Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

SIFA ZA WATIIFU NO.1

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

SIFA ZA WATIIFU NO.1

WAFUASI WAKWELI WA MITUME

* Ni alama gani zinazoonesha ukweli wa wafuasi wa Mitume?.

* Kuna athari gani katika kuwakubali na kuwafuata Mitume?.

Katika makala iliyopita tulielezea kuhusu wafuasi wa kweli wa Mitume ya Mwenyeezi Mungu (s.w) na sifa walizonazo watiifu hao. katika makala hii tutaendelea kuelezea sifa nyengine walizonazo watu hao.

Mwenyeezi Mungu akielezea kuhusiana na Waumini na watiifu wa kweli, ambao wako katika rehema zake Yeye Allah (s.w), anasema:-

يَا اَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ مَن يَرْتَدَّ مِنكُمْ عَن دِينِهِ فَسَوْفَ يَاْتِى اللّهُ بِقَوْمٍ يُحِبُّهُمْ وَيُحِبُّونَهُ اَذِلَّةٍ عَلـٰي الْمُؤْمِنِينَ اَعِزَّةٍ عَلـٰي الْكَافِرِينَ يُجَاهِدُونَ فِى سَبِيلِ اللهِ وَلاَ يَخَافُونَ لَوْمَةَ لآئِمٍ ذٰلِكَ فَضْلُ اللهِ يُؤْتِيهِ مَن يَشَاءُ وَاللّهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ[1]

Enyi mlio amini! Atakaye iacha miongoni mwenu Dini yake, basi Mwenyezi Mungu atakuja leta watu anao wapenda nao wanampenda, wanyenyekevu kwa Waumini na wenye nguvu juu ya makafiri, wanapigania Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawaogopi lawama ya anaye laumu. Hiyo ndiyo fadhila ya Mwenyezi Mungu, humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu na Mwenye kujua.

*Wanatiwa nguvu Waislamu kuwa wasivunjike nyoyo wakiona baadhi ya waliosilimu wanatoka Uislamuni, kwani Mwenyeezi Mungu atawaleta mabora kuliko hao waliritadi, na ambao watakuwa na sifa za Uislamu khasa, na akazitaja Mwenyeezi Mungu katika hii Aya ya 54, 55,56, baadhi ya sifa za Waislamu wa kweli, basi natujitahidi nazo mwisho wa jitihada yetu.

2. Athari zinazopatikana kwa kumtii Mwenyeezi Mungu na Mitume yake, na hatima ya watiifu hao.

Kumtii Mwenyeezi Mungu na Mitume yake, na kukubali yale wanayoamrisha, kunaleta athari na faida nyingi duniani na akhera, miongoni mwa hizo ni kama hizi zifuatazo:-

2-1. Kuondoa khitilafu za kielimu na za kimatendo.

Katika jamii kuna wataalamu wa kielimu, ambao wanakhitilafiana katika masula mbali mbali, yakiwemo masuala ya kiitikadi, ahkamu, n.k. na kila mmoja katika wataalamu hao hutoa dalili zake ili kuthibitisha ile nadharia yake au jambo ambalo ana itikadi nalo. Lakini pale ambapo Mitume wanabainisha jambo kutokana na elimu ambayo wamepewa na Mola wao, watu wote hupata uhakika wa lile jambo ambalo walikuwa wamekhitilafiana nalo kielimu, kama anavyosema Nabii Issa (a.s):-

وَلَمَّا جَاء عِيسَي بِالْبَيِّنَاتِ قَالَ قَدْ جِئْتُكُم بِالْحِكْمَةِ وَلِاُبَيِّنَ لَكُم بَعْضَ الَّذِى تَخْتَلِفُونَ فِيهِ فَاتَّقُوا اللهَ وَاَطِيعُونِ[2]

Na alipo kuja Isa na dalili zilizo wazi, alisema: Nimekujieni na hikima, na ili nikuelezeni baadhi ya yale mliyo khitalifiana. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na mnit'ii mimi.

Vile vile katika kujenga uhusiano au katika mambo ambayo yanataka uamuzi kuzingatia jamii ilivyo, kuna watu ambao kila mmoja hutafuta na kuamua lile lenalomletea manufaa na maslahi yake binafsi, bila ya kufikiria hali ya watu wengine, katika hali ambayo pindi wakirejea kwa Mitume, Mitume huwaongoza na kuwaonyesha njia ya uamuzi ambao utawaletea kheri wote, na jamii itaishi katika amani na usalama. kama anavyosema Allah (s.w):-

يَا اَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ اَطِيعُواْ اللّهَ وَاَطِيعُواْ الرَّسُولَ وَاُوْلِى الاَمْرِ مِنكُمْ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِى شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَي اللهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ ذٰلِكَ خَيْرٌ وَاَحْسَنُ تَاْوِيلاً[3]

Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema.

*Kila wenye kutawalishwa ukubwa inataka watiiwe maadamu wanayoamrishwa ndiyo sahihi, ikiwa hapana kiongozi wa kutiiwa mambo yatakuwa ovyo ovyo, na patatokea fujo, na Uislamu haupendi mambo ovyo ovyo, wala haupendi dhulma na jeuri. Basi viongozi (wa kidini) watiiwe maadamu wanaamrisha mambo yaliyo ndivyo. Wakiamrisha yaliyo siyo hapana ruhusa kutiiwa.

Na ikitokea mzozano - kuwa wao wakubwa wanaona ndivyo, na nyinyi mlio chini mnaona sivyo - basi itazamwe Mwenyeezi Mungu au Mitume yake wamesema nini katika mfano wa jambo hilo,na ifuatwe hukumu ya Mwenyeezi Mungu na Mitume yake, likiwa linastahiki kufuatwa lifuatwe, na likiwa halistahiki lisifuatwe. Wala asishadidie tena huyo mkubwa kuwa naliwe tu. Japo sivyo sharia inavyosema, mategemeo iwe sharia ya Mwenyeezi Mungu na Mitume yake.

 

MWISHO

[1] Surat Al-Maidah Aya ya 54

[2] Surat Az-Zukhruf Aya ya 63

[3] Surat An-Nisaa Aya ya 59

 

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini