Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

FAIDA ZA KUTOWEKA IMAMU MUOKOZI NO3

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
FAIDA ZA KUTOWEKA IMAMU MUOKOZI NO.3

KUJITAKASA.
Qur-ani kariym inasema:- "Na sema (uwaambie): "tendeni mambo (mazuri). Mwenyeezi Mungu atayaona mambo yenu hayo na Mtume wake na Waislamu. Na mtarudishwa kwa Mjuzi wa siri na dhahiri; naye atakwambieni (yote) mliyokuwa mkiyatenda[1]." Katika hadithi imeelezewa kwamba neno Muu-mini katika aya hii ni Maimamu[2].

Kutokana na maelezo ya hapo juu imeeleweka wazi kwamba Imam anaona amali au matendo ya watu ambayo wanayafanya, na kwa sababu hii basi kuna faida kubwa kwa watu kujihadhari na amali (matendo) mabaya ambayo wanayafanya, kwa kuelewa kuwa Imamu wao anayaona matendo hayo, na hii inapelekea kujirekebisha na matendo mabaya, na kufanya matendo mema. Jambo la muhimu ni kwamba kila mwanaadamu anatakiwa ajilinde na kufanya matendo mabaya na aitakase nafsi yake kwa kufanya matendo mema.

KITUO CHA KIELIMU NA KIFIKRA.

Maimamu ndio walimu wa mwanzo na wa asili katika dunia, na siku zote watu walikuwa wakifaidika na elimu pamoja na mafunzo yao, katika kipindi alichotoweka Imam Mahdi watu walikuwa hawawezi kuwasiliana na Imamu wao na kutatuliwa matatizo yao, tofauti na Maimamu waliopita, lakini tatizo hili halikupelekea watu washindwe kutafuta elimu na kupata mafunzo ya dini yao,bali walitumia njia nyengine mbali mbali ili kujifunza mafunzo hayo, katika kipindi kifupi ambacho Imam alitoweka watu walitumia njia ya barua kwa kuwapa Naibu wao, na kuuliza masuala, na Imam aliwajibu kwa barua na baadae kuwapa barua hizo Naibu zao.

Bwana Is-haka aliuliza suala kwa Imam Mahdiy.

Imam Mahdiy alimjibu suala hilo kwa njia ya barua, na jawabu yake ilikuwa kama hivi ifuatavyo:-Mwenyeezi Mungu akuongowe na uwe thabiti katika imani na dini yako. Ama kuhusu suala ulilouliza ya kwamba Ami zetu (au watu wa familia yetu) na baadhi ya watu katika ukoo wetu ni wenye kupinga amri zetu, elewa kwamba mbele ya Allah (s.w) hakuna umuhimu katika ukoo, (yaani ikiwa mtu mmoja katika ukoo wa Imam ni mwenye kupinga amri ya Mola wake Mwenyeezi Mungu hamuangalii mtu huyo kwa kuwa ni katika ukoo wa Imam akampa cheo na kufumbia macho uovu anoufanya mtu huyo).Na matokeo yake mtu huyo yatamkuta kama yaliyomkuta mtoto wa Nabii Nuh. Ama kuhusu mali ambazo mnazituma kama hazitakuwa za halali sitazipokea. na tutapokea mali ambazo ni za halali.

Basi mtu yoyote atakayejihalalishia mali zetu na kuzitumia mali hizo bila ya idhini yetu sisi, itakuwa ni sawa na aliyekula moto, ama kuhusu vipi utafaidika na mimi katika dunia ni kwamba,kuwepo kwangu katika dunia ni kama jua na nuru (muangaza), na mimi ndiye ninayeleta amani katika dunia, mfano wa nyota zinavyoleta amani katika mbingu, na usiulize masuala ambayo hayana faida nawe, na usijitie mashakani kujifunza masuala ambayo hujalazimishwa kuyajua, na omba dua kwa wingi ili nidhihiri haraka. Salamu kwako wewe bwana Is-haka bin yaaqub, na salamu kwa watu wote ambao ni wenye kufuata haki na wanaotaka kuongoka.

Baada ya kutoweka Imam Mahdi kwa muda mfupi Maulamaa wa kishia walikuwa wakimuuliza Imam masuala ya kielimu, na kifira na matatizo mengi mengine na Imamu alikuwa akiwajibu kwa njia ya barua kupitia Naibu wake.

Mmoja katika wanafunzi wa Ur-dibiyly ajulikanaye kwa jina la Miyri Ul-laam anasema:- "Siku moja mnamo saa sita za usiku alikuwa katika jengo ambalo amezikwa Imam Aliy (a.s). Baada ya muda mfupi akamuona mtu anaelekea katika jengo hilo, wakati alipomsogelea aligundua kuwa ni mwalimu wake Sheikh Ahmad Muqadasi Ur-dibiyly, baada ya kufahamu kuwa ni yeye akajificha, mlango wa jengo hilo ulikuwa umefungwa lakini baada ya mwalimu wake kufika mlangoni mwa jengo hilo mlango ulifunguka wenyewe na yeye akaingia ndani ya jengo hilo, na baada ya muda mfupi alitoka kuelekea upande wa mji wa Kufe, naye akamfuata hali ya kuwa hana habari, hadi akafika katika msikiti wa Kufe, akaingia ndani ya Msikiti na kwenda katika kaburi la Imam Aliy (a.s), akabakia kwa muda na baadae akatoka kuelekea katika mji wa Najaf, naye akaendelea kumfuata hadi kufika katika Msikiti wa Hinana, akaenda chafya na mwalimu wake akasikia sauti hiyo wakati alipogeuka nyuma akamuona kuwa ni mwanafunzi wake, akamuuliza unafanya nini usiku huu ? naye akamjibu kuwa alikuwa anamfata nyuma nyuma toka katika jengo ambalo amezikwa Imam Aliy. Miyri Ul-aam akaapa na kumuomba mwalimu wake ampe siri ya aliyoyaona katika usiku huo.

Mwalimu wake akasema "Ntakwambia lakini kwa masharti" na sharti yake ilikuwa hii:-

Toka wakati atakapokuwa hai asimwambie mtu siri hiyo, naye akakubali sharti hiyo.

Akamwambia kila wakati nnapokutwa na matatizo na nikawa siwezi kuyatatua huja katika kaburi la Imam Aliy na kumuomba anisaidie kutatua matatizo yangu, na usiku wa leo nimepata matatizo ndipo nikaamua kuja katika kaburi la Imamu, nawe umeshuhudia nilipofika mlango ulikuwa umefungwa ,lakini ulifunguka nami nikaingia ndani nikaomba mahitaji yangu na Imam Aliy amenitatulia. baada ya muda nikasikia sauti ambayo iliniamuru niende katika Msikiti wa mji wa Kufe nikaulize suala langu kwa Imam Mahdiy, nami nikauliza suala langu na Imam akanijibu suala langu na sasa narejea nyumbani kwangu[3].

[1] Suratu-At-Tawba aya ya 105.

[2] Rejea katika kitabu cha Kaafi, juzuu ya kwanza, mlango wa aradhil-aamali, ukurasa wa 171.

[3] Rejea kitabu Buharul-an-war, juzuu ya 52, ukurasa wa 174

(4). Rejea kitabu Kamalu din, juzuu ya 2,mlango wa 48, ukurasa wa 235 hadi 28
MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini