Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

MWEZI MTUKUFU WA RAMADHAN KATIKA QURANI

0 Voti 00.0 / 5

MWEZI MTUKUFU WA RAMADHAN KATIKA QURANI

Ramadan inatajwa katika Quran kwenye Sura 2 aya 185 inayosema:
Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa ni wongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Basi ataye kuwa mjini katika mwezi huu naafunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru.
Kufuatana na mapokeo ya kiislamu Muhammad alianza kupokea ufunuo wa aya za Qurani katika kipindi cha Ramadhani. Kutokana na historia hii Waislamu huangalia Ramadhani kama mwezi mtakatifu katika kalenda ya Kiislamu.
Kuna wataalamu wanaoona ya kwamba kutokea kwa utaratibu wa kufunga mwezi mzima uliathiriwa na desturi ya kufunga katika Kanisa la Syria. Kufuatana na Bukhari, Waarabu asilia na Wayahudi wa Uarabuni kabla ya kuja kwa Uislamu walifunga kwa siku chache tu, kwa mfano siku ya Ashura [1] [2] [3]
KUSOMA QURANI
“Mwezi wa Ramadhani ambayo imeteremshwa ndani yake Qur-an hali ya kuwa ni uongofu kwa watu …………" Kwa kuwa katika mwezi huu ndio Qurani iliteremshwa kwa Mtume, inatakiwa kwa muislam kufanya bidii kuisoma angalau juzuu moja kwa siku ili aweze kumaliza msahafu ifikapo mwisho wa mwezi huu wa Ramadhan.
KUHARAKISHA KUFUNGUA
Miongoni mwa sunna tukufu zinazotakiwa kwa mfungaji katika mwezi huu kuzikimbilia, ni kuharakisha kufungua baada tu ya kuzama jua, kwani Mtume amesema katika hadithi iliopokewa na Tirmidhy, Ibnu khuzayma na Ibnu Habban: “Hakika nimpendaye zaidi miongoni mwa waja wangu ni anayefanya haraka katika wao kufungua saumu.”
KUSALI USIKU
Inatakiwa kwa muislam kuyatumia masiku ya mwezi huu mtukufu katika kumuabudu Allah kwa kusali na kufanya ibada nyengine, kwani ni mwezi wa pekee ambao ndani yake kunapatikana usiku wa cheo (Laylatul Qadr) ambao ibada ya usiku huo inalingana na ibada ya miezi elfu moja, na kwa hekima yake Allah hakutubainishia kuwa ni usiku wa tarehe ngapi. Na hii ni moja miongoni mwa fadhila za kusali katika masiku ya mwezi huu. Vile vile mwenye kusimama kwa ibada katika masiku haya husamehewa makosa yake yote yaliyotangulia, kama alivyosema Bwana Mtume: “Mwenye kusimama usiku wa Ramadhani kwa kufanya ibada hali ya kuwa na imani na kutaraji thawabu anasamehewa yoteyaliotangulia miongoni mwa makosa yake.” (Bukhari na Muslim).
KULA DAKU
Kula daku vilevile ni miongoni mwa sunna tukufu zinazodharauliwa na wengi kati ya waislam na fadhila zake ni kubwa kupita kiasi, miongoni mwazo ni kurehemewa na Allah na kutakiwa msamaha na malaika watukufu kama alivyosema Mtume katika hadithi: “Hakika Allah na Malaika wake wanawarehemu wenye kula daku.” (Twabrani, Ibnu Habban).
Vile vile Mtume amesisitiza katika hadithi kwa kusema kuwa: “Hakika daku ni baraka amekupeni Allah, hivyo basi musiiache”. (Annasai)
KUKAA ITIKAAF
Inatakiwa kwa muislam kuujaalia mwezi huu na kuutumia katika kuchuma na kuvuna aina tofauti ya mema ikiwemo Itikaaf, kwani ni miongoni mwa ibada bora sana zinazomkurubisha mja kwa Mola wake hasa awapo katika mwezi huu wa Ramadhani, kwani baadhi ya wanavyuoni wamesema kuwa haisihi ibada hii ya itikaaf pasi na funga. Na yatoshe malipo makubwa yaliotajwa katika hadithi; Mtume amesema: “Mwenye kukaa itikaaf siku kumi katika mwezi wa Ramadhani, basi ni kama aliyehiji na akafanya umra mara mbili mbili." (Bayhaq)
KUTOA SADAKA
Miongoni mwa ibada tukufu alizokuwa akizifanya Mtume ni kutoa sadaka na alilipa umuhimu sana jambo hili hadi wakati wa kuondoka kwake ulimwenguni alipokuwa katika sakaratul mauti kila alipopata fahamu ilikuwa akimuuliza Bibi Aisha iwapo ashazitoa sadaka zile dirhamu nne zilizokuwa nyumbani? Kadhalika kutoa huku kwake kulikuwa kukiongezeka katika Ramadhani.
KUMTAJA ALLAH
Katika mwezi huu wa Ramadhani kadhalika inatakiwa kwa muislam kuwa mengi ya maneno yake yawe katika kumtaja Allah (Subhaanahu wa Ta’ala), kwani ni jambo ambalo linasaidia katika kuusafisha moyo wake na kuiboresha funga yake. Allah ametuamrisha tumtaje kwa wingi katika aya nyingi za Qurani, na hii ndio ibada pekee aliyosema Allah kuwa ifanywe kwa wingi, na miongoni mwa aya hizo; “Enyi Mlioamini mtajeni Allah kwa wingi na mumtakase yeye asubuhi na jioni.” (Al- Ahzaab 41 na 42)
Kadhalika Mtume alifundisha aina tofauti za kumtaja Allah ili tusichoke na jambo hili kwani mwanadamu ni mwepesi wa kuchoka na jambo moja tu. Vile vile akatuonyesha tofauti kubwa iliopo kati ya anayemtaja Allah na asiyefanya hivyo kati hadithi aliposema; “Mfano wa anayemtaja Allah na asiyemtaja ni mfano wa mtu aliyehai na aliyekufa.” (Bukhari).
Haya ni baadhi ya yanayotakiwa kufanywa na muislam, hasa awapo ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, hivyo basi tujihimu katika kuyatekeleza haya tuliyoelezwa na tumuombe Allah atutakabaliye matendo yetu “Amin”.
Marejeo

•  Bukhari-Ibn-Ismail, AbdAllah-Muhammad. "Sahih Bukhari - Book 031 (The Book of Fasting), Hadith 222.". hadithcollection.com. Retrieved 19 July 2012.
•  Bukhari-Ibn-Ismail, AbdAllah-Muhammad. "Sahih Bukhari - Book 031 (The Book of Fasting), Hadith 223.". hadithcollection.com. Retrieved 19 July 2012.
•  Bukhari-Ibn-Ismail, AbdAllah-Muhammad. "Sahih Bukhari - Book 031 (The Book of Fasting), Hadith 220.". hadithcollection.com. Retrieved 19 July 2012.

 

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini