Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

KUUNGANISHA SALA MBILI

0 Voti 00.0 / 5

KUUNGANISHA SALA MBILI
KWA NINI MASHIA HUSALI KWA KUUNGANISHA SALA KWA PAMOJA DHOHR – ASR NA MAGHRIB – ISHA
Baadhi ya watu huuliza ni kwa nini Mashia’ husali kwa kuunganisha pamoja sala ya Adhuhuri – Alasiri na Maghrib – ‘Isha wakati ambapo wengi wa Waislamu husali kwa kutenganisha sala hizo ?
Kwa kulijibu swali hili sisi tutawaleteeni kwa mapana maamrisho yote tunayoyafuata yanatokana na kumfuata Mtume Muhammad s.a.w.w.
Ama kuhusu sala, namna ya kusali, nyakati zake na namna ya kufanya wudhu na shariah zote zimetokana na Qur’n, Mtume Muhammad s.a.w.w.na Ahlul Bayt a.s.
Ingawaje Madhehbu mengine yanadai kuwa wanafuata Quran na Sunnah, lakini madai yao matupu bila ya uthibitisho, haiwezi kuthibitisha ukweli wowote. Kwa hakika sisi tunavyofuata kwa vithibitisho na Sunnah, ni kwa hakika kweli na hakiki kwa kutokana na shakhsiyyah wenyewe i.e. Ahul-Bayt a.s. ambao ni wananyumba ya Mtume Muhammad s.a.w.w. na ambao walikuwa wakiishi nae na walijua kila kitu kuhusu misemo na matendo yake yote. Bila shaka hakuna wa kukana ukweli na uhakika huu !
Kutafsiri na kuielewa Quran Tukufu inategemea sana Ahadith. Na hapa ni lazima kabisa kutegemea Ahadith zile zilizo sahihi na kweli (zisiwe zimebuniwa ). Hakuna shaka kuwa sisi Mashia’ tunafuata Sunnah sahihi na kweli kabisa ambayo tumeipokea kutoka kwa Ahlul Bayt a.s. ya Mtume Muhammad s.a.w.w. na ndiyo mwongozo wetu sahihi wa kuifuata Qur'an Tukufu na Mtume Muhammad s.a.w.w. .

NAMNA YA KUSALI
Inambidi kila Mwislamu amfuate Mtume Muhammad s.a.w.w. kwa kikamilifu katika maamrisho na matendo yake kuhusiana na imani, ‘ibadah, matendo na tabia zake. Lakini kwa kutokana na sababu makhsusi za umuhimu wa Sala, ikiwa ndiyo nguzo ya Dini ya Kiislamu, Mtume Muhammad s.a.w.w. ametuamrisha na kutusisitiza sisi tusali vile alivyokuwa akisali yeye mwenyewe bila ya kufanyiwa mabadiliko. Kwa haya hali zifuatazo zinaweza kujitokeza Mambo yote yatakuwa faradhi (wajib) ambayo Mtume Muhammad s.a.w.w. alikuwa akiyatenda mfano kusoma kwa Sura-al-Hamd katika rakaa ya kwanza ya kila sala. Hii ni wajib hivyo haimbidi Mwislamu yeyote kuiacha kwa makusudi.
Vivyo hivyo, mambo na matendo yote ambayo yalikuwa hayakutendwa na Mtume Muhammad s.a.w.w. basi yatakuwa Haraam kuyatenda mfano Kusali kwa kuunganisha Dhohr na ‘Asr na Maghrib na ‘Isha iwapo Mtume Muhammad s.a.w.w. alikuwa hakusali hivyo.
Iwapo Mtume Muhammad s.a.w.w. alikuwa akitenda mambo fulani mara zingine, inamaanisha kuwa jambo hilo lilikuwa limepewa ruhusa katika Shariah mfano, Kusali sala Msikitini au nyumbani, kusoma kwa sura ndefu au fupi baada ya Sura al-Hamd katika rakaa mbili za mwanzoni mwa sala, kusali Dhuhuri na ‘Asr au Maghrib na ‘Isha kama ilivyokuwa akisali Mtume Muhammad s.a.w.w. mwenyewe mara nyingi, kwa hiari yake na kwa makusudi bila ya kuwapo na sababu ya kumlazimu kusali hivyo kama mvua, safari, vita au Hajj, n.k.
Sisi hatudai kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. alikuwa daima akisali hivyo kwa kuunganisha sala mbili kwani kama ingalikuwa hivyo basi ingalikuwa Wajib kwa Waislamu wote kusali hivyo hivyo tu. Lakini kwa kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. mwenyewe alikuwa amesali kwa kuunganisha sala mbili mara nyingi bila ya sababu ya kumlazimisha, hivyo inamaanisha kuwa kusali hivyo kwa kuunganisha kunaruhusiwa. Vile vile inamaanisha kuwa hivyo ni Sunnah ya Mtume Muhammad s.a.w.w. Sisi tunaamini kuwa si faradhi kusali sala hizo daima kwa kuunganisha, kwa sababu Mtume Muhammad s.a.w.w. mwenyewe alikuwa akizisali mbali mbali mara zingine.
Sisi tunastaajabishwa mno kusikia kuwa baadhi ya Waislamu wanathubutu kusema kuwa kusali huku kwa kuunganishwa kumeharamishwa, bila ya kujali kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. mwenyewe alikuwa akisali hivyo. Kwa kuwa lilikuwa ni tendo la Mtume Muhammad s.a.w.w. mwenyewe basi ni Sunnah pia kumfuata. Kwa kusadiki na kuamini na kufuata matendo yake, sisi kwa hakika ndio tunaofuata Sunnah yake., kwa sababu ni wajib kumfuata Mtume Muhammad s.a.w.w. sio kwa swala hili tu bali katika kila maswla.
Jambo ambalo ndugu zetu Waislamu wanalolipinga ni kuhusu wakati wa sala zote hizo. Hivyo naomba tuyazungumzie hayo kutokea Ayah za Qur'an Tukufu.

WAKATI WA SALA KATIKA QUR’AN TUKUFU
Sisi tutapenda kurejea katika Qur'an Tukufu na kuona wakati wa Sala ulioelezwa na Allah swt kwa ajili ya Waislamu.
Katika Sura Bani Israil , 17, Ayah ya 78 Allah swt anatuambia :
‘ Simamisha Sala jua linapopinduka (likaenda Magharibi) mpaka giza la usiku; usomaji wa alfajiri; kwa hakika unashuhudiwa.’
Katika Ayah hii Allah swt kwa waziwazi anatuelezea wakati wa sala kama zifuatazo :
Linapopinduka jua : Yaani ni kuanza kwa wakati wa sala za Adhuhuri na ‘Asr.
Giza la usiku : Yaani ni mwanzo wa Sala za Magharib na ‘Isha.
Itabidi kuzingatia kuwa wakati wa Magharib na wakati wa kufuturu Saumu kunatofautiana baina ya Mashia’ ambao ndio wafuasi halisi wa Ahlul Bayt a.s. ya Mtume Muhammad s.a.w.w. na Waislamu ambao wengi ni wafuasi wa Abu Hanifa, Shafii, Maliki na Hanbali.
Mashia’ wanaamini kuwa wakati wa Maghrib unaanza baada ya kupotea mwanga mwekundu katika magharibi, ambayo ni mng’ao wa mwanga wa jua ambapo jua huwa halionekani. Hii ni dalili kuwa wakati wa Sala ya Maghrib ndio mwanzo wa usiku, na ndio wakati halisi ambao Mashia wanaoufuata.
Usomaji wa alfajiri : Ni wakati wa Sala ya alfajiri. Ama kwa mujibu wa Ahadith Usomaji wa alfajiri kwa hakika inashuhudiwa kwa sababu Malaika wa Usiku na Malaika wa Siku, wote wanashuhudia Sala ya Alfajiri.
Hivyo ni dhahiri kabisa, kwa mujibu wa Ayah hii kuwa wakati muhimu kabisa za Sala zipo tatu :
1. Dhuhuri na ‘Asr
2. Maghrib na ‘Isha
3. Sala ya Al-Fajr.
Vile vile Allah swt anatuambia katika Sura al-Hud , 11, Ayah ya 114 kuwa :
‘ Na simamisha Sala katika ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zilizo karibu na mchana. Hakika mema huondoa maovu. Huu ni ukumbusho kwa wanaokumbuka.’
Katika Ayah hii pia tumepatiwa nyakati tatu za Sala kama ifuatavyo :
Kwanza na pili : Sehemu za siku, yaani asubuhi ambayo ndiyo kianzio cha siku, na mchana ambayo ndiyo sehemu ya pili ya siku, na ambazo ndizo nyakati za kuanza sala za Adhuhuri na ‘Asr.
Tatu : Masaa ya kwanza ya usiku ; ambayo ndiyo wakati wa Sala za Magharib na ‘Isha.
Kwa mara nyingine tena imetuwia waziwazi kuhusu nyakati za Sala kutokea Qur'an Tukufu kuwa kuna nyakati tatu maalumu za Sala.
Kwanza : Kunapoanzia mchana hadi kabla ya kuzama kwa jua ndiko wakati wa Dhuhur na ukifuatiwa na ‘Asr.
( kunapokucha na kuchwa kwa jua, chukua masaa yote uyagawe kwa mbili ndipo utakapopata wakati huu tunaouita kuanza kwa Dhohr au mchana tunavyouita hapa)
Pili : Kutokea kuzama kwa jua ya uhakiki ambapo ndiko kunakoanza usiku ndio wakati wa Sala ya Maghrib ikifuatiwa na Sala ya ‘Isha.
Tatu : Sala ya Alfajiri.

NYAKATI ZA SALA ZA MTUME MUHAMMAD S.A.W.W.
Ingawaje Waislamu wanakubaliana na kuunganishwa kwa nyakati za Sala za Adhuhuri na ‘Asr na Maghrib na ‘Isha, lakini wasio Mashia’ wanadai kuwa kuunganishwa huku imeruhusiwa katika hali fulani fulani tu kama vile msimu wa mvua, safarini hususan katika Hijja (‘Arafat) au katika hali ya ugonjwa au vitani. Ambapo Mashia’ wanatoa ushahidi uliomadhubuti na mkweli kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. aliunganisha na kusali sala hizi bila ya kuwa na matatizo hayo.
Zipo Ahadith mbalimbali za Mtume Muhammad s.a.w.w. na Ahlul – Bayt a.s. katika vitabu muhimu na za Ahadith (Kutub-eArbaa’) mfano al-Kafi, al-Faqih, al-Istebsaar na al-Tahdhib kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. alikuwa akizisali sala za Dhuhuri na ‘Asr na Maghrib na ‘Isha kwa pamoja katika siku za kawaida bila ya kuwapo na sababu ya kufanya hivyo. Kwa kuwa vitabu hivyo ni vya Mashia’, sisi tutawaleteeni marejeo kutokea vitabu vya Ahl Sunnah (Masunni) ambavyo vinasadikiwa kuwa ni Sahih na ndizo chanzo cha Shariah baada ya Qur'an Tukufu .
Hadith ya kwanza : Katika Sahih Muslim na Sahih Bukhari, ni vitabu vinavyoaminiwa sana na Masunni baada ya Qur'an Tukufu -- katika sura (kuunganisha sala mbili ) kwa kumnakili Ibn ‘Abbas amabye amesema kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. alisali sala mbili za Dhuhuri na ‘Asr kwa kuunganisha huko Madina bila ya kuwa na udhri wowote wa khofu na wala hakuwa safarini.
Wakati Ibn ‘Abbas alipoulizwa ni kwa nini Mtume Muhammad s.a.w.w. alisali kwa kufanya hivyo? Yeye alijibu : “Yeye hakutaka mtu yeyote kutokea ‘Ummah wake apate shida.”
Hadith ya pili : Katika Sahih Bikhari, ambacho ndicho kitabu bora kabisa miongoni mwa Masunni, imeandikwa katika sura ya kuchelewesha sala ya Adhuhuri hadi ‘Asr kwa kumnakili Ibn ‘Abbas ambaye alisema kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. alisali rakaa saba akiwa huko Madina na rakaa nane (Yaani aliunganisha sala ya Maghrib, rakaa tatu na ‘Isha rakaa nne na vile vile Adhuhuri, rakaa nne na ‘Asr rakaa nne ).
Hadith ya tatu : Katika Sahih Bukhari, vile vile tunamnakili Ibn ‘Abbas ambaye anaelezea kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. alisali kwa kuunganisha sala ya Maghrib na ‘Isha na sala ya Adhuhuri na ‘Asr bila ya kuwa na sababu yoyote ya khofu au safari. Na pale alipoulizwa ni kwa nini amefanya hivyo, alijibu : “Mtume Muhammad s.a.w.w. hakutaka kuwasababishia magumu kwa ‘Ummah wake.”
Hadith ya nne : Al-Tabarani kutokea kwa ‘Abdullah Ibn Mas'ud alisema kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. alisali kwa kuunganisha sala za Adhuhuri na ‘Asr na maghrib na ‘Isha, na pale alipoulizwa ni kwa nini alisali kwa kuunganisha ? Yeye alijibu : “Mimi nimefanya hivyo kwa kutokuwaingiza ‘Ummah wangu katika ugumu.” Hadith hii imeelezwa na al-Zarqani katika Sharh al-Muwatta’a, j.1, uk.263.
Hadith ya tano : Wakati ‘Abdullah ibn ‘Umar alipoulizwa ni kwa nini Mtume Muhammad s.a.w.w. alikuwa akisali sala kwa kuunganisha pamoja kwa sala za Adhuhuri na ‘Asr na vile vile Maghrib na ‘Isha bila ya kuwa safarini au kuwa na khofu ya aina yoyote ? Yeye alijibu : “Mtume Muhammad s.a.w.w. alikuwa hataki kuiingiza ‘Ummah wake katika magumu.” Hadith hii imeelezwa katika kitabu mashuhuri kiitwacho, Kanz al-‘ummal, j.4, uk.242.
Hadith ya sita : Katika Sahih Muslim imesemwa kuwa Ibn ‘Abbas alisema : “Sisi tulikuwa tukisali sala mbili kwa kuunganisha pamoja katika zama za Mtume Muhammad s.a.w.w. .”
Inatubidi tuangalie kwa makini kuwa Muslim katika Sahih yake ameweka Sura maalum (ya kuunganisha sala mbili kwa pamoja bila ya kuwa safarini ) ambamo amezielezea ahadith sahihi zaidi ya kumi huku akithibitisha kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. alikuwa akisali sala kwa kuunganisha bila ya vipingamizi vya aina yoyote au kwa sababu zozote.
Sababu za kuunganisha sala mbili imeelezwa kwa uwazi katika Ahadith kuwa kutokuuweka ‘Ummah katika magumu , kwa sababu tunaona kuwa kusali sala za Adhuhuri mbali na Sala ya ‘Asr na Maghrib na ‘Isha kunaleta ugumu mara nyingi, hususan kwa tabaka la watu wanaofanyakazi na watu ambao wako mashughuli. Matatizo kama haya kwa watu kama hawa kunaweza kuwafanya wasiweze kusali sala zao za siku.

BAADHI YA FAIDA MUHIMU
Kuunganisha sala mbili ni hali na neema itokayo kwa Allah swt kwa waja wake kwa sababu Allah swt anajua kuwa hali hii ndiyo ya hakika ya kusali kwa waja wake wengi katika hali mbalimbali. Hakuna mtu yeyote aliye na haki ya kuweka vipingamizi katika amri hii ya Allah swt yenye neema ambayo ilikuwa ikitekelezwa na Mtume Muhammad s.a.w.w. kwa mara nyingi.
Ipo riwaya kuwa siku moja mtu mmoja alileta malalamiko kwa al-Imam Hassan al ‘Askari a.s. kuwa yeye alikuwa tajiri lakini akafilisika na kuwa masikini. Imam a.s. alimwambia, “Unganisha sala mbili, na hapo utakipata kile ukitakacho.” (Wasa’il al-Shiah, j.2, uk.162 ).

KWA KUKAMILISHA
Kwa mujibu wa vithibitisho tulivyoviona hapo juu kutoka Qur'an Tukufu na Ahadith sahih, na hivyo imedhihirika kwetu waziwazi kuwa kuunganisha kwa sala za Dhuhuri na ‘Asr na Maghrib na ‘Isha ndiyo kwa hakika Sunnah Sahihi na ndivyo Mtume Muhammad s.a.w.w. alivyokuwa akisali na kwa maana hiyo ndivyokumfuata. Wale wanaokanusha kwa hakika wanakanusha Sunnah hakika na wanapinga kile alichokuwa akikitenda Mtume Muhammad s.a.w.w. mwenyewe. Na wale wanaoifuata basi wanaifuata Islam kwa uhakika i.e. Mashia’, wanamfuata Mtume Muhammad s.a.w.w. pamoja na maneno na matendo yake aliyokuwa akiyatenda (yaani wanafuata nyayo zake).

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini