Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

UTAKASO WA MAIMAMU NO.3

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
UTAKASO WA MAIMAMU (A.S) NO.3
ISMAH YA IMAMU.
Moja katika sifa na sharti muhimu zinazomuwajibikia Imam kuwa nazo ni ismati, (ismati yaani kuepukana na maovu na kutofanya madhambi).
Imamu anatakiwa kuwa ni mwenye elimu ya hali ya juu ili aweze kuwaongoza wengine, na kwa sababu mbili hizi (yaani kutokufanya madhambi na kuwa na elimu ya hali ya juu) Imamu hujizuia na kuitakasa nafsi yake na maovu, na kujiepusha kufanya madhambi, basi kwa vile Imamu ni mwenye kuelewa na kufafanua masuala ya dini, yeye ndie anayefahamu vipi tunatakiwa kuyafanyia kazi masuala hayo, na huyapambanuwa yale yenye kuleta maslahi na yenye kuleta ufisadi na upotovu katika jamii ya kiislamu.
Kuna dalili tofauti za kuthibitisha kwamba Imamu ameepukana na maovu na wala sio mwenye kufanya madhambi, na dalili hizo tunazishudia katika Qur-ani tukufu au katika hadithi tofauti zilizonakiliwa kutoka kwa Mtume Wetu Muhamad (s.a.w.w).
DALILI ZINAZOTHIBITISHA KUWA IMAMU NI LAZIMA ACHAGULIWE NA ALLAH (S.W)
1.Allah (s.w) katika qur-ani anasema kwamba yeye ndie Hakimu wa kila kitu, na viumbe wote ni lazima wamtii Mola wao, kwa hivyo kwa maelezo hayo inadhihirika wazi kwamba kutokana na hekima za Mola wetu yeye ndie anayeelewa nani anaweza kuwa Imamu na kuwaongoza wengine katika njia iliyo sahihi, basi kwa sababu Mtume Muhammad (s.a.w) amechaguliwa na Mola Imam pia ni lazima achaguliwe na Mola.

2.Hapo mwanzo tulielezea kwamba moja katika sheria ambazo anatakiwa Imam kuwa nazo ni elimu na aepukane na maovu na madhambi,na hakuna mtu yoyote anayeelewa ni nani mwenye sifa hizo isipokuwa Mola, kwa sababu Mola ndie anaejuwa kila la dhahiri na batini (yaani anamjua binaadamu undani wake, na nje yake) . Allah (s.w) katika suratul-baqara aya ya 124 anasemakumwambia Nabii Ibrahim "mimi nimekuchaguwa kuwa Imam wa Wanaadamu".

Mwisho wa mazungumzo haya ni vizuri kama tutaelezea tabia njema za Imam wa nane hadharati Ridhaa (a.s) ambaye ameelezea kwa uzuri sifa za Imamu.

Watu ambao wana shaka na wameleta ikh-tilafu (yaani wamehitilafiana) katika masuala ya Imamu na wanasema kwamba watu wenyewe wanaweza kumchaguwa Imamu na kwamba Imamu hachaguliwi na Mola watu hao hawana elimu, kwa sababu hawaelewi Imamu mbele ya Allah ana umuhimu gani, na wao hawana hiyari ya kumchagua mtu yoyote wanayemtaka kuwa Imamu wao.

Imam ni mwenye kudra (yaani ni mwenye nguvu) za hali ya juu kabisa, kielimu,? Imam ni sehemu ambayo Allah (s.w) baada ya kufariki Mtume (s.a.ww)amewachaguwa watu wengine kuwa ni viongozi katika dini ya kiislamu, Imam ni khalifa wa Allah, na ni khalifa wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) na ni sehemu ya Imamu Aliy, na ni urithi wa Imamu Hassan na Imam Hussein (a.s) Imam ni nguzo ya dini, na nidhamu ya waislamu, na ni maslahi katika dunia, na ni utukufu walionao waumini, kukamilika kwa sala, funga,Hija, jihadi yote haya yatakamilika ikiwa wanaadamu watamkubali Imamu wao.

Kila kitu ambacho Mola amekiharamisha Imam anakiharamisha ni kila kitu ambacho Mola amekihalalisha Imam anakihalalisha, na Imamu anahukumu vile ambavyo Mola ameamrisha, anafanya himaya katika dini ya Mola wake, ni mwenye kutumia hekima na mawaidha katika kuwaongoza watu katika njia ya Mola wake.

Imam ni mfano wa jua ambalo nuru yake inamurika dunia nzima,Imam ni mfano wa mwezi ambao unang'aa, na ni mfano wa taa yenye nuru ambayo inamurika, na ni nyota ambazo wakati kukiwa kiza zinaongoza katika njia, bahari, na sehemu tofauti. basi Imamu humuokowa mwanaadamu katika fitna na ujahili.

Imamu ni kama baba ambaye ana mapenzi, na ni kama kaka katika familia, na ni kama mama ambaye ni mwenye mapenzi na mtoto wake mdogo, Imam ni mtu ambaye ametakasika na kila maovu na ameepukana na madhambi na kila aibu, Imamu ni mwenye elimu, Imam katika zama zake ni mmoja tu (yaani haiwezekani katika zama moja kuwa na Imamu zaidi ya mmoja). hakuna mtu atakaedai madai ya uongo na kusema yeye ni Imam, na hakuna mtu atakaedai kuwa ana elimu zaidi ya Imam, hakuna mtu atakayejifananiza na Imam kwa kitu chochote.

Basi kuna mtu gani anaweza kumuelewa Imam na sifa alizonanzo , au kuna watu gani watakaoweza kumchagua Imam kwa sifa ambazo Mola ameamrisha Imam kuwa nazo? kuna watu wangapi waliojidai kuwa na elimu zaidi ya Imam na wameshindwa, kuna watu wangapi waliokuwa wakubwa na wenye vyeo lakini mbele ya Imamu wametahayari, na kuna wangapi waliojifanya wana hekima lakini mbele ya Imam hawakuwa chochote, basi kuna mtu gani anaweza kumsifu na kumjuwa Imam na fadhila zake?

Watu wote waliokuwa na nguvu na walio dhaifu, wenye vyeo na hekima wamesalenda mbele ya Imamu.

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini