Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

ATHARI NJEMA BAADA YA UTUME NO.2

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
ATHARI NJEMA BAADA YA UTUME NO.2

* Mapinduzi ya Mitume yalileta athari gani katika jamii?.
BAADA YA KUBASHIRIWA UTUME
Mapinduzi ya Mitume hayakuwa na harakati zisizokuwa na malengo, bali yalikuwa ni hadafu na madhumuni ya juhudi zilizofanywa kwa ajili ya kufikia katika malengo maalumu, nayo ni kusuluhisha jamii, na kuwatakasa watu wa jamii nzima duniani.
Hapana shaka kuwa Mitume imeteuliwa miongoni mwa watu.
BAADHI YA ATHARI ZENYE BARAKA BAADA YA MITUME KUPEWA UTUME.
1. Furaha katika maisha
Baada ya Mitume kupewa Utume na kuja katika jamii ya watu kwa ajili ya kuwalingania na kuwataka waamini dini ya Mola mmoja, Mola ambaye ndiye mmiliki wa kila kitu duniani, katika kipindi hicho watu walikuwa wakiishi maisha ya tabu na mashaka bila ya kuona mafanikio yoyote au kuwa na matumaini katika maisha yao, lakini baada ya kuja Mitume jamii ilitokwa na mashaka hayo.
Na Mitume iliwaletea furaha na mategemeo ambayo ndiyo muhimu katika maisha ya wanaadamu,  furaha ambayo ilienea miongoni mwa watu wote, na furaha hiyo iliwapa matumaini na kuwaondolea madhila waliyokuwa nayo kabla ya kuja mitume, basi jamii iliikubali dini mpya waliyokuja nayo Mitume, na wakawa wako tayari kufanya kila wanaloweza na kustahamili tabu na mashaka na kila yanayowakuta ili kuwa pamoja na Mitume hiyo.
Na kwa upande mwengine jamii ilitoka katika hali ambayo hakuna mtu yoyote aliyekuwa anatilia maanani wadhifa wake au lile linalomuwajibikia kulifanya, na watu walikuwa hawana hisia yoyote katika jamii yao, lakini baada ya kuja Mitume ambao walikuja na dini ya Mwenyeezi Mungu, watu walisimama kidete wakakabiliana na maadui zao na kupinga fikra za kijahilia, na wakawa pamoja na Mitume kwa kila hali, walikubali kuhama miji yao ambayo ilikuwa imetawaliwa na makafiri, walipigana jihadi na kuipigania dini ya Mwenyeezi Mungu, ili kupata ridhaa ya Mwenyeezi Mungu, katika Qur-ani tunasoma:-

وَالسَّابِقُونَ الاَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالاَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللّهُ عَنْهُمْ وَرَضُواْ عَنْهُ وَاَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِى تَحْتَهَا الاَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا اَبَداً ذٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ[1]
Na wale walio tangulia, wa kwanza, katika Wahajiri na Ansari, na walio wafuata kwa wema, Mwenyezi Mungu ameridhika nao, na wao wameridhika naye; na amewaandalia Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
* Mwenyeezi Mungu atawalipa watu wema waliotangulia na wa sasa na watakaokuja.
Alama nyengine iliyowaletea furaha katika maisha yao ni kupata elimu, elimu ambayo walipewa na Mitume yao, kama inavyosema Qur-ani Tukufu:-
هُوَ الَّذِى بَعَثَ فِى الاُمِّيِّينَ رَسُولاً مِّنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِهِ وَيُزَكِّيهِمْ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَإِن كَانُوا مِن قَبْلُ لَفِى ضَلاَلٍ مُّبِينٍ[2]
Yeye ndiye aliye mpeleka Mtume kwenye watu wasio jua kusoma, awasomee Aya zake na awatakase, na awafunze Kitabu na hikima, ijapo kuwa kabla ya haya walikuwa katika upotofu ulio dhaahiri.
Alama nyengine iliyoleta furaha katika maisha ya watu ni kuweka mipaka ya Mwenyeezi Mungu, na Mitume ilisisitiza kutii amri zake Allah (s.w), miongoni mwa mipaka hiyo ni kuhusiana na hukumu za Mwenyeezi Mungu, kwa mfano ndani ya Qur-ani kuhusu kisasi tunasoma hivi:-

وَلَكُمْ فِى الْقِصَاصِ حَيَاةٌ يَاْ اُولِيْ الاَلْبَابِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ[3]

Mtakuwa nao uhai mzuri katika kulipiza kisasi enyi wenye akili, ili msalimike.
*Watakuwa na uhai mzuri kwa sababu kila mtu atakaa kwa adabu yake, kwani anajua kuwa akiua atauawa na akidhuru na yeye atafikishiwa madhara, katika kujikimbiza madhara nafsi yake yanakimbizika hayo madhara kwa watu wengine.
Natija tunayoipata katika maelezo hayo ni kwamba, mwanaadamu anatakiwa kuishi kwa kutii amri za Mola wake, na kufuata dasturi na miongozo ya Mitume yake, na ni njia hii tu
itakayomuwezesha mwanaadamu kuishi katika maisha mema na kufikia katika saada. Kama Qur-ani inavyosema:-
يَا اَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ اسْتَجِيبُواْ لِلّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُم لِمَا يُحْيِيكُمْ وَاعْلَمُواْ اَنَّ اللّهَ يَحُولُ بَيْنَ الْمَرْءِ وَقَلْبِهِ وَاَنَّهُ إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ[4]
Enyi mlio amini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapo kuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu huingia kati ya mtu na moyo wake, na kwamba hakika kwake Yeye tu mtakusanywa.

*Wanafahamishwa viumbe wote kuwa kila analowaitia Mtume ni la kheri yao viumbe vyote duniani na Akhera, na wanafaahamishwa nguvu za Mwenyeezi Mungu kuwa anaweza kufanya atakavyo, na juu ya hivi hawafanyii waja wake ila ya kheri tu.

[1] Surat Tawba Aya ya 100

[2] Surat Jumua Aya ya 2

[3] Suratul Baqarah Aya ya 179

[4] Surat Al-Anfaal Aya ya 24

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini