Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

HESHIMA YA RAMADHANI

0 Voti 00.0 / 5

HESHIMA YA RAMADHANI

"Mwezi wa Ramadhani ni ambao imeteremshwa ndani yake Qur'ani kuwa mwongozo kwa watu..." (Qur'ani: 2:185)
Waislamu kote ulimwenguni hufunga mwezi ambao ni mwema kuliko miezi yote, ulio na masiku bora kuliko masiku yote, wenye masaa ya baraka kuliko masaa yote na amali zifanyikazo katika mwezi huo ni makbuli kuliko baki ya maombi. Nao ni mwezi wa Ramadhani.
Mwezi huu wa Ramadhani ambao ni mwezi wa tisa wa miezi wa Kiislamu, ni mwezi wa pekee wa aina yake kwa utukufu. Ni mwezi wa kusameheana, kuombeana heri na hata kufanya ibada kwa wingi na kwa usahali kabisa.
Mwezi huu una matukio mbali mbali ya kihistoria ambayo hayatasahaulika, na ambayo vile vile hupambanua wazi utukufu wake.
Imam Ja'far As-sadiq (a.s.) alisema kutoka kwa Babuye, (Mtume s.a.w.) "Taurati ilishuka na kumfikia Nabii Musa (a.s.) tarehe 6 Ramadhani, nayo Injili iIiteremshiwa Nabii Isa (a.s.) tarehe 12 za Ramadhani, kadhalika Zaburi ya Nabii Daud (a.s.) iliteremshwa mnamo tarehe 18 za Ramadhani, vile vile Qur'ani Takatifu iliteremka katika usiku wa Laylatul Qadri ambao kwa kawaida huwa katika mwezi huu wa Ramadhani."
Bila shaka hiyo ni heshima kuu kabisa. Na umejionea mwenyewe, hakuna kitabu kati ya vitabu vitukufu vinne kutoka kwa Mungu kilichoshuka ila kilishuka mwezi huu wa Ramadhani, na hayo yote ni kuonyesha utukufu wa mwezi huu. Kwa hivyo lazima vitendo vyetu katika mwezi huu viwe vitukufu kama mwezi wenyewe ulivyo.
Na katika Historia, tunasimuliwa baadhi ya matukio ya mwezi huu huu wa Ramadhani, kwa mfano:
1. Imam Hasan bin Ali bin Abi Talib (a.s.) mwanawe Sayyidna Ali (a.s.) wa kwanza, na Mjukuu wa Mtume (s.a.w.) alizaliwa mwezi huu wa Ramadhani tarehe 15 mwaka wa 3 wa tangu Mtume kugura toka Makkah kuja Madina. Mtume mwenyewe ndiyo aliyemfanyia Akiki kwa kumchinjia mbuzi alipotimiza siku 7. Sayyidna Hasan (a.s.), kama ilivyokuja katika Historia, alimfanana sana Babuye, Mtume (s.a.w.) sehemu ya juu. Naye Mtume (s.a.w.) alimnbashiria kuwa "Bwana wa vijana wa peponi".
2. Vita vya Badr vinavyojulikana zaidi (vita vikuu vya Badr, au Ghazwatul Badr) vilitukia siku ya Ijumaa mwezi wa Ramadhani tarehe 17 mwaka wa 624 A.D. Vita hivi ndivyo vilivyopambanua baina ya wakweli na waongo. Mushirikina (waabudu masanamu) waliharibikiwa sana na Waislamu ndio walioibuka na ushindi.
3. Katika mwezi huu huu, Mtume (s.a.w.) aliirudisha Makkah chini ya himaya ya Kiislamu tarehe 10 mwaka wa 630 A.D. Baada ya kuiteka Makkah, dini ya Islamu ilizidi mno nguvu na makafiri kuharibikiwa.
4. Imam, Sayyidna Ali bin Abi Talib (a.s.), bin Ami yake Mtume (s.a.w.) aliyezaliwa katika Kaaba, alipigwa upanga na adui wa Uislamu, Abdu Rahmani bin Muljim tarehe 19 ya mwezi huu wa Ramadhani mwaka wa 40 Hijria.
Alipigwa upanga msikitini huko Kufa, Iraq alipokuwa amekwenda kusali sala ya Alfajiri, na alifariki siku ya tatu yake, yaani tarehe 21 Ramadhani.
Sayyidna Ali (a.s.), Simba wa Mungu alishirikiana sana na Mtume (s.a.w.) na kuhudhuria vita vyote pasina kukimbia na ndiye aliyebaki kitandani cha Mtume (s.a.w.) alipokuwa akihamia Madina.

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini