Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

KUBASHIRIWA UTUME

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

KUBASHIRIWA UTUME NO.1

* Mapinduzi ya Mitume yalileta athari gani katika jamii?.

BAADA YA KUBASHIRIWA UTUME

Mapinduzi ya Mitume hayakuwa na harakati zisizokuwa na malengo, bali yalikuwa ni hadafu na madhumuni ya juhudi zilizofanywa kwa ajili ya kufikia katika malengo maalumu, nayo ni kusuluhisha jamii, na kuwatakasa watu wa jamii nzima duniani.

Hapana shaka kuwa Mitume imeteuliwa miongoni mwa watu, kwa kuzingatia Aya hii:-

لَقَدْ مَنَّ اللّهُ عَلـٰي الْمُؤمِنِينَ إِذْ بَعَثَ فِيهِمْ رَسُولاً مِّنْ اَنفُسِهِمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِهِ وَيُزَكِّيهِمْ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَإِن كَانُواْ مِن قَبْلُ لَفِى ضَلالٍ مُّبِينٍ[1]

Hakika Mwenyezi Mungu amewafanyia wema mkubwa Waumini vile alivyo waletea Mtume aliye miongoni mwao wenyewe, anaye wasomea Aya zake, na anawatakasa, na anawafunza Kitabu na hikima, ijapo kuwa kabla ya hapo walikuwa katika upotovu ulio wazi.

Maelezo kuhusiana na Aya.

Hapa Mwenyeezi Mungu anawakumbusha waislamu neema kubwa aliyowapa- ya kuwaletea Mtume, na kuonyesha kuwa walikuwa katika upotevu mkubwa, na sasa wameingia katika uongofu mkubwa mno kabisa.

Lakini kwa kuthibiti kauli za Mitume katika jamii, na juhudi za viongozi wa kidini zilikuwa na athari na faida kiasi ya kwamba waliweza kuleta mabadiliko makubwa katika jamii, na athari zao hizo zenye baraka zinaonekana katika kipindi kirefu, na zimebakia kitarekhe.

Baada ya kuja Mitume, watu ambao walikuwa wakiabudu masanamu na waliopotoka na kupotea kwa kufuata sunna za kijahilia walizinduka, na hata wengine walikubali kufuata njia za Mitume hiyo baada ya kujiona kuwa hawakuwa katika mwenendo sahihi, kama inavyosema Qur-ani:-

وَجَاء مِنْ اَقْصَي الْمَدِينَةِ رَجُلٌ يَسْعَي قَالَ يَا قَوْمِ اتَّبِعُوا الْمُرْسَلِينَ[2]

Na akaja mtu mbio kutokea upande wa mbali wa mjini, akasema: Enyi watu wangu! Wafuateni hawa walio tumwa.

* Wafuateni hawa walio tumwa – yaani wafuatwe Mitume - Na vile vile kwa wale ambao walikuwa wakitafuta uhuru wao na wamechoka na dhulma na kutokuwepo uadilifu, kwa watu madhalimu waliokuwa wametawala zama hizo, kwa kuja Mitume waliweza kupigania haki na uhuru wao. Kwa mfano;Baadhi ya watu wa Bani Israel walikubali kufuata desturi za Mtume wao, wakiwa chini ya uongozi wa - Taluti - walisimama kidete na kuwa madhubuti kwa kukabiliana na jeshi la – Jaluti – pale Qur-ani iliposema:-

فَهَزَمُوهُم بِإِذْنِ اللهِ وَقَتَلَ دَاوُودُ جَالُوتَ وَآتَاهُ اللّهُ الْمُلْكَ وَالْحِكْمَةَ وَعَلَّمَهُ مِمَّا يَشَاءُ وَلَوْلاَ دَفْعُ اللهِ النَّاسَ بَعْضَهُمْ بِبَعْضٍ لَّفَسَدَتِ الاَرْضُ وَلَـكِنَّ اللّهَ ذُو فَضْلٍ عَلـٰي الْعَالَمِينَ[3]

Kwa idhini ya Mwenyezi Mungu waliwatimua, na Daudi akamuuwa Jaluti, na Mwenyezi Mungu akampa Daudi ufalme na hikima, na akamfundisha aliyo yapenda. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hawapambanishi watu kwa watu basi dunia ingeli haribika. Lakini Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya walimwengu wote.

*Nabii Daudi alikuwa ni askari katika hilo jeshi la Mfalme Taluti. Akapigana kwa nia nzuri na ushujaa mkubwa kabisa, hata akamuuwa mfalme wa hao maadui (makafiri), aliyekuwa akiitwa Jaluti,basi Mwenyeezi Mungu akampa Utume na Ufalme na mengineyo kwa hayo aliyofanya.

Kwa upande mwengine, kwa wale waliokuwa wamedhulumiwa wakiwa mateka chini ya viongozi hao wa kidhalimu, walipoona wamepata maficho na kujitetea kutokana na dhulma waliyokuwa wakifanyiwa, kwa mategemeo waliwaelekea Mitume na kuwaambia:-

وَمَا لَكُمْ لاَ تُقَاتِلُونَ فِى سَبِيلِ اللهِ وَالْمُسْتَضْعَفِينَ مِنَ الرِّجَالِ وَالنِّسَاء وَالْوِلْدَانِ الَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا اَخْرِجْنَا مِنْ هَـذِهِ الْقَرْيَةِ الظَّالِمِ اَهْلُهَا وَاجْعَل لَّنَا مِن لَّدُنكَ وَلِيّاً وَاجْعَل لَّنَا مِن لَّدُنكَ نَصِيراً[4]

Na mna nini msipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu na ya wale wanao onewa, wanaume na wanawake na watoto, ambao husema: Mola Mlezi wetu! Tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhaalimu, na tujaalie tuwe na mlinzi anaye toka kwako, na tujaalie tuwe na wa kutunusuru anaye toka kwako.

*Baada ya kuhama Mtume Makka walisalia baadhi ya Waislamu – wanaume na wanawake na watoto – wameadhibiwa na jamaa zao na kufungwa ndindindi, hawawezi kukimbia wakaja Madina.

Na wanadhiliwa na kutaabishwa kweli kweli, basi wanahimizwa Waislamu vikitokea vita wapigane kweli kweli na hao makafiri mpaka waweze kuwaokoa hao Waislamu wanaotaabishwa hivyo.

Basi Waislamu wa kweli wakayafuata haya, wakapigana hata wakaitia Makka mikononi mwao. Akatawalishwa liwali wa kiislamu akawatoa taabuni wale Waislamu waliokuwa wakitaabishwa na kuomba vile, dua ilisibu baada ya amri kufuatwa.

Watu baada ya kuona mafanikio katika mapinduzi waliyoyafanya Mitume waliingia katika dini ya Mwenyeezi Mungu makundi kwa makundi, kama alivyoashiriwa katika surat Nasr, pale Allah (s.w) aliposema:-

إِذَا جَاء نَصْرُ اللهِ وَالْفَتْحُ. وَرَاَيْتَ النَّاسَ يَدْخُلُونَ فِى دِينِ اللهِ اَفْوَاجاً[5]

Itakapo kuja nusura ya Mwenyezi Mungu na ushindi.

Na ukaona watu wanaingia katika Dini ya Mwenyezi Mungu kwa makundi,Natija tunayoipata katika maelezo hayo ni kwamba; kwa kuteuliwa Mitume kulisababisha harakati katika jamii, harakati ambazo ziliwafanya wale ambao waliojitakasa nafsi zao na wenye kutafuta haki kukubali kuwafuata Mitume, na kujenga umoja. Na kwa upande mwengine madhalimu walisimama kidete kukabiliana na waislamu ili kubadilisha sunna za Kiislamu walizokuja nazo Mitume,lakini kwa uweza wake Allah (s.w) hawakufanikiwa na waliyokuwa wakiyataka, - yaani kuzibadilisha sunna za Allah (s.w) - kwani ni jambo lililowazi kabisa kuwa sunna za Mwenyeezi Mungu haziwezi kubadilishwa, na Mwenyeezi Mungu siku zote huwasaidia Waumini na Waislamu kukabiliana na makafiri, kama anavyosema allah (s.w) kuelezea mafanikio ya Mitume:-

وَلَقَدْ كُذِّبَتْ رُسُلٌ مِّن قَبْلِكَ فَصَبَرُواْ عَلـٰي مَا كُذِّبُواْ وَاُوذُواْ حَتَّي اَتَاهُمْ نَصْرُنَا وَلاَ مُبَدِّلَ لِكَلِمَاتِ اللهِ وَلَقدْ جَاءكَ مِن نَّبَإِ الْمُرْسَلِينَ[6]

Na hakika walikanushwa Mitume wa kabla yako. Nao wakavumilia kule kukanushwa, na kuudhiwa, mpaka ilipo wafikia nusura yetu. Na hapana wa kubadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu. Na bila ya shaka zimekujia baadhi ya khabari za Mitume hao.   

Mwenyeezi Mungu huwapa Mitume yake cheo cha Utume baada ya kufahamu hali ya jamii ilivyo, na katika kipindi chote hiki cha tarekhe tumeshuhudia kuwa Mwenyeezi Mungu hatarajii lolote kutoka kwa waja wale isipokuwa baada ya kuwaongoza , kuwaonya au kuwataka wazingatie ibra kutoka umati uliopita, kwani kwa kufanya hivyo huwafanya waumini kuweza kupambanua haki na batili, na huweza kukabiliana na tabu na mashaka kutokana na fadhila na rehema zake Allah (s.w).

وَكُـلاًّ نَّقُصُّ عَلَيْكَ مِنْ اَنبَاء الرُّسُلِ مَا نُثَبِّتُ بِهِ فُؤَادَكَ وَجَاءكَ فِى هَـذِهِ الْحَقُّ وَمَوْعِظَةٌ وَذِكْرَي لِلْمُؤْمِنِينَ[7]

Na yote tunayo kusimulia katika khabari za Mitume ni ya kukupa nguvu moyo wako. Na katika haya imekujia haki na mawaidha na ukumbusho kwa Waumini.

* kusikia yaliyowapata wengine na natija nzuri iliyopatikana kunashajiisha moyo, ndiyo maana Mwenyeezi Mungu akakithirisha kutaja visa vya wema na vya wabaya, tusione kuwa sisi tumeonewa.

[1] Surat Al-Imrani aya ya 164

[2] Surat yaasin Aya ya 20

[3] Suratul-Baqarah Aya ya 251

[4] Suratun –Nisaa Aya ya 75

[5] Surat Nasr Aya ya 1-2

[6] Surat Al-An-aam Aya ya 34

[7] Surat Hud Aya ya 120

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini