Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

ALLAH (S.W) HAJAFANANA NA KITU

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

 ALLAH (S.W) HAJAFANANA NA KITU

Miongoni mwa sifa nyengine za Allah (s.w) ni:-

MWENYEEZI MUNGU SI KIUMBE, HANA KIWILIWILI NA KATU HAONEKANI.

Sisi tuna imani ya kuwa; Mwenyeezi Mungu haonekani kwa macho katu, kwa sababu kuona kwa macho kunamaanisha kuwa Mwenyeezi Mungu ni kiumbe aliye na kiwiliwili, aliye katika sehemu maalumu, au umbo maalumu, hali ya kwamba sifa hizoo ni sifa za viumbe vilivyoumbwa na Mwenyeezi Mungu, hali ya kwamba ubora na utukfu wa sifa za Mwenyeezi Mungu uko juu zaidi, kiasi ya kwamba haiwezekani kumfananisha Yeye na sifa za viumbe, kwa hivyo hatuwezi kumsifu Mwenyeezi Mungu kwa sifa za viumbe vyake, kwa hiyo kuwa na itikadi ya kumuona Mwenyeezi Mungu sio sahihi, na itikadi hiyo ni miongoni mwa aina fulani za shirki, na huko ndio kumshirikisha Mwenyeezi Mungu, Mwenyeezi Mungu Mtukufu anasema:-

لاَّ تُدْرِكُهُ الاَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الاَبْصَارَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ[1]

Macho hayamfikilii bali Yeye anayafikilia macho. Naye ni Mjuzi, Mwenye khabari.

Na ni kwa dalili hiyo basi, kaumu ya Bani Israili ikatoa hoja kumwambia Nabii Mussa (a.s) kuwa hawatamuamini Mwenyeezi Mungu isipokuwa pale watakapomuona, pale waliposema:-

وَإِذْ قُلْتُمْ يَا مُوسَي لَن نُّؤْمِنَ لَكَ حَتَّي نَرَي اللهَ جَهْرَةً فَاَخَذَتْكُمُ الصَّاعِقَةُ وَاَنتُمْ تَنظُرُونَ[2]

Na mlipo sema: Ewe Musa! Hatutakuamini mpaka tumwone Mwenyezi Mungu waziwazi. Ikakunyakueni radi nanyi mnaangalia.

Maelezo kuhusiana na Aya:

Kisa cha Mayahudi kutaka kumuona Mwenyeezi Mungu wazi wazi kinatajwa pia katika Talmud.

Basi Nabii Mussa (a.s) akaipeleka kaumu hiyo katika mlima ujulikanao kwa jina la Tur, akakariri mahitajio yao na hoja zao walizozitoa za kumuona Mwenyeezi Mungu, basi Nabii Mussa (a.s) akasikia jawabu hii kutoka kwa Mola wake:-

وَلَمَّا جَاء مُوسَي لِمِيقَاتِنَا وَكَلَّمَهُ رَبُّهُ قَالَ رَبِّ اَرِنِى اَنظُرْ إِلَيْكَ قَالَ لَن تَرَانِى وَلَـكِنِ انظُرْ إِلَي الْجَبَلِ فَإِنِ اسْتَقَرَّ مَكَانَهُ فَسَوْفَ تَرَانِى فَلَمَّا تَجَلَّي رَبُّهُ لِلْجَبَلِ جَعَلَهُ دَكّاً وَخَرَّ موسَي صَعِقاً فَلَمَّا اَفَاقَ قَالَ سُبْحَانَكَ تُبْتُ إِلَيْكَ وَاَنَاْ اَوَّلُ الْمُؤْمِنِينَ[3]

Na alipo kuja Musa kwenye miadi yetu, na Mola wake Mlezi akamsemeza, alisema: Mola wangu Mlezi! Nionyeshe nikutazame. Mwenyezi Mungu akasema: Hutoniona. Lakini utazame huo mlima.

Ukibaki pahala pake basi utaniona. Basi alipo jionyesha Mola Mlezi wake kwa mlima, aliufanya uvurugike, na Musa akaanguka chini amezimia. Alipo zindukana alisema: Subhanaka, Umetakasika!

Natubu kwako, na mimi ni wa kwanza wa Waumini.

Ni tukio hilo basi ndilo lililothibitisha kuwa Mwenyeezi Mungu haonekani katu.

Sisi tuna itikadi ya kuwa; ikiwa kuna baadhi ya Aya na Riwaya za Kiislamu zinaelezea kuhusu kuonekana kwa Mwenyeezi Mungu, makusudio ya Aya hizo sio kuonekana kwa macho, bali ni kuonekana ndani ya nyoyo, na kushuhudiwa ndani ya nafsi za wanaadamu. kwa sababu siku zote Aya za Qur-ani zinazifasiri Aya nyengine.

القران یفسر بعضه بعضا[4]

Kwa hakika Qur-ani inafasiri baadhi ya Aya nyengine.

Mbali ya hayo, tukiongezea kuithibitisha kauli hiyo, Imamu Aliy (a.s) alipokuwa akijibu suala la mmoja wa wafuasi wake, pale alipoulizwa:

یا امیر المؤمنین هل رأیت ربک.

yaani, Ewe Amiyrul-Muuminiyna, hivi kweli umewahi kumuona Mola wako? Imamu Aliy (a.s)  akamjibu  kwa kumwambia: أأعبد مالا اری ; yaani, hivi kweli nitaabudu nisiyemuona?. baadae akaendelea kwa kusema:-

" لا تدرکه العیون بمشاهدة العیان. ولکن تدرکه القلوب بحقایق الایمان[5] "

Macho katu hayawezi kumuona Mwenyeezi Mungu kwa uwazi, lakini nyoyo na nafsi za wanaadamu kwa kutumia nguvu za imani zinaweza kumuona Allah (s.w).
Sisi tuna itikadi ya kuwa; Kumnasibisha Mwenyeezi Mungu kwa sifa za viumbe, kama mwenyeezi Mungu kuwa na sehemu au zama maalumu, kuwa ana kiwiliwili, au kuwa na itikadi ya kuwa Mwenyeezi Mungu anaweza kushuhudiwa kwa macho, husababisha kuwa mbali na taaluma au elimu ya kumtambua Mwenyeezi Mungu, na mwenye na itikadi hizo basi atakuwa amemshirikisha Mwenyeezi Mungu, ndio Mwenyeezi Mungu (s.w) ni mbora wa kila kitu, na mbora wa kila sifa, na hakuna kitu chochote kinachofanana na Yeye.[4]  Hiyo ni hadithi maarufu iliyonukuliwa na Ibni Abbasi, lakini vile vile hadithi hiyo imenukuliwa kwa mtindo mwengine na Amiyrul-Muuminina Imamu Ali (a.s) ndani ya kitabu chake cha Nahjulbalagha, ان الکتاب یصدق بعضه بعضا...  yaani kwa hakika Qur-ani inafasiri baadhi ya aya nyengine. (Nahjulbalagha, hutuba ya 18),  na katika riwaya nyengine, imekuja kwa mtindo huu. وینطق بعضه  ببعض ویشهد بعضه علی بعض

yaani kwa hakika Qur-ani inabainisha baadhi ya aya, na inabainisha na kutoa shahada ya baadhi za Aya. (Nahjulbalagha, hutuba ya 103.)

[1] Surat Al-An-aam Aya ya 103

[2] Suratul-Baqarah Aya ya 55

[3] Surat Al-Aarafu Aya ya 143.

[5] Nahjulbalagha, hutuba ya 179.

 

MWISHO
 

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini