Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

UWIANO ULIOPO BAINA YA QUR_ANI NA AHLULBAYT (A.S)

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

UWIANO ULIOPO BAINA YA QUR_ANI NA AHLULBYT (A.S)

Kwa hiyo, natija inayopatikana katika somo hilo ni kuwa,ikiwa kuna mtu au kundi lolote lile lenye madai ya kuwa kitabu cha Qur-ani kinatosha, au kupinga amri za Mitume ya Mwenyeezi Mungu,kundi hilo au mtu huyo atakuwa amepinga maamrisho ya Mola wake. na kwa hakika atakuwa hakufanya amali ya yale yaliyomo ndani ya Qur-ani. Basi mtu huyo yuko mbali na Mwenyeezi Mungu.

Kwa hiyo, ikiwa Waislamu watamuamini Mwenyeezi Mungu na Mitume yake, na wakaamini na kutii yale ambayo wameamrishwa, hapana shaka wataepukana na mabalaa ya Mataghuti, na viongozi wenye kuleta ufisadi katika jamii. Kama inavyosema Qur-ani takatifu:-

وَلَوْ كَانُوا يُؤْمِنُونَ بِالله والنَّبِيِّ وَمَا اُنزِلَ إِلَيْهِ مَا اتَّخَذُوهُمْ اَوْلِيَاء وَلَـكِنَّ كَثِيراً مِّنْهُمْ فَاسِقُونَ[1]

Na lau wangeli kuwa wanamuamini Mwenyezi Mungu, na huyu Nabii, na yaliyo teremshwa kwake, wasingeli wafanya hao marafiki. Lakini wengi katika wao ni wapotofu.

*  Katika Aya hiyo ya 82, unatajwa ubaya wa Mayahudi na Manasara kuwa wanahiyari kuwafanya makafiri vipenzi vyao kuliko Waislamu, na hali ya kuwa wanajua kuwa Waislamu ndio wazuri au ndio walio katika haki, lakini husuda yao kubwa juu ya Waislamu, basi hata wakiwa vipi, wanawachukia tu. Na makafiri wengine ndio vivi hivi. Wanaona watu wa dini nyengine ni bora kuliko Waislamu .

Mwenyeezi Mungu anawaambia watu hao ni bora kama wangelikuwa pamoja na wale waliofuata njia njema, na kutii amri za Mola wao, kama inavyosema Qur-ani:-

وَمَن يُطِعِ اللّهَ وَالرَّسُولَ فَاُوْلَـئِكَ مَعَ الَّذِينَ اَنْعَمَ اللّهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاء وَالصَّالِحِينَ وَحَسُنَ اُولَـئِكَ رَفِيقاً[2]

Na wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume, hao wa pamoja na wale alio waneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii, na Masiddiqi, na Mashahidi, na Watu wema. Na uzuri ulioje kuwa pamoja na watu hao!

*  Kila watakaofanya mema wataingia peponi. Na kila watakaoingia Peponi watakutana na wenzao wa Peponi wawe pamoja humo, katika baadhi za nyakati, japokuwa wako mahala mbali mbali kwa mnasaba wa daraja walizopewa kwa amali zao ambazo hazikuwa namna moja. Lakini juu ya hivi watakutana.

Miongoni mwa daraja zilizotajwa hapa ni daraja ya:-

a) Unabii. b) Mkweli. c) Mashahidi (Martyrs). d) Usalih. (competent or pious).

Salih ni anayetekeleza haki za Mwenyeezi Mungu zilizo juu yake na kutekeleza haki za viumbe wenziwe zilizo juu yake, kwa mwisho wa uweza wake. Na Shahidi ni anayefanya haya na akapata bahati ya kuuawa kwa ajili ya dini. Na Siddiqi ni kama yule Salih, lakini anatekeleza kwa ukamilifu zaidi kabisa.

Na Unabii ni kupindukia mipaka ya Ubinaadamu na kufikia daraja ya Malaika.

Maelezo kwa ufupi ya makala zilizopita.

* Mitume ya Mwenyeezi Mungu haikuchukua malipo yoyote kutoka kwa watu kwa sababu ya kuwaongoza wao katika njia ya uongofu, na kitu kikubwa alichokitaka Mtume (s.a.w.w) kwa watu kikiwa kama ni malipo ni kuwataka watu kuwaamini  Ahlulbayt na kuwa na mapenzi nao. Na hiyo ni kwa sababu ya kudumisha madhumuni yake. Na kuihifadhi dini ya Kiislamu.

* kiongozi wa jamii ya Kiislamu ni amana muhimu ya Mwenyeezi Mungu, kwa hiyo amana hiyo ni lazima apewe mtu anayestahiki kuiongoza jamii ya Kiislamu.

* Mtume (s.a.w.w) na Maimamu (amani ziwe juu yao) ndio wafasiri waaminifu wa Aya za Qur-ani, na ndio watu bora wanaoweza kuhukumu kwa uadilifu, kwa sababu hiyo basi ili kukifahamu kitabu cha Qur-ani ni lazima tuzingatie kwa makini yale waliyoamrisha watu hao Watukufu.

Maswali:-

1.Hivi kweli Mtume Muhammad (s.a.w.w), alitaka malipo yoyote kwa watu kwa sababu ya kuwaongoza wao katika njia njema?.

2. Qur-ani Takatifu inaelezea nini kuhusu amana?.

3. Amana  kubwa ya Mwenyeezi Mungu ni ipi?.Na ni mtu gani anayestahiki kupewa amana hiyo?.
4. Hivi kweli Qur-ani inatosha kuwaongoza watu katika njia njema?.

[1] Surat Al-Maidah Aya ya 81.

[2] Surat Nisaa Aya ya 69

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini