Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

DU’A YA MWEZI WA RAMADHANI (SEHEMU YA 6)

0 Voti 00.0 / 5

DU’A YA MWEZI WA RAMADHANI (SEHEMU YA 5)
اللّهُمَّ فَرِّجْ عَنْ كُلِّ مَكْرُوبٍ
Ewe Mola Mfariji Kila Mwenye Huzuni
MAANA YA ‘MAKRŪB’
Neno ‘Makrūb’ ni shamirisho ya jina ambalo asili yake ni kitenzi cha jina ‘karb’ lenye maana ya ‘huzuni nyingi’.
Allāma Tabātabā’i katika kitabu chake ‘al-Mizān’, anamnukuu Sheikh Rāghib Isfahāni, Mtaalamu mashuhuri wa kuandika kamusi ya maneno ya Qur’an, akisema ya kwamba:
الْكَرْبُ الغَمُّ الشَّدِيْدُ
“Karb maana yake ni ‘huzuni kubwa”.1
Neno ‘karbala’ kwa mfano, limejengeka kutokana na neno (Karb) huzuni na majonzi na (balā) mtihani.
Hivyo basi kwa ufupi, Makruub,’ ni mtu ambaye ana huzuni nyingi na majonzi.
CHANZO CHA HUZUNI
Katika sehemu hii ya dua, tunamuomba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) Kwa unyenyekevu awaondolee wote hali ya kuwa na ‘huzuni na majonzi’ wale wote walioko kwenye hali hii. Yeyote anayeomba kuondolewa kwa huzuni na majonzi anaomba pia kuondolewa kwa sababu ambazo pia husababisha huzuni. Hata hivyo ni lazima tuelewe kwamba, sababu za huzuni zinatafautiana kulingana na watu na mazingira tofauti. Kwa mfano, wale wenye ukaribu na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) japokuwa hawana huzuni kwa kuikosa dunia na starehe zake:
أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ
“Hakika marafiki (vipenzi) vya Allah hawaogopi wala hawahuzuniki” (Qur’an 10:62)
Hupatwa na huzuni kwa yale yatakayo wafika makafiri katika siku za usoni (Allah anamwambia Mtume Wake):
أَفَمَنْ زُيِّنَ لَهُ سُوءُ عَمَلِهِ فَرَآهُ حَسَنًا ۖ فَإِنَّ اللَّهَ يُضِلُّ مَنْ يَشَاءُ وَيَهْدِي مَنْ يَشَاءُ ۖ فَلَا تَذْهَبْ نَفْسُكَ عَلَيْهِمْ حَسَرَاتٍ ۚ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ بِمَا يَصْنَعُونَ
“Basi roho yako isitoke kwa majonzi juu yao…”2 (Qur’an 35:8)
Imam Khomeini (r.a.) katika kitabu chake maarufu kiitwacho ‘Hadithi al-Arbain’ anasema:
“…Yeyote ambaye ameweza kutambua utukufu wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa kiwango kikubwa na akavijua vituo vitukufu vya Allah (s.w.t.) zaidi ya wengine, huwa anaumia zaidi na kuteseka kwa kiwango kikubwa sana kwa dhambi za viumbe na makosa yao dhidi ya utukufu wa Mwenye Mungu (s.w.t.). Vile vile, yule mwenye mapenzi na huruma kwa viumbe wa Mwenyezi Mungu huteseka kwa kiwango kikubwa mno kwa uhalifu wao na hali zao mbaya za kimaisha. Na bila ya shaka Mtume wa mwisho (s.a.w.w.) alikuwa amekamilika zaidi katika vituo vyote hivi na alikuwa juu kuwashinda Mitume wote na Mawalii kwa kiwango chake cha ukamilifu na ubora. Hivyo kuteseka kwake na kuhuzunika kwake kulikuwa kukubwa kuliko yeyote katika hao…”
Wakati mwingine sababu ya huzuni huwa tofauti. Kwa mfano kuhusiana na Mtume Ayyub (a.s.), tunasoma yafuatayo katika moja ya dua za mwezi wa Ramadhani:
يَا مُلَيّنَ الحَدِيدِ لِدَاوُدَ عَلَيْهِ السّلامُ يَا كَاشِفَ الضُّرّ وَالكُرَبِ العِظَامِ عَنْ أَيّوبَ عَلَيْهِ السّلام
“Ewe mlainishaji wa chuma kwa Daudi (a.s.), Ewe Muondoaji wa huzuni na majonzi makubwa kwa Ayyub (a.s.)…”
Hii inayonyesha kwamba Mtume Ayyub (a.s.) alipata misiba mikubwa katika uhai wake, kama hadithi ifuatayo inavyo tuonesha:
Ali bin Ibrahim anaelezea katika hadithi ndefu aliyoipokea kutoka kwa Abu Basir kwamba, Imam al-Sadiq (a.s.) amesema:
“…Kisha mwili wake (Mtume Ayyub (a.s.)) wote, ila akili na macho, ulipatwa na ugonjwa. Kisha ibilisi aliupulizia ukawa kidonda kimoja kutoka kichwani hadi miguuni. Alibakia (Mtume Ayyub (a.s.)) katika hali hiyo kwa muda, akimhimidi na kumshukuru Mwenyezi Mungu, mpaka akatokwa na wadudu mwilini. Na mdudu alipokuwa akianguka kutoka kwenye mwili wake, alikuwa akimrudisha na kumwambia,’Rejea kwenye sehemu yako alipo kuumbia Mwenyezi Mungu’, na alianza kutoa harufu mbaya, wakazi wenzake wa mji wakamfukuza kutoka kwenye mji ikawa chakula chake anakipata kutoka kwenye mazubala yaliyotupwa nje ya mji”.3
Vile vile ‘huzuni kubwa’ imetajwa kuhusiana na Mtume Nuhu (a.s.). Tazama aya ifuatayo:
وَنُوحًا إِذْ نَادَىٰ مِنْ قَبْلُ فَاسْتَجَبْنَا لَهُ فَنَجَّيْنَاهُ وَأَهْلَهُ مِنَ الْكَرْبِ الْعَظِيمِ
“Na Nuhu alipotulingania zamani (kutuomba), nasi tukamuitikia, na tukamuokoa yeye na watu wake kutoka kwenye shida kubwa”. (Qur’an 21:76)
Wafasiri wa Qur’an wana tafsiri mbali mbali kuhusiana na sababu ya huzuni hii. Baadhi yao kama vile Tabarsi katika ‘Majma’ al-Bayān’ anasema kwamba imetokana na maudhi aliyoyapata (Nabii Nuh (a.s.) kutoka kwa watu wake, ambapo Mawlā Kāshāni anasema kwamba yawezekana sababu ziwe ni zote mbili, maudhi ya watu wake na mafuriko makubwa.
Hata hivyo, baadhi ya vyanzo vya huzuni hutokana na udhaifu wa imani na mapenzi ya dunia: kwa sababu mtu hana anasa za maisha ambazo wengine huonekana kuzifaidi, unaweza kumuona ana huzunika. Kwa mfano wale wanao jiuwa kutokana na huzuni nyingi na majonzi, hufanya hivyo kwa ukosefu wa subira au ‘lengo’ katika maisha. Kwa hiyo sio kila makrūb ni sawa.
Kwa hiyo, muombaji lazima atilie maanani sababu tofauti za huzuni na majonzi, na kwa unyenyekevu amuombe Allah amuondelee kama ipasikanavyo. Kwa mfano, kwa yule ambaye huzuni yake inasababishwa na ukosefu wa mambo ya ziada ya starehe za kidunia, anatakiwa amuombe Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amuondolee mapenzi ya dunia katika moyo wake. Na yule ambaye amekumbwa na hali ya umasikini, amuombe Allah (s.w.t.) amtekelezee haja zake ili aweze kuyashughulikia mambo yake ya kila siku kwa bidii akiwa na utulivu moyoni; na mwenye kusumbuliwa na maradhi, aombe kuondolewa maradhi hayo, ili aweze kuwa na amani na utulivu utakao mwezesha kufanya mema yatakayomtengenezea akhera yake.
KUWAKUMBUKA WANAO HUZUNIKA LEO
Kuyajua yanayo endelea ulimwenguni kwa sasa, huenda kukakosa umuhimu kwa baadhi ya watu. Kwa mfano mtu anajiuliza, nifanye nini kama watu wengine wanakufa kwa njaa Afghanistani? Sina namna ya kuwahudumia, kwa hivyo kujua hali mbaya waliyonayo na kutoijua hakuna tofauti yeyote.
Bila ya shaka fikra kama hii inatokana na mtazamo mfinyu. Kwa kuwa mwandamu ana uwezo wa kumtakia uongofu mwanadamu yeyote mwengine. Kwa hivyo kutojali ni fikira ngeni kwenye asili yake. ‘Kutoweza kuwasaidia wanaodhulumiwa’ sio sababu ya kutokujali kwa upande wetu.
Kwanza, dhamiri zetu zingelipenda kujua hali ya ndugu zetu walio na shida ulimwenguni.
Pili, kama hatuna uwezo wa kimali, Allah (s.w.t.) ametufungulia mlango wa dua. Na kwa kupitia maombi kwa ajili ya wenye shida kwa kweli mambo yanaweza kubadilika.
Tatu, kuna mambo mengi ambayo tunaweza kuyafanya kwa pamoja ili kuvunja uwezo wa kiburi cha ulimwengu, lakini hatulitambui hilo.
Kwa mfano, wafanyaji biashara wetu ambao huagiza bidhaa kutoka kwenye nchi kama vile Israel kwa bei ya chini, wanaweza kuacha shughuli kama hizo ili wasichangie katika kuwaua wapalestina wasio na hatia. Vile vile wengi wetu kwa njia ya kuzunguka hutangaza bidhaa zinazotengenezwa na ukiburi wa ulimwengu. Kama tungezigomea bidhaa hizo, zisingeweza kusitawi kama zilivyo sasa. Leo, lau viongozi wa kiarabu wataamka na waache kunyenyekea huu ukiburi wa ulimwengu, bila ya shaka mabadiliko mengi yatapatikana.
JUKUMU LA KIBINAFSI
Lakini jukumu langu ni nini kama mtu binafsi ninapoisoma sehemu hii ya du’a? Wengi wetu wana uwezo wa kiwango fulani na wanaweza kuathiri ipasavyo. Kwa hivyo tuipime nguvu tuliyo nayo kwa matumizi yetu, na tuchukue hatua kivitendo kwa kuwaondolea shida na huzuni wale ambao tunaweza kuwasaidia. Kwa kuwa hatujakalifishwa kulifanya lililo nje ya uwezo wetu, kama Qur’an inavyotuambia katika (Al-Baqara – 2:286):
لَا يُكَلِّفُ اللَّهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا ۚ لَهَا مَا كَسَبَتْ وَعَلَيْهَا مَا اكْتَسَبَتْ ۗ رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِنْ نَسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا ۚ رَبَّنَا وَلَا تَحْمِلْ عَلَيْنَا إِصْرًا كَمَا حَمَلْتَهُ عَلَى الَّذِينَ مِنْ قَبْلِنَا ۚ رَبَّنَا وَلَا تُحَمِّلْنَا مَا لَا طَاقَةَ لَنَا بِهِ ۖ وَاعْفُ عَنَّا وَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا ۚ أَنْتَ مَوْلَانَا فَانْصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ
“…mwenyezi mungu haikalifishi nafsi yeyote ila kwa kiasi cha
uwezo wake…”
Hivyo kama nina uwezo wa kuisaidia familia fulani na kuiondoa kwenye huzuni, inanipasa kufanya hivyo. Na ikiwa mimi ni kiongozi wa jamii fulani na ninaweza kuwaondolea huzuni wale wanaosumbuka kutokana na ‘utaratibu mbaya wa kijamii’ ulioko katika jamii hiyo, itanipasa kufanya hivyo kwa kuweka utaratibu mzuri unaofaa. Na orodha inaendelea hivyo hivyo (kila mtu na nafasi yake katika jamii). Ufumbuzi zaidi unapatikana kulingana na uwezo alionao muombaji dua. Vinginevyo kuisoma sehemu hii ya du’a itakuwa haina faida yeyote ila mtu kuchezesha ulimi tu, au kuonyesha unafiki wa mtu; Mwenyezi Mungu atuepushe na aibu kama hiyo.
KUZIFURAHISHA NYOYO ZA WAUMINI
Kumfurahisha mu’umini kwa kumuondolea huzuni aliyonayo moyoni ni moja katika mambo muhimu ambayo vitabu vyetu vya hadithi vinaelezea kwa upana. Zifuatazo ni baadhi ya hadithi zinazofaa tafakari:
1. Imepokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.) kwamba:
مَنْ سَرَّ مُؤْمِنًا فَقَدْ سَرَّنِي، وَ مَنْ سَرَّنِي فَقَدْ سَرَّاللّه
“Atakaye mfurahisha mu’umini basi amenifurahisha mimi na atakaye nifurahisha mimi basi amemfurahisha Allah (s.w.t .).”4
2. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema pia:
إنَّ فِي الْجَنَّةِ دَارًا يُقَالُ لَهَا دَارُ الْفَرَحِ لَا يَدْخُلُهَا إلاَّ مَنْ فَرَّحَ يَتامَى الْمُؤْمِنِيْنَ
“Hakika peponi kuna nyumba iitwayo nyumba ya furaha hakuna atakae iingia ila aliye wafurahisha mayatima wa waumini.”5
NYONGEZA ZA HUZUNI
Baadhi ya nyongeza za huzuni zinapendekezwa sana; zinaweza kuwa njia za kuelekea kwenye ufanisi na amani. Kutubia kikwelikweli na kujuta ni moja katika nyongeza hizo.
Imam ‘Ali (a.s.) amenukuliwa akisema:
سُرُوْرُ الْمُؤْمِنِ بِطَاعَةِ رَبِّهِ وَ حُزْنُهُ عَلَى ذَنْبِهِ
“Furaha ya mu’umini ni kwa kumtii Mola wake na huzuni yake ni kwa sababu ya madhambi yake.”6
Kwa kweli kujuta ni sharti la kimsingi miongoni mwa masharti sita ya Istighfar (ya kuomba msamaha) yaliyoelezwa na Imam ‘Ali (a.s.) katika Nahjul Balagha Imam (a.s.) anasema:
أَوَّلُهَا النَّدَمُ عَلَى مَا مَضَى
“Sharti la kwanza [la Istighfar] ni kujutia (makosa) yaliyopita”.”
Nayo Qur’an Tukufu (3:135) inasema:
وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنْفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَنْ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَىٰ مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ
“Na wale ambao wanapofanya jambo la aibu au wakazidhulumu nafsi zao humkumbuka Mwenyezi Mungu na wakaomba msamaha kwa madhambi yao na ni nani anayesamehe madhambi isipokuwa Mwenyezi Mungu.?”
Maula Faidh Kāshāni katika tafsiri yake iitwayo ‘al-Sāfi’ kuhusiana na aya hii ameelezea kisa kifuatacho:-
[kwa kukifupisha tutanukuu nukta muhimu pekee.]
Siku moja katika zama za Mtume (s.a.w.w.) kijana kwa jina la Bahlul alimjia Mtume (s.a.w.w.) akiwa analia. Mtume (s.a.w.w.) alipomuuliza sababu yakulia, alimjibu kwamba amefanya madhambi mengi makubwa ambayo baadhi tuu yanatosha kuwa sababu ya kutupwa kwake motoni. Kisha Mtume (s.a.w.w.) alimuuliza maswali kadhaa ambayo aliyajibu. Mazungumzo yalipofikia kilele Mtume (s.a.w.w.) alimuuliza,. “Jee kuna mwengine mbali na aliye Mkubwa awezae kusamehe madhambi makubwa?” Kijana alijibu, “ Naapa kwa Allah hakuna mwengine” kisha Mtume (s.a.w.w.) alimwambia amfahamishe moja ya madhambi yake hayo.
Na kijana alimpa kisa chake kama ifuatavyo: “Nilikuwa nikichimba makaburi kwa miaka saba. Na nilikuwa nikimfukua aliyezikwa na kuchukua alichonacho. Siku moja mwanamke aliyetokana na Ansaar alifariki, na baada ya kuzikwa, watu waliondoka wakiwemo familia yake. Usiku ulipofika nilikwenda kwenye kaburi lake nililifukua mwili wake nikautoa nje. Kisha niliuvua nguo na kuuacha uchi nje ya kaburi na kuondoka. Ghafla shetani alinijia kwenye akili na akaanza kunishawishi kuhusu (mwili huu). Na hapo niliamua kurudi nyuma na kwa kushindwa kuidhibiti nafsi yangu, nilitenda kitendo kibaya na maiti hiyo. Kisha niliondoka na kuiwacha kwenye hali hiyo ghafla nilisikia sauti iliyotoka nyuma yangu iliyosema,
“Adhabu ikushukie ewe kijana kutoka kwa Hakimu wa Siku ya Kiyama, Siku ambayo tutasimama mbele yake bila ya nguo kama ulivyoniacha miongoni mwa wafu, ukanitoa kwenye kaburi langu ukanivua sanda yangu na ukaniacha nikiwa sina tohara; Adhabu ikushukie.”
Kijana alipomaliza kuelezea kisa chake hiki, alisema, “kutokana na haya niliyoyafanya, sitaraji kupata harufu ya peponi kamwe”. Baada ya kusikiliza haya yote, Mtume (s.a.w.w.) alimwambia kuwa mbali na mimi ewe muovu; nakhofia nisiunguzwe na moto wako; kwa kuwa ukaribu mno na moto.
Kijana aliposikia hivyo, aliondoka alipokuwepo Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) na akaelekea mjini, ambako alinunua vyakula na kuelekea mlimani. Alipofika huko alifunga mikono yake kwenye shingo na akaanza kuomba dua, kulia, kuomba msamaha na kutubu kwa muda wa siku arobaini, mchana na usiku. Inasemekana ya kwamba wanyama walikuwa karibu naye pia, walilia kwa ajili yake baada ya siku arobaini kukamilika aliinua mikono juu na akaomba huku analia na kusema, “Ewe Allah umeamua kuchukua hatua gani kuhusu matarajio yangu? Ikiwa umeyakubali maombi yangu na ukayasamehe makosa yangu nakuomba umjulishe Mtume (s.a.w.w.) jambo hilo. Na ikiwa haujayakubali, basi nakuomba uniteremshie moto unichome, au adhabu ya hapa duniani, ili niepukane na kudhalilika Siku ya Kiyama.”
Na hii ndiyo sababu ya kushuka aya iliyopita-(3:135/6)
Baada ya kushuka aya hii, Mtume (s.a.w.w.) alikwenda kwa yule kijana na akamkuta anendelea kulia.
(Kisa chenyewe ni kirefu cha kuhuzunisha lakini tumejaribu kukifupisha). Na hapo Mtume (s.a.w.w.) alimkaribia na kumwambia, “Nakupa habari njema (kutoka kwa Allah (s.w.t.)) kwamba wewe ni mtumwa wa Allah uliyeachwa huru kutoka kwenye moto.”7
•    1. ‘Allāma Tabātabā’i, al-Mizān fi Tafsiri’l Qur’an, j. 7, uk. 134.
•    2. Mawlā Sayyid Radi al-Din bin Tāwūs, j.1, uk. 364.
•    3. Imesimuliwa na Imamu Khumayni katika kitabu chake cha hadithi 40.
•    4. Muhammadi al-Rayy Shahri, Mizān al-Hikma, j. 2, uk. 1219, tr. 8465.
•    5. Ibid, j. 2, uk. 1291, tr. 8460.
•    6. Ibid, j.2, uk. 129 tr. 8455.
•    7. Mawlā Fayd Kāshāni, Tafsir al-Sāfi, j. 1, uk. 382 – 384.

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini