Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

MAZAZI YA MTUME (S.A.W.W)

2 Voti 05.0 / 5

MAULID YA KUZALIWA KWA MTUME (S.A.W.W)

Napenda kuchukua nafasi hii muhimu kudhihirisha furaha kubwa niliyonayo moyoni kwa kuzaliwa muokozi wa Mwanadamu Mtume wa Uislaam Muhammad (s.a.w.w). Bwana Mtume (S.a.w.w) alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka wa tembo uliosadifiana na mwaka 570 Miladia kama ambavyo Waislaam wengi wa Madhehebu ya Kisuni wanavyoamini.Na kundi lingine la Waislamu ambalo linaundwa zaidi na Waislamu wa madhehebu ya Kishia wao wanaamini kwamba, Mtume wa Uislamu alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka huo huo wa tembo.Hivyo kuanzia tarehe 12 hadi 17 (sawa na wiki moja) ni masiku ya Waislaam wote ulimwenguni kusherehekea kwa kuzaliwa Mtume wao (s.a.w.w) bila kujali tofauti ilipo ya kihistoria kuna siku ya kuzaliwa kwake.Suala hili la kuunganisha tarehe mbili ziwe rasmi kwa Waislaam wote bila kujali madhehebulimekuwa ni bora zaidi kuliko kuutumia muda huo kubishana bishana kuna tarehe sahihi ya kuzaliwa kwake (s.a.w.w),suala hili limepelekea kuwepo hali ya umoja kwa Waislaam kwani hukutana kuanzia tarehe 12 hadi 17 kwa lengo la kukumbusha kunako uzawa wa Mtume (s.a.w.w) na kujadili mambo mbali mbali ya Kiislaam , kupeana nasiha mbali mbali na kukumbushana kwani hakika ya ukumbusho ni wenye kuwafaa Waumini.Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislaam ya Iran Imam Khomeini (Mwenyeezi Mungu Amrehemu) ndiye mwasisi wa fikra hii ya kuziunganisha pamoja tarehe mbili yaani(12 na 17) ziwe tarehe rasmi kwa Waislaam kukutana na kusherehekea siku ya kuzaliwa Bwana Mtume (s.a.w.w) ambapo masiku hayo yaliyobaina ya tarehe mbili aliyapatia anuani ya "WIKI YA UMOJA".

Baada ya utangulizi huo ningependa kuchukua nafasi hii kuwapongeza Waislaam wote Ulimwenguni kote kwa mnasaba wa kuzaliwa Mtume Muhammad (s.a.w.w).Kwa wale wapenzi wa Mtume (s.a.w.w) siku ya leo ya kuzaliwa Mtume wao (s.a.w.w) huichukulia kuwa ni siku muhimu sana ukilinganisha na masiku mengine ,kwani Mtume (s.a.w.w) ni Nuru katika Umma huu,Mtume (s.a.w.w) ni Rehma katika umma huu,Mtume (s.a.w.w) ni Kiigizo chema katika umma huu,Mtume (s.a.w.w) ni Mwokozi wa Mwanadamu katika umma huu, Mtume (s.a.w.w) ni Mwenye Huruma zaidi kwa umma huu,Mtume (s.a.w.w) ni sababu ya kuwepo amani katika umma huu na hilo amelithibitisha Allah (s.w) katika Qur'an Tukufu, nikiashiria katika madhumuni ya Aya hiyo alisema (s.w) kwamba "anasita kuwaadhibu (waovu katika umma huu) maadam Mtume (s.a.w.w) ni mmoja kati ya watu wa umma huu"

Laiti kama si hivyo basi kulingana na madhambi ya baadhi ya watu katika umma wanayoyafanya kwa sasa au waliyoyafadha,nadhani yamezidi mara kumi yale madhambi yaliyofanywa na watu waliotangulia kabla ya umma huu wa Mtume (s.a.w.w) kama vile wale watu aliowangamiza Allah (s.w)

katika zama za Nabii Luutu,Nabii Swalehe,Nabii Nuh (a.s),walifanya madhambi Allah (s.w) akakasirika kwa vitendo vyao akaamua kuwaangamiza,lakini ukilinganisha madhambi ya sasa ni makubwa zaidi kuliko yale ya zama hizo,kwanini Allah (s.w) mpaka leo hii hajauangamiza umma huu? Ni kwa sababu katika umma huu yumo mbora wa viumbe ,Sayyid wa Manabii na Mitume,wa Mwisho katika listi ya Manabii na Mitume Bwana wetu Muhammad (s.a.w.w), huyu ndiye Mtume Muhammad (s.a.w.w) ambaye ndiye sababu ya Allah (s.w) kutouadhibu umma huu kulingana na makamu ,cheo,daraja, na nafasi aliyokuwa nayo kwa Allah (s.w).Hivyo Mtume (s.a.w.w) ni amani kwa Umma huu pia ni Rahma kwa walimwengu wote,kwani kamtoa Mwanadamu kwenye giza na kumuingiza katika Nuru.Mtume (s.a.w.w) alikuwa mpole,hadi Allah (s.w) akasisitiza na kukumbusha kunako upole kwa kusema:

"فَبِما رَحْمَة مِنَ اللّهِ لِنْتَ لَهُمْ وَ لَوْ كُنْتَ فَظًّا غَليظَ الْقَلْبِ لاَنْفَضُّوا مِنْ حَوْلِ"

Maana yake: Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungeli kuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangeli kukimbia. (Suura Aali Imraan, Aya ya 159-).

Hapa Mwenyeezi Mungu anadhihirisha akhlaq na tabia ya hali ya juu aliyokuwa nayo bwana wetu Mtume (s.a.w.w),hakuwa mkali,alipenda watu watu walimpenda,aliishi baina yao alikula nao walikula nae,kila mtu alijihisi yuko huru kuongea na Mtume (s.a.w.w) hakuogopwa kama smba kwani tabia zake na na jinsi alivyokuwa akiishi na watu ni mambo yaliyopelekea watu wamtambue siku zote kuwa ni mtu laini kwao mwenye kuwasikiliza na kutatua matatizo yao,na hii ndio siri na sababu kubwa iliyopelekea Mtume (s.a.w.w) aweze kufikisha kwa ukamilifu ujumbe wa Allah (s.w) kwa walimwengu wote.kwani laiti kama angelikuwa mtu mwenye jeuri,mkali kupindukia,mwenye maneno makali kama upanga ,mwenye moyo mgumu kama jiwe asiyeingilika,basi ingelikuwa tabu watu kukubali ujumbe aliokuja nao kutoka kwa Allah (s.w).

Huyu ndiye Mtume (s.a.w.w) ambaye leo hii tunasherehekea na kukumbuka kuzaliwa kwake.hakika alikuwa mtu ambaye tukiamua kumzungumzia hatuwezi kummaliza maana tutakesha bila kumaliza,amekusanya sifa zote nzuri na hatuwezi kumsifia kwa kiwango kinachotakiwa kiukamilifu ispokuwa yule anayemjua zaidi Mtume (s.a.w.w) ndiye mwenye uwezo huo ambaye ni Allah (s.w).Salamu ziwe juu yako ewe Mjumbe wa Mwenyeezi Mungu (s.a.w.w) na kwa watu wa Nyumba yako waliotwaharishwa (a.s).

Ni neema kwa kubwa ya Mwenyeezi Mungu (s.w) kwa waja wake kuwatumia Mjumbe aliyebeba ujumbe wake ambaye kaitwa Mbinguni kwa jina la Ahmad na Ardhini kwa jina la Abal-Qaasim Muhammad (s.a.w.w).Kwa hakika Mtume (s.a.w.w) amefanikiwa kuufikisha Ujumbe huo kwa waja wa Mwenyeezi Mungu (s.w) kwa mafanikio ya hali ya juu na kwa ukamilifu kama alivyotakiwa kufikisha.Ujumbe huo wa Allah (s.w) alioubeba Bwana Mtume (s.a.w.w) umekamilishwa kwa kutangaza Wilaya kwa Ahlul-bayt wake (a.s) ambao ni Mwasii na Makhalifa wake baada yake katik Umma wake (s.a.w.w).Suala hili la kutangaza Wilaya kwa Ahlul-bayt (a.s) lilikuwa ni suala muhimu ambalo lilichukuliwa kuwa ndio litakalo kamilisha kikamilifu ufikishaji wa Ujumbe alioteremshiwa ambapo laiti kama asingefikisha hilo basi angehesabika kuwa hajafikisha ujumbe alioteremshiwa na yote aliyoyafanya katika kipindi cha miaka 23 ingelikuwa kazi bure,!!

Mwenyeezi Mungu (s.w) anamwambia Mtume (s.a.w.w) katika Qur'an Tukufu akisema:

"Ewe Mtume fikisha uliyotoremshiwa kutoka kwa Mola wako,na usipofanya hivyo utakuwa hujafikisha ujumbe wake"

Ujumbe aliotakiwa kuufikisha kwa Mujibu wa Wanazuoni na Wafasiri wa Qur'an Kutufu ni:

"Kumtangaza Amirul-Muuminin,Imam wa Mashariki na Magharibi Simba wa Mwenyeezi Mungu, Imam Ali Bin Abi Twalib (a.s) kuwa ni Wasii wake na Khalifa wake baada yake".

Baada ya Mtume (s.a.w.w) kulitekeleza hilo kwa kumtangaza Imam Ali (a.s) mbele ya mkusanyiko mkubwa wa maswahaba akiwemo Abu bakri (R.a) na Umaru (R.a) pamoja na Uthman (R.a),Mwenyeezi Mungu akatangaza rasmi kuwa sasa dini imekamilika na nimekuridhieni dini ya Uislaam iwe dini yenu.Anasema Mwenyeezi Mungu (s.w) kuhusu hilo katika Suuratul Maidah,Aya ya 3, namna hii:

"Basi kwa sababu ya Reheme ya Mwenyeezi Mungu umekuwa laini kwao,na kama ungelikuwa jeuri (,mkali ,mshari) mwenye moyo mgumu,(watu ) wangekukimbia".

اليوم أکملتُ لکُم دِيناکُم وأتمَمتُ عَليکُم نِعمَتِي،وَرَضِيتُ لَکُم الإسلامَ دِيناً

"Leo nimewakamilishieni dini yenu,na kuwatimizieni neema yangu,na nimewapendeleeni Uislaam uwe dini yenu"

Tunamshukuru Allah (s.w) kwa kutukamilishia dini yetu na kutimiza neema yake kwetu pamoja na kuridhia na kutupendeleea Uislaam uwe dini yetu,pia tunamshukuru Allah (s.w) kwa kutujalia tukawa miongoni mwa wale waliopata bahati ya kuitikia wito na kuupokea Ujumbe wa Allah (s.w) aliokuja nao Bwana wetu Mtume (s.a.w.w) pasina kuuliza kwani nini wala kufanya khiana.Pia tunamuomba Allah (s.w) atujalie tuwe miongoni mwa wale wenye kuidhihirisha haki na kuitenga na batili.Pia hatuna budi kumshukuru Allah (s.w) aliyetujalia tukawa miongoni mwa wale waliopata bahati ya kushikamana na Wilaya ya Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) na Ahlul-bayt (a.s) kwa ujumla.

Ujumbe wangu mzito kwa siku ya leo kwa waislaam wote ulimwenguni ni hadithi tukufu ya Mtume (s.a.w.w) inayoitwa "HADITHU-THAQALAYNI" ambapo Mtume wetu (s.a.w.w) ametutaka tushikamane na vizito viwili hivi:

Tukifanikiwa kushikamana na vizito hivi viwili kama Mtume wetu (s.a.w.w) alivyotutaka tufanye,basi tutafaulu hapa duniani na kesho akhera.

KITABU CHA MWENYEEZI MUNGU (QUR'AN) NA KIZAZI CHAKE KITUKUFU (ITRA) AHLUL-BAYT WAKE

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini