazima kutumia maneno mazuri yenye hekima ambayo yanahusiana au kuwiana na maudhui yanayojadiliwa, ili kusipelekee uadui kwa yule anayepewa mawaidha hayo kwa majadiliano, bali majadiliano hayo yamfanye akae kimya yule anayejadiliwa, kimya ambacho kinatokana na maneno ya hekima aliyowaidhiwa mtu huyo, kama tunavyosoma kuhusiana na Mtume Muhammad (s.a.w.w) alipokuwa akijadiliana na makafiri:-

اَوْ خَلْقاً مِّمَّا يَكْبُرُ فِى صُدُورِكُمْ فَسَيَقُولُونَ مَن يُعِيدُنَا قُلِ الَّذِى فَطَرَكُمْ اَوَّلَ مَرَّةٍ فَسَيُنْغِضُونَ إِلَيْكَ رُؤُوسَهُمْ وَيَقُولُونَ مَتَي هُوَ قُلْ عَسَي اَن يَكُونَ قَرِيباً[3]

Au umbo lolote mnalo liona kubwa katika vifua vyenu. Watasema: Nani atakaye turudisha tena? Sema: Yule yule aliye kuumbeni mara ya kwanza! Watakutikisia vichwa vyao, na watasema: Lini hayo? Sema: A'saa yakawa karibu!

*Hapa Makafiri wanaona kuwa Mwenyeezi Mungu hana uweza wa kumfufua mwanaadamu, Ndiyo wanaambiwa “Na wawe na nguvu za kiumbe gani hicho chenye nguvu kuliko chochote,” na wakifa, Mwenyeezi Mungu anaweza kuwafufua.

[1] Surat Al-Israa Aya ya 39

[2] Surat Luqmani Aya ya 13

[3] Surat Al-Israa Aya ya 51


MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini