Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

HISTORIA YAKUZALIWA MTUME ( S.A.W.W)

24 Voti 03.2 / 5

HISTORIA YA MAISHA YA MTUME MUHAMMAD BIN ABDILLAH (S.A.W).

Bismillah Ar-rahmaan Ar-rahiim.

Assalaam Alaikum Warahmatullah Taala Wabarakaatuh.

Maisha ya Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w) mwana wa Abdullah yako wazi zaidi kuliko yale ya Mitume (a.s) wengine waliomtangulia.Kwa nini? jawabu lake ni kwasababu: Kadiri wakati ulipokuwa ukizidi kupita ndivyo mabadiliko ya kihistoria,mabadiliko ya vitabu,mabadiliko ya sheria na hata shakhsia zao yalivyozidi kutokea, vyote hivyo vilipotoshwa na hivyo maisha yao kutojulikana vyema.

Kwa hakika hakuna nyaraka zilizopo ispokuwa zile tunazozipata kutoka katika Kitabu Kitukufu cha Dini ya Kiislaam  ambacho ni Qur’an Tukufu ambayo ni maneo ya Mwenyeezi Mungu (s.w) na Maneno ya Mtume (s.a.w) na Watu wa nyumba yake waliotwaharishwa yaani Ahlul bayt wake (a.s).

Kuna historia iliyokuwa wazi na safi kabisa inayozungumzia maisha ya Mtume (s.a.w) na kuzibainisha sifa za maisha yake kwa njia safi yenye kuridhisha kabisa.

Mtukufu Mtume (s.a.w) ni Mtume wa mwisho ambaye kachaguliwa na Mwenyeezi Mungu (s.w) kuwaongoza walimwengu wote.Hivi sasa ni karne kumi na nne (14) zimepita,katika kipindi hicho yaani karne 14 zilizopita wanadamu walikiishi katika hali ambayo hakuna athari yoyote ile ya Tawhid iliyokluwa ikionekana ispokuwa kutajwa jina tu.Watu walikuwa wameipuuza tawhid kikamilifu.Maadili na uadilifu vilikuwa vimetoweka kabisa katika jamii ya wanadamu.mwenye nguvu ndiye aliyekuwa akitamba na kuonekana dunia imeumbwa kwa ajili yake peke yake na wengine hawana haki katika dunia hii,ubabe ulitawala kila sehemu.Kaaba Tukufu ilikuwa imegeuzwa na kuwa sehemu ya kuabudia masanamu na Dini ya Nabii Ibrahim (a.s) ilikuwa imebadilishwa na kuwa ya kuiabudu miungu mbali mbali.

Waarabu walikuwa wakiishi katika maisha ya kikabila na hata baadhi ya miji yao kama huko Hijaz,Yemen na sehemu nyinginezo zilikuwa zikitawaliwa kwa misingi ya ukabila.Waarabu walikuwa wakiishi katika unyonge na hali za kubaki nyuma kimaisha .Badala ya kujishughulisha na utamaduni na ustaarabu walijishughulisha na walijishughulisha na maovu,ulevi ,kamali na tama za kimwili.Hawakuishia hapo tu bali walikuwa wakiwazika watoto wao wa kike wakiwa hai kabisaa maana walikuwa na itikadi za ajabu,walikiamini kuwa mtoto wa kike ni mkosi hivyo alipokuwa akizaliwa mtoto wa kike walikuwa hawaoni tabu kumzika akiwa hai.!

Wengi wa waarabu hao walikuwa wakiishi kwa njia ya wizi,uharamia,uuaji,na kupora mali mifugop na ngome za wenzao.Unyama na umwagaji damu ni mambo yaliyokuwa yakichukuliwa kuwa ya heshima na ya kumletea sifa kubwa.Utakuta walikuwa wakishindana kufanya uovu na ili mtu akishinda na kuonekana ni bingwa wa uovu apewe heshima kubwa na sifa ya hali ya juu.

Katika mazingira kama hayo;Mwenyeezi Mungu (s.w) Mwenye rehema na mapenzi ya hali ya juu kwa waja wake alimchagua Mtume Muhammad (s.a.w) ili kuwabnadilisha na kuwaongoza walimwengu wote.Mwenyeezi Mungu (s.w) baada ya kumchagua akamteresha Qur’an Tukufu iliyojumuisha Elimu takatifu,Tawhid,njia za kutekeleza Uadilifu, na mawaidha yenye faida kubwa sana.

Mwenyeezi Mungu (s.w) alimwamuru awaite watu kuelekea maisha ya ubinadamu na kushikamana na haki kwa kuitumia Kitabu Kitufu Qur’an.

KUZALIWA KWA MTUME (S.A.W).

Mtume Muhammad (s.a.w) alizaliwa katika mji mtakatifu unaoitwa Makka mwaka wa 570 AD.Mwaka huu ulijulikana kama mwaka wa Tembo.Mtume Muhammad (s.a.w) alizaliwa katika Familia  ya Kiarabu yenye heshima kubwa sana na iliyokuwa maarufu sana kila sehemu.Baba yake Mtume (s.a.w) ni Abdullah,baba yake huyu alifariki dunia kabla ya kuzaliwa kwake.Pia Mtume (s.a.w) alimpoteza Mama yake mzazi alipofikisha umri wa miaka sita (6).Baada ya miaka miwili au alipofikisha umri wa miaka minane (8),Babu yake {Abdul Mutw-twalib},aliyempenda sana Mtume na aliyekuwa msimamizi wake naye pia aliaga dunia.Baadaye Mtukufu Mtume (s.a.w) aliwekwa chini ya usimamizi na ulinzi wa baba yake mdogo Abu Twalib {ambaye ni Baba yake Amirul-Muuminina Ali -a.s-}.Na huu ulikuwa ni usia wa Babu yake Mtume (s.a.w) kwa mwanae huyo Abu Twalib ambapo alimtaka asimamie maisha yake (s.a.w) na kumpa ulinzi wa kutosha dhidi ya maadui wabaya waliokuwa na lengo la kutaka kumdhuru Mtume (s.a.w),usia huu baada ya kifo cha {Abdul Mutw-twalib},{Abu Twalib} aliufanyia kazi ipasavyo.

Abu Twalib alimpenda sana Mtume (s.a.w) kama vile alivyowapenda watoto wake bila ya kumbagua na wakati mwingine alizidisha mapenzi kwa Mtume (s.a.w) kuliko hata watoto maana likuwa halali mpaka anahakikisha Mtume (s.a.w) ubavuni mwake na mengine mengi ambayo yalionyesha ni jinsi gani anavyotilia umuhimu maisha ya Mtukufu Mtume (s.a.w).Hadi miezi michache kabla ya Hijra (yaani kabla ya kutoka Makka kwenda Madina), Abu Twalib (Mwenyeezi Mungu amrehemu) alikuwa akifanya kila awezalo kwa lengo la kuhakikisha anamhami Mtume Muhammad (s.a.w) na hakupumzika hata kidogo.

Kama walivyokuwa waarabu wengineo,waarabu wa Makka walijishughulisha na ufugaji mbuzi, kondoo na ngamia.Walikuwa pia wakifanya biashara na nchi jirani na Makka kama vile Syria.Walikuwa watu wasiojua kusoma wala kuandika na hawakufanya juhudu zozote zile za kuwaelimisha watoto wao.

Kama vile watu wake wote,Mtume Muhammad (s.a.w) pia hakuwa amejifunza kusoma wala kuandika,lakini tangu mwanzoni mwa maisha yake alifanikiwa kuwa na sifa nzuri sana na nyingi sana.Hakuwahi kuabudu masanamu,hakuwahi kusema uongo,hakuwa kuiba wala kupora mali za watu wala kufanya khiana.

Alijizuia na uovu,utovu wa nidhamu,pamoja na utovu wa adabu na vitendo vyote vya kuaibisha.Alikuwa mwerevu na mwenye bidii.Kwahiyo alipata umashuhuri sana na kupendwa sana na watu katika kipindi cha muda mfupi sana ambapo watu {kwa  harakaharaka} kutokana na tabia nzuri zisizokuwa na kifani walizoziona kwa Mtume Muhammad (s.a.w) na ambazo walikuwa hawajawahi kuziona kwa binadamu yeyote kabla yake ziliwafanya wakaamua kumbandika jina la “MUHAMMAD MWAMINIFU”.Kwa kawaida Waarabu walikuwa wakimwachia amana zao na kuzungumzia kila mara juu ya uaminifu wake na bidii yake.

Mtume Muhammad (s.a.w) alipokuwa na umri wa miaka karibia ishirini (20) Mwanamke mmoja,Tajiri mkubwa wa Makka,aliyekuwa akiitwa Khadija Al-kubra, baada ya kuona sifa nzuri za Mtume (s.a.w) na uaminifu wake wa hali ya juu, alimchangua Mtume Muhammad (s.a.w) kuwa mwakilishi wake katika masuala ya biashara zake.

Mwanamke huyu alipata faida kubwa sana kutokana na ukweli,uaminifu na busara na bidii ya Mtume Muhammad (s.a.w).Bila shaka Mwanamke huyu aliendelewa kuvutiwa zaidi na shakhsia na adhama ya Mtume Muhammad (s.a.w) na hatimaye kutoa pendekezo la kutaka kuolewa na Mtume Muhammad (s.a.w).Mtume Muhammad (s.a.w) alikubali pendekezo hilo,na katika umri wa miaka  ishirini na tano (25) akamuoa Mwanamke huyo aliyekuwa tajiri mkubwa.Miaka mingi baadaye,pia aliendelea kufanya biashara na Mtume Muhammad (s.a.w) ambaye sasa ni mumewe tiyari.

Akiwa akichukuliwa kuwa ni mmoja kati ya watu,Mjumbe wa Mwenyeezi Mungu (s.w) Mtume Muhammad (s.a.w) alikuwa na uhusiano wa kawaida na watu ahadi alipofikisha umri wa miaka arobaini (40).Bila shaka alikuwa akitofautiana na watu hao katika nukta kadhaa ambapo tunamkuta Mtume (s.a.w) alikuwa na sifa nzuri na aliepuka vitendo viovu na pia uhusiano mbaya uliowapoteza wengi.Mtume (s.a.w) Hakuwa mtu wa shari,hakuwa na moyo mgumu,hakujidai,hakuringa na wala hakujiona mbora kuliko wengine kitu ambacho kiliwafanya watu kumpa heshima kubwa na kumwamini.

Siku moja Waarabu walipokuwa wakijenga upya Kaaba Tukufu,kulitokea ugomvi mzito wa kutosikilizana kati ya makabila kuhusiana na uwekaji wa jiwe Jeusi mahala pake katika Kaaba hiyo Tukufu.Kila kabila linataka ndilo liwe lenye kuweka jiwe hilo katika mahala pake kwenye Kaaba hiyo Tukufu.Hivyo ikawa ni nivute nikuvute na amani ikawa iko hatarini kutoweka kati yao.Watu waote wakamchagua Mtume (s.a.w) kuwa msuluhishi wa ugomvi huo.

Mtume (s.a.w) aliwaamuru watu hao (waliokuwa wakivutana katika ugomvi huo ambao kidogo tu wapigane kama sio Mtume-s.a.w-kuwasuluhisha) waliweke jiwe hilo Jeusi {ALHAJARUL-AS-WAD} katika shuka lenye ncha nne,kisha akawaamuru wakuu wa makabila hayo kila mtu ashike pembe ya shuka hilo na kunyanyua shuka hilo juu.Wakuu wa makabila hayo wakafanya hivyo na kulinyanyua shuka hilo lililokuwa na jiwe hilo Jeusi kisha Mtume (s.a.w) akapanda juu ya kaaba mpaka usawa wa kukaa jiwe hilo na kulipokea jiwe hilo Jeusi na kuliweka mahala pake kwenye Kaaba hiyo Tukufu ambako mpaka leo hii jiwe hilo liko mahala pale.Kwa njia hii Mtume (s.a.w) akawa ameumaliza ugomvi na kukata mzizi wa fitina bila ya kutokea mauaji yoyote ya umati wala kumwaga damu.

Hata kama Mtukufu Mtume (s.a.w) alikuwa akimwabudu Mwenyeezi Mungu (s.w) na kujiepusha kuiabudu miungu kabla ya kubaathiwa au kabla ya kutumwa kuwa Mtume, watu hawakumjali kwa vile hakutangaza wazi wazi mapambano yake dhidi ya imani na itikadi (za kijaahiliyya) zisizokuwa na msingi.Hali hiyo pia ilihusika na wale waliokuwa wafuasi wa dini nyinginezo kama vile wayahudi, na wakristo ambao waliishi kwa heshima miongoni mwa Waarabu bila ya kusumbuliwa na Waarabu.

TUKIO LA MTAWA BUHAYRA HUKO SYRIA ALIPOKUTANA NA MTUME (S.A.W).

Mtume Muhammad (s.a.w) alipokuwa akiishi na Amu yake Abu Twalib na alipokuwa hajabalehe au hajabaleghe bado,Abu Twali (ambaye ni Ami yake au  Baba yake mdogo) alifanya safari ya kwenda Damascaus nchini Syria kwa lengo la kibiashara ambapo pia aliandamana na Mtume (s.a.w).

Ndugu msomaji,msafara huo ulikuwa ni msafara mkubwa sana tena sana na watu wengi walibeba bidhaa nyingi za kibiashara na tofauti tofauti hadi Syria na kuingia katika mji wa Busra.Baada ya kuuingia mji huu waliweka hema lao karibu na nyumba moja ya Utawa na kupumzika zao hapo.Mtawa mmoja aliyekuwa kijulikana kwa jina la “BUHAYRA” alitoka nje ya nyumba hiyo na kuwakaribisha au kuwaalika kwa chakula.Kila Mtu aliukubalimwaliko huo wa Mtawa huyo “Buhayra” na kuingia ndani ya nyumba hiyo ya kifahali.Abi Twalib naye alishiriki katika mwaliko huo lakini akamwachia mtoto wa kaka yake (yaani Mtume Muhammad s.a.w) bidhaa zake kisha ndio akajiunga na wenzake wote walioingia ndani ya nyumba hiyo ya utawa ili kuitikia mwaliko wa “Buhayra”.

Baada ya watu wote kuingia ndani,

Buhayra akauliza:

“Je kila mtu yuko hapa”.

Abu Twalib akajibu:

“Kila mtu yuko hapa ispokuwa kijana mdogo mmoja ambaye ni mdogo kwa umri kuliko wote”.

Buhayra alisema:

“Pia mlete”.

Abu Twalib alimwita Mtume Muhammad (s.a.w) ambaye wakati huo alikuwa amesimama zake chini ya Mzeituni (nje ya nyumba hiyo) ili aje kwa mtawa huyo.

Buhayra alimtazama Mtukufu Mtume (s.a.w) kwa uangalifu mkubwa sana na kumwomba amkaribie zaidi huku akimwambia kuwa alikuwa na jambo la kumwambia.Buhayra alimchukua Mtume (s.a.w) kando naye Abu Twalib hakuwaachia waende kando wawili tu bali aliwakaribia na kujiunga nao kando.

Buhayra alimwambia Mtume Muhammad (s.a.w):

“Nitakuuliza swali kwa kuapa kwa LAT na UZZA, je utanijibu?”

{LAT na UZZA yalikuwa ni majina ya miungu wawili waliokuwa wakiabudiwa na watu wa Makka}.

Mtume (s.a.w) alisema:

“Miungu hawa wawili ndio ninaowachukia sana”

Buhayra alisema;

“Kwa kuapa kwa Mwenyeezi Mungu,je utaniambia ukweli?”

Mtume Mtukufu (s.a.w) ambaye ni rahma kwa walimwengu wote akajibu kwa kumwambia:

 

“Daima mimi husema ukweli na sijawahi kusema uongo;uliza swali lako”.

Buhayra akaanza kuuliza:

Mwisho wa sehemu ya kwanza.

Usikose sehemu ya pili kuhusiana na maswali ya Buhayra kwa Mtume (s.a.w) na majibu ya Mtume (s.a.w) kwa Buhayra.

Nimaswali mazuri kutoka kwa Buhayra na ni majibu mazuri kutoka kwa Mtume (s.a.w).Yote hayo utayajua ukifuatilia sehemu ya pili ya maisha ya Mtume (s.a.w) itakuwayo kuja hivi punde Inshaallah.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini