Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

ATHARI NJEMA BAADA YA UTUME NO.3

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

ATHARI NJEMA BAADA YA UTUME NO.3

* Mapinduzi ya Mitume yalileta athari gani katika jamii?.

BAADA YA KUBASHIRIWA UTUME

Mapinduzi ya Mitume hayakuwa na harakati zisizokuwa na malengo, bali yalikuwa ni hadafu na madhumuni ya juhudi zilizofanywa kwa ajili ya kufikia katika malengo maalumu, nayo ni kusuluhisha jamii, na kuwatakasa watu wa jamii nzima duniani.

Hapana shaka kuwa Mitume imeteuliwa miongoni mwa watu.

Katika makala iliyopita tulielezea athari njema zenye baraka zilizojitokeza baada ya Mitume kubashiriwa utume, katika makala hii tutaelezea athari nyengine, miongoni mwa hizo ni:

2. KUJENGA UMOJA NA KUONDOA HITILAFU

Mitume ilifanya jitihada sana ili kujenga umoja ulio thabiti na kuondoa hitilafu miongoni mwa watu, kwa sababu baadhi ya wakati katika jamii unaweza ukaonekana umoja kidhahiri tu, na baada ya muda mfupi umoja huo ukaondoka, umoja ambao ulitokana na mipaka ya fikra za watu au maisha waliyokuwa wakiishi, au ulitokana na mapendeleo yao ya kimoyo, kama inavyoonekana kwa watu wa mwanzo ambao walijenga umoja kutokana na sababu hizo au nyenginezo, lakini baada ya watu hao kukua kifikra, walijiwa na masuala tofauti akilini mwao, na wakaingiwa na hadafu na madhumuni tofauti ambazo zilileta athari katika nyoyo zao, hatimae kutokana na fikra walizokuwa nazo zilisababisha kuleta hitilafu baina yao, kama tunavyoshuhudia ndani ya Qur-ani:-

وَمَا كَانَ النَّاسُ إِلاَّ اُمَّةً وَاحِدَةً فَاخْتَلَفُواْ وَلَوْلاَ كَلِمَةٌ سَبَقَتْ مِن رَّبِّكَ لَقُضِيَ بَيْنَهُمْ فِيمَا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ[1]

Wala watu hawakuwa ila Umma mmoja tu. Kisha wakakhitalifiana. Na lau kuwa si neno lililo kwisha tangulia kutokana na Mola wako Mlezi, hapana shaka hukumu ingeli kwisha katwa baina yao katika hayo wanayo khitalifiana.

*Ubaya wao zaidi ni kuwa wanapokhitalifiana hivyo, wakaletewa Mitume wa kuwatoa katika hizo khitilafu na kuwaongoa, hawakubali kufuata, hushika pale pale walipo.

Mwenyeezi Mungu aliituma Mitume yake ili kuja kuondoa khitilafu zilizokuwepo miongoni mwa watu, na kuanzia zama za Nabii Nuhu (a.s) aliituma Mitume na kuwapa sheria zake ili awabashirie watu mabashirio mema au kuwatia hofu na adhabu ya Siku ya Kiama, ili waokoke na maisha ya kijahilia waliyokuwa wakiishi, na Mitume hiyo kwa kuwabainishia watu uhakika na kuwaonyesha njia iliyo haki na kuwapa kasha lenye thamani na lenye elimu itakayowasaidia wao kifikra na kimaarifa, na kwa sababu hiyo basi Mitume iliwanufaisha watu na kuwataka kujenga umoja utakaokuwa thabiti katika jamii yao, kama inavyosema Qur-ani:-

كَانَ النَّاسُ اُمَّةً وَاحِدَةً فَبَعَثَ اللّهُ النَّبِيِّينَ مُبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ وَاَنزَلَ مَعَهُمُ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ لِيَحْكُمَ بَيْنَ النَّاسِ فِيمَا اخْتَلَفُواْ فِيهِ وَمَا اخْتَلَفَ فِيهِ إِلاَّ الَّذِينَ اُوتُوهُ مِن بَعْدِ مَا جَاءتْهُمُ الْبَيِّنَاتُ بَغْياً بَيْنَهُمْ فَهَدَي اللّهُ الَّذِينَ آمَنُواْ لِمَا اخْتَلَفُواْ فِيهِ مِنَ الْحَقِّ بِإِذْنِهِ وَاللّهُ يَهْدِى مَن يَشَاءُ إِلَي صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ[2]

Watu wote walikuwa ni umma mmoja. Mwenyezi Mungu akapeleka Manabii wabashiri na waonyaji. Na pamoja nao akateremsha Kitabu kwa Haki, ili kihukumu baina ya watu katika yale walio khitalifiana. Na wala hawakukhitalifiana ila wale walio pewa Kitabu hicho baada ya kuwafikia hoja zilizo wazi, kwa sababu ya uhasidi baina yao. Ndipo Mwenyezi Mungu kwa idhini yake akawaongoa walio amini kwendea haki katika mambo waliyo khitalifiana. Na Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye kwenye Njia Iliyo Nyooka.

Vile vile baadhi ya wakati, katika jamii kutokana na fikra tofauti walizonazo au kutokana na kujitokeza makundi tofauti ya watu ambayo yanaweza kuleta fikra ya kujenga umoja na kuleta utulivu katika jamii yao, na kila mtu akawa ameshhughulika na maisha yake yeye mwenyewe, wakawa pamoja na kushirikiana katika kufanya mambo yao ya ibada, lakini vile vile umoja wa aina hii ni wa kupita na wa mara moja tu, kiasi ya kwamba kama patatokea matatizo katika jamii na akatafutwa msuluhishaji ambaye atakuwa ni miongoni mwao, hapana shaka patadhihirika watu ambao ni wenye kutaka manufaa yao wenyewe na watahukumu kutokana na matamanio yao ya kibinafsi, na kwa sababu hiyo basi kutatokea khitilafu za kila aina, kama Qur-ani inavyoashiria uhakika huo:-

إِنَّ الدِّينَ عِندَ اللهِ الإِسْلاَمُ وَمَا اخْتَلَفَ الَّذِينَ اُوْتُواْ الْكِتَابَ إِلاَّ مِن بَعْدِ مَا جَاءهُمُ الْعِلْمُ بَغْياً بَيْنَهُمْ وَمَن يَكْفُرْ بِآيَاتِ اللهِ فَإِنَّ اللهِ سَرِيعُ الْحِسَابِ[3]

Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu. Na walio pewa Kitabu hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa sababu ya uhasidi ulio kuwa baina yao. Na anaye zikataa Ishara za Mwenyezi Mungu basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.

Kutokana na maelezo tuliyoyaelezea tumefahamu kuwa, kabla ya kuletwa Mitume katika jamii ya watu kulikuwa na khitilafu, na baadhi ya khitilafu zilitokea hata baada ya kuja Mitume pia, lakini chanzo cha khitilafu zote hizo ni kwa sababu watu hawakuwa na elimu ya kutosha, na wengi wao walikuwa ni madhalimu wanaofanya mambo kutokana na  matamanio yao ya kibinafsi, kwa hiyo sababu zinazofanya umoja uthibiti ni kuwa na elimu na imani iliyo madhubuti, na Mitume ya Mwenyeezi Mungu imekuja kufikisha ujumbe wa Mwenyeezi Mungu na kuwalingania watu katika dini ya Mwenyeezi Mungu, vile vile kuondosha khitilafu walizonazo, na watakaofaidika na umoja huo ni Waumini tu, makafiri na wanafiki siku zote watakuwa katika mashaka ya kukhitilafiana na  kugawanyika, kama anavyosema Allah (s.w):-

لاَ يُقَاتِلُونَكُمْ جَمِيعاً إِلاَّ فِى قُرًى مُّحَصَّنَةٍ اَوْ مِن وَرَاء جُدُرٍ بَاْسُهُمْ بَيْنَهُمْ شَدِيدٌ تَحْسَبُهُمْ جَمِيعاً وَقُلُوبُهُمْ شَتَّي ذٰلِكَ بِاَنَّهُمْ قَوْمٌ لاَّ يَعْقِلُونَ[4]

Hawatapigana nanyi kwa mkusanyiko isipo kuwa katika vijiji vilivyo zatitiwa kwa ngome, au nyuma ya kuta. Wao kwa wao vita vyao ni vikali. Utawadhania kuwa wako pamoja, kumbe nyoyo zao ni mbali mbali. Hayo ni kwa kuwa wao ni watu wasio na akili.

[1] Surat Yunus Aya ya 19

[2] Suratul-Baqarah Aya ya 213

[3] Surat Al-Imrani Aya ya 19

[4] Suratul-Hashr Aya ya 14

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini