Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

ARUBAINI YA IMAM HUSEIN (A.S)

0 Voti 00.0 / 5

Arubaini ya Imam Hussein.

Ukurasa Mwingine wa Mapambano ya Ashura

Arubaini ya Imam Hussein, Ukurasa Mwingine wa Mapambano ya Ashura
Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Makala hii imeandikwa kwa mnasaba wa Siku ya Arubaini ya Imam Hussein (A.S), ambayo inahuisha matukio ya siku ya arubaini baada ya mauaji ya mjukuu wa Mtume Mtukufu, Imam Hussein bin Ali (A.S) katika ardhi ya Karbala nchini Iraq.
Imepokewa katika historia ya Kiislamu kwamba; siku ya arubaini baada ya tukio chungu na la kusikitisha la kuuawa mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (S.A.W.W), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, msafara wa baadhi ya watu waliobakia hai katika familia ya mtukufu huyo ulipitia tena Karbala ukiwa njiani kurejea Madinatul Munawwarah. Siku hiyo Imam Zainul Abidin mwana wa Imam Hussein (A.S) akiwa pamoja na shangazi yake Zainab binti Ali bin Abi Twalib na watu wengine wa familia ya Mtume waliopatwa na masaIbu ya mauaji makubwa ya Karbala, walifanya majlisi ya maombolezo katika makaburi ya mashahidi wa Karbala. Imepokewa kwamba sahaba mwema wa Mtume (S.A.W.W) Jabir bin Abdillahil Ansari (R.A) pia siku hiyo alifika Karbala kuzuru mashahidi wa tukio la Ashura pamoja na watu wa msafara wa familia ya Imam Hussen AS. Katika siku hiyo ya Arubaini ya Imam Hussein na mashahidi watukufu wa Karbala, Waislamu wafuasi wa Ahlulbait na watu wa Nyumba ya Mtume huhuisha tukio hilo la kusikitisha na kukumbuka masaibu yaliyowapata wana na vipenzi vya Mtume wetu Muhammad SAW.
Msafara wa familia ya Imam Hussein AS uliokuwa ukirejea Madina kutoka Sham kwa mtawala dhalimu wa Bani Umayyah Yazidi mal'uni, ulibakia Karbala kwa muda wa siku tatu na baada ya kufanya majlisi ya maombolezo na kuwakumbuka mashahidi wa tukio hilo la kusikitisha ulielekea katika mji mtakatifu wa babu yake Hussein Madinatul Munawwarah.
Karbala katika historia ya Uislamu ina maana ya imani na kujitolea mhanga kwa ajili ya dini ya Mwenyezi Mungu na thamani za kibinadamu, na Ashura yaani tarehe 10 Muharram,siku aliyouawa shahidi Imam Hussein Bwana wa Mashahidi SA, inamaanisha historia ya hamasa, kumpenda Mwenyezi Mungu, haki na hakika yote. Kwa msingi huo hapana shaka kuwa hamasa ya Imam Hussein ni tochi inayomulikia wanamapambano na wapigania haki na uadilifu kote duniani katika zama na mahala tofauti. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kwa mujibu wa hadithi ya Mtume wetu Muhammad Mkweli Mwaminifu SAW, Hussein ni nuru ya uongofu na jahazi la wokovu.
Hussein bin Ali AS alikuwa mwanamageuzi mkubwa aliyeanzisha harakati yake kubwa kwa shabaha ya kupambana na upotofu na upotoshaji wa dini na thamani za kibinadamu uliokuwa ukifanywa na watawala wa Banii Umayyah. Huu ndio mwenendo wa wanamageuzi adhimu wa historia ambao daima hufanya juhudi kubwa za kuokoa jamii ya mwanadamu na kuielekeza katika njia nyoofu.
Kwa hakika jambo lililokuwa likimtatiza mno Imam Hussein katika zama hizo ulikuwa ujahili na ujinga wa watu. Kwa msingi huo, mtukufu huyo alifanya jitihada kubwa za kuwaamsha watu na kuwaondoa katika giza la ujinga lililotanda tena miongo kadhaa baada ya kufariki dunia babu yake, Muhammad SAW. Tunaweza kusema kuwa moja ya matunda adhimu ya harakati na mapambano ya Imam Hussein AS katika siku ya Ashura huko Karbala, ni kuiamsha jamii ya Kiislamu. Kimsingi moja na njia zinazotumiwa na watawala madhalimu kwa ajili ya kudhibiti watu ni kuwabakisha au kuwazamisha katika ujinga, mghafala na anasa za kupita za dunia. Hapana shaka kuwa, utawala wowote fasidi na wa kidhalimu hauwezi kubakia hai kwa kudumisha dhulma, mateso na uonevu. Kwa hivyo watawala madhalimu hufanya jitihada za kubadili itikadi za watu na mitazamo yao kuhusu masuala mbalimbali kwa maslahi ya tawala zao na kudhamini uhai wa serikali zao kupitia njia hiyo ya hadaa na kupotosha itikadi sahihi.
Banii Umayyah walitumia mbinu hiyo ya kishetani kwa ajili ya kutawala jamii ya Kiislamu na daima walikuwa wakifanya jitihada za kubadili na kupotosha thamani na itikadi sahihi za tangu zama za Mtume SAW kwa maslahi yao. Walieneza mafundisho yaliyopotoshwa ya dini katika jamii na kubadili kabisa mitazamo na itikadi za watu kwa maslahi yao. Ukosefu wa maarifa miongoni mwa baadhi ya Waislamu katika kipindi hicho nyeti cha historia ulisaidia mno kueneza upotoshaji huo wa Banii Umayyah. Kwani wakati watu wa jamii wanapokuwa na uchache wa maarifa ya dini ya Mwenyezi Mungu, masuala mengi ya kijamii, kisiasa na kadhalika husombwa na wimbi la opotoshaji. Katika mazingira kama haya yumkini hata abidi na watu wanaoonekana watenda ibada wakahadaika na kuwa nyezo zinazotumiwa na watawala dhalimu na fasiki. Mtume Muhammad SAW alitahadharisha katika zama za uhai wake kuhusu hatari ya kujitokeza kundi kama hili la abidi na wafanya ibada waliohadaika na kutumbukia katika mitego ya watawala dhalimu. Amesema katika hadithi iliyopokewa na wanazuoni wa Kiislamu kwamba: "Litatokeza kundi miongoni mwenu ambalo ninyi mutaziona swala na swaumu zenu kuwa ni duni na si lolote mbele ya swala na swaumu zao, na amali zenu nzuri zitaonekana chache na sizizokuwa na thamani mkabala wa amali zao. Watu wa kundi hilo watakuwa wakisoma Qur'ani kwa wingi lakini kisomo hicho cha Qur'ani hakivuki makoo yao (na kutekelezwa katika vitendo). Kundi hilo litaondoka katika dini mithili ya mshale unavyoondoka katika upinde." Mtukufu Mtume amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Aali zake, analiarifisha kundi hilo kuwa ni la watu wenye ufahamu finyu, wasioona mbali na makaidi.
Baada ya Imam Hussein AS kutambua vyema hatari ya watu kama hawa hususan katika ngazi ya utawala na uongozi wa umma wa Kiislamu, alianzisha harakati kubwa ya mageuzi na kuwazindua Waislamu na kuzidisha wimbi la mwamko wa kidini, kisiasa na kijamii. Imam Hussein AS anabainisha sifa za kundi la watu hao akisema: "Ni watumwa wa dunia, na dini imekuwa kichezeo katika ndimi zao. Hufuata dini maadamu inakidhi matakwa na matamanio yao, na wanapopatwa na mtihani na balaa, wenye dini halisi miongoni mwao huwa kalili na wachache mno."
Banii Umayyah waliifanya dini ya Mwenyezi Mungu kama mwanasesere wa malengo yao ya kisiasa na walifanya jitihada kubwa za kubadili mafundisho halisi ya dini na kupotosha maana zake. Imam Hussein aling'amua na kuelewa vyema hali hiyo na akajifunga kibwebwe katika harakati ya kuweka wazi jambo hilo na kubainisha hali ya kisiasa na kijamii ya wakati huo. Aliwatahadharisha Waislamu kuhusu njama za kubadilishwa thamani za dini yao na taathira mbaya za kukaa kimya mbele ya upotofu huo. Alieleza kuwa, hatari kubwa zaidi kwa jamii ya Kiislamu ilikuwa serikali ya mtawala dhalimu na anayeabudu dunia na matamanio ya nafsi yake. Kwa msingi huo alikuwa akisisitiza mno juu ya udharura wa kutomkubali Yazid bin Muawiya kama khalifa na mtawala wa Waislamu.
Lengo la harakati ya Imam Hussein
Tangu mwanzoni mwa harakati yake Imam Hussein AS alilitaja lengo la mapambano hayo kuwa ni kuamrisha mema na kukataza maovu na kurekebisha umma wa babu yake Mtume wa Mwenyezi Mungu. Harakati hiyo ya Imam Hussein ya kuwaamsha Waislamu, mapambano yake na kisha kuuawa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu katika medani ya Karbala vilitia mshtuko mkubwa katika kiwiliwili cha umma wa Kiislamu na kuwaamsha waliokuwa wamelala.
Mwanahistoria mashuhuri wa Kiislamu Ibn Khaldoun ameandika yafuatayo kuhusu athari za tukio la Ashura na kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume SAW: Mauaji ya Hussein bin Ali bin Abi Twalib yalizusha wimbi kubwa la hasira na chuki ya Waislamu dhidi ya utawala wa Bani Umayyah. Baadhi ya watu walijuta mno kutokana na kwamba hawakumsaidia mwana wa Mtume, na taratibu wimbi la mwamko lilianza kuenea kwa kasi katika jamii ya Kiislamu na kutayarisha uwanja mzuri wa harakati za Tawwabin kwa maana ya (Waliotubu) na Mukhtar bin Ubaid al Thaqafi." Mwisho wa kunukuu.
Mchango wa Bibi Zainab katika harakati ya Ashura
Nafasi na mchango wa Bibi Zainab binti Ali bin Abi Twalib AS, dada yake Imam Hussein na vilevile Imam Ali bin Hussein Zainul Abidin mwana wa Hussein bin Ali AS, ulikuwa na umuhimu mkubwa sana katika kufanikisha mapambano ya mjukuu huyo wa Mtume. Hotuba zilizotolewa na watukufu hao wawili huko Kufa, Iraq na Sham kwa mtawala dhalimu na mal'uni Yazid bin Muawiya katika siku za mwanzoni za baada ya kuuawa shahidi Imam Hussein AS, zilikuwa cheche za mwanzoni zilizozusha wimbi kubwa la mwamko na harakati kubwa baina ya watu waliokuwa wameghiriki katika mghafala na ujinga. Hotuba na maneno ya waziwazi ya wabeba ujumbe hao wa harakati na mapambano ya Karbala yalitikisa nguzo za utawala wa Bani Umayyah na kuweka wazi malengo ya njia ya haki ya Imam Hussein AS.
Matunda ya mapambano ya Hussein AS.
Kwa hakika mapambano ya Imam Hussein AS yalikuwa na matunda makubwa katika nyanja za kisiasa na kijamii. Matunda ya mapambano hayo yalikuwa na taathira kwa zama hizo na kufanya mabadiliko katika zama zilizokuja baadaye. Hii ni kutokana na ukweli kwamba harakati ya mtukufu huyo ilifuata misingi na thamani zinazokubaliwa na wanadamu katika mahala na zama zote. Mambo kama kumuweka mbele ya Mwenyezi Mungu na mafundisho yake, kupigania uadilifu na kupinga dhulma na uonevu yalitawala na kuonekana katika awamu zote za harakati na mapambano ya Imam Hussein AS. Kwa hakika tunaweza kusema kuwa mapambano ya Imam Hussein AS hayana kifani katika suala la kuzusha wimbi la hamasa na mwamko katika umma na kudhirisha ukamifu wa kiroho, kujitolea na kusabilia nafsi na kila lililoghali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
Ni kutokana na ukweli huo ndiyo maana mapambano ya Hussein amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake, ikaendelea kutoa ilhamu na kuwa ibra kwa wapigania uhuru, haki na uadilifu katika nyakati na zama zote. Hii leo harakati ya mtukufu huyo inaweza kuwa ilhamu kwa mataifa yote yanayokandamizwa na kupigania haki, uhuru na uadilifu kote duniani bila ya kijali dini, kaumu wala utaifa wao.
Ni kwa sababu hiyo hiyo pia ndiyo maana kiongozi wa harakati za kupigania uhuru za watu wa India Mahatma Ghandhi akaitaja harakati na mapambano ya Imam Hussein kuwa ndiyo yaliyompa ilhamu katika juhudi zake za kuwakomboa watu wa India. Vilevile mapinduzi makubwa ya wananchi wa Iran yalipata ushindi kwa kufuata ibra na mafunzo ya Ashura ya Imam Hussein AS na yangali yanasonga mbele na kudumisha mapambano dhidi ya mashetani wa dunia ya sasa na akina Yazidi wa zama hizi kutokana na kushikamana na misingi ya harakati ya Bwana wa Mashahidi, Imam Hussein AS.
Ashura ilikuwa siku moja ya tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria lakini taathira zake kubwa zitabakia daima dawamu na kuwa tochi inayowamulikia wapigania haki kote duniani. Mapambano ya Imam Hussein yataendelea kuwa chemchemi ya maji safi inayokata kiu ya wanaotafuta maarifa, haki na kweli na kutoa ilhamu na ibra kwa harakati za kupambana na batili. Darsa za Ashura zitaendelea kusomwa katika zama na mahala tofauti maadamu mpambano wa haki na batili na dhulma na uadilifu ungali unashuhudiwa katika pembe mbalimbali za dunia.
Maalumu ya Arubaini ya Imam Hussein, Ukurasa Mwingine wa Mapambano ya Ashura yanafikia tamati. Tunamuomba Mwenyezi Mungu SW atupe shafaa ya Imam Hussein AS na atufufue pamoja na mashahidi wa Karbala. Amin ya Rabbal alamiin.
Wassalam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini