Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

KUZIDI KWA ELIMU NA KUDHIHIRIKA HAKI

0 Voti 00.0 / 5


 BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

UBORA WA NIDHAMU YA AKHERA KULIKO DUNIA NO.2

* Ni nidhamu gani iliyo bora? nidhamu ya duniani au nidhamu ya Akhera?

* Ni dalili gani zilizo bora zinazoonesha maendeleo ya ubora huo wa nidhamu?.

Dunia ni madrasa na shule ya mpito, dunia ni sehemu inayomkuza mwanaadamu na kumzidishia kiwango chake cha fikra, dunia ni sehemu inayompeleka mwanaadamu katika ukamilifu na kumfanya awe mcha Mungu, dunia ni sehemu ya biashara ya kuitakasa nafsi na maovu kwa wale Mawalii wa Mwenyeezi Mungu.

KUZIDI KWA ELIMU NA KUDHIHIRIKA UHAKIKA.

Miongoni mwa utukufu unaoonyesha ubora wa nidhamu ya Akhera kuliko nidhamu ya dunia ni kuwa, siku ya Kiyama ni siku ya kudhihirika uhakika na haki zote, siku hiyo vizuizi vyote vilivyokuwa vikisababisha kutofahamika elimu au taaluma yoyote ile vitaondolewa, nyenzo ambazo zinamtambulisha mwanaadamu zitakuwa na nguvu na uwezo wa hali ya juu kabisa, kiasi ambacho mwanaadamu ataondoka katika hali kughafilika na atakuwa na uwezo wa kudiriki na kufahamu yale yote ambayo hakuweza kuyafahamu duniani, kuhusiana na hayo Allah (s.w) anasema:-

لَقَدْ كُنتَ فِى غَفْلَةٍ مِّنْ هَذَا فَكَشَفْنَا عَنكَ غِطَاءكَ فَبَصَرُكَ الْيَوْمَ حَدِيدٌ[1]

(Aambiwe): Kwa hakika ulikuwa umeghafilika na haya; basi leo tumekuondolea pazia lako, na kwa hivyo kuona kwako leo ni kukali.

Na kwa wale ambao walikuwa na shaka ya siku hiyo, (waliokuwa na shaka ya kuwepo malipo ya waliotenda maovu), baada ya kuona nidhamu ya Akhera, na vipi Mola Mtakatifu anawalipa waja wake kulingana na amali zao, basi watu hao katika siku hiyo watasema:-

قَالُوا يَا وَيْلَنَا مَن بَعَثَنَا مِن مَّرْقَدِنَا هَذَا مَا وَعَدَ الرَّحْمَنُ وَصَدَقَ الْمُرْسَلُونَ[2]

Watasema: Ole wetu! Nani aliye tufufua kwenye malazi yetu? Haya ndiyo aliyo yaahidi Mwingi wa Rehema na wakasema kweli Mitume.

isitoshe, katika Siku ya Kiyama, kwa wale ambao walileta khitilafu katika kuifahamu njia sahihi ya dini, hali ya kwamba wanaielewa njia sahihi, bali walifanya hivyo kwa ajili ya kupata mafanikio ya malengo yao, basi walimkhalifu Mwenyeezi Mungu, na Mitume yake na Ahlulbayt (a.s), basi siku hiyo yatadhihirika yale yaliyomo ndani ya nafsi zao, na hakutakuwa na mtu yoyote yule atakayekuwa na shaka katika kumuamini Mola wake, kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani takatifu:

وَلاَ تَكُونُواْ كَالَّتِى نَقَضَتْ غَزْلَهَا مِن بَعْدِ قُوَّةٍ اَنكَاثاً تَتَّخِذُونَ اَيْمَانَكُمْ دَخَلاً بَيْنَكُمْ اَن تَكُونَ اُمَّةٌ هِيَ اَرْبَي مِنْ اُمَّةٍ إِنَّمَا يَبْلُوكُمُ اللّهُ بِهِ وَلَيُبَيِّنَنَّ لَكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ مَا كُنتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ[3]

Wala msiwe kama mwanamke anaye uzongoa uzi wake baada ya kwisha usokota ukawa mgumu. Mnavifanya viapo vyenu kuwa ni njia ya kudanganyana baina yenu kwa kuwa ati taifa moja lina nguvu zaidi kuliko jengine? Hakika Mwenyezi Mungu anakujaribuni kwa njia hiyo. Na bila ya shaka atakubainishieni Siku ya Kiyama mliyo kuwa mkikhitalifiana.

 Maelezo kuhusiana na Aya.

 Huu ni mfano tu anaopigiwa anayevunja ahadi yake, mafano wake kama mtu aliyepoteza nguvu zake barabara katika kusokota uzi au kamba, kisha akainyambulia mbali.

Na ni kwa sababu hiyo basi, Mwenyeezi Mungu ameiita siku hiyo kuwa ni siku ya kudhihirika uhakika wa amali za watu na yale yaliyomo ndani (batini) ya nyoyo za watu. kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani:-

يَوْمَ تُبْلَي السَّرَائِرُ[4]

Siku zitakapo dhihirishwa siri.

Siku hiyo ni siku ya kudhihirika yale yaliyomo ardhini, kwa sababu uhakika wa yale yaliyomo ardhini yamefungamana na siku hiyo . kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani:-

وَاَشْرَقَتِ الاَرْضُ بِنُورِ رَبِّهَا وَوُضِعَ الْكِتَابُ وَجِيءَ بِالنَّبِيِّينَ وَالشُّهَدَاء وَقُضِيَ بَيْنَهُم بِالْحَقِّ وَهُمْ لاَ يُظْلَمُونَ[5]

Na ardhi (siku hiyo) itangara, kwa nuru ya Mola wake, na madaftari (ya vitendo) yatawekwa; na wataletwa Manabii na mashahidi, na kutahukumiwa baina yao kwa haki wala hawatadhulumiwa.

Hatimae watu watapata habari ya uhakika wote, na litaondolewa pazia la unafiki la baadhi ya watu, watu ambao walifanya jitihada zao zote ili kubatilisha akida sahihi kwa upotofu wao na kutoa nadharia zao potofu ambazo zinatokana na akida chafu za shirki, basi siku hiyo ni siku ya kuwekwa wazi uhakika na kudhirishwa uovu. katika qur-ani tunasoma:-

وَاَلْقَوْاْ إِلَي اللهِ يَوْمَئِذٍ السَّلَمَ وَضَلَّ عَنْهُم مَّا كَانُواْ يَفْتَرُونَ[6]

Na siku hiyo watasalimu amri mbele ya Mwenyezi Mungu, na yatapotea waliyo kuwa wakiyazua.

[1] Surat Qaf Aya ya 22
[2] Surat Yaasin aya ya 52.
[3] Suratun-nahli Aya ya 92.
[4] Surat –Atarik Aya ya 9
[5] Surat Zumar Aya ya 69
[6] Surat Nahli Aya ya 87

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini