Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

UHURU WA KIJAMII WA MWANAMKE

0 Voti 00.0 / 5

UHURU WA KIJAMII WA MWANAMKE
UHURU WA KUJICHAGULIA MAJALIWA YAKE
Siku moja msichana aliyeonekana kuwa na wasi wasi na kutatizika alikuja kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na kusema: “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Baba yangu amenifanyia dhulma kubwa.”
“Amekufanyia nini?”
“Ana mpwa wake na amenioza kwake bila idhini yangu.”
“Kama ni hivyo, kubaliana na alichofanya na kuwa mke wa binamu yako.”
“Simpendi binamu yangu. Vipi naweza kuwa mke wa mtu nisiyempenda?”
“Basi hakuna kilichoharibika. Kama humpendi chagua mtu mwingine unayempenda.”
“Lakini pia, ninampenda sana. Sipendi mtu mwingine. Sitakuwa mke wa mtu mwingine. Lakini kwa sababu baba yangu aliniozesha bila idhini yangu, nilikuja kwa makusudi kuzungumza na wewe. Nilitaka useme hayo uliyoyasema. Nilitaka wanawake wote wajue kuwa akina baba hawana haki tena ya kuamua watakavyo na kuwaozesha binti zao kwa yeyote ambaye wao akina baba wanayempenda.”
Kisa hiki kimesimuliwa na fakihi mashuhuri katika vitabu: Masalik (cha Shahid Thani), na Jawahirul Kalam. Katika kipindi cha kabla ya Uislamu, Waarabu, kama watu wengine wote wa zama hizo, walifikiri kuwa walikuwa na mamlaka kamili juu ya binti zao, dada zao na wakati fulani hata mama zao.
Hawakuitambua haki ya wanawake ya kujichagulia waume zao, mtu pekee aliyekuwa na haki ya kuchagua mume wa muolewaji alikuwa ni baba au kaka, na kama hawa hawapo basi baba wadogo na baba wakubwa. Ilikuwa inafikia hatua kuwa akina baba walichagua mume wa binti yao ambaye bado hata hajazaliwa. Mwanaume aliingia mkataba na mwanaume mwingine kuwa akizaa mtoto wa kike, basi akikua atakuwa mke wa huyu mwanaume wa pili.
NDOA KABLA YA KUZALIWA.
Siku moja Mtume alipokuwa katika Hija yake ya mwisho, akiwa juu ya farasi na akiwa na bakora mkononi mwake alifuatwa na mtu mmoja, mtu huyo akasema:
“Nina malalamiko”
“Ndiyo, sema kuna nini?”
“Miaka kadhaa huko nyuma, katika kipindi cha kabla ya Uislamu Tariq bin Murqa’a na mimi tulishiriki katika vita. Wakati wa mapigano alikuja kutaka mkuki na akapiga kelele; “Je, kuna yeyote ambaye atanipa mkuki na achukue zawadi?” Nilimwendea na kumuuliza ni zawadi gani angetoa.
Akasema angenipa binti yake wa kwanza atakayemzaa. Toka kipindi hicho miaka mingi imepita. Hivi karibuni, baada ya kuulizia, niligundua kuwa ana binti aliyekua katika nyumba yake. Nilimwendea na kumkumbusha juu ya ahadi. Lakini alirudi nyuma na kutaka mahari mapya. Sasa nimekuja kuulizia ili kuona kama mimi ni mwenye haki au yeye ndiye mwenye haki.?”
“Huyo msichana ana umri gani?”
“Msichana ameshakua. Mvi zinaonekana kichwani mwake.”
“Kama ukiniuliza mimi, nyinyi wote hamko na haki. Endeleeni na shughuli zenu na mwacheni huyu msichana kivyake.”
Mwanaume huyu alishangazwa na jibu hili na alimtazama Mtume mara kadhaa. Alishangaa hii ni aina gani ya fatwa. Hata kama angelipa mahari mpya na baba wa binti angemuozesha kwake kwa hiari, bado ndoa hiyo isingekuwa halali.
Mtume alitazama kushangaa kwa mwanaume huyo na akasema: “Usiwe na wasi wasi. Ukifanya mambo kama nilivyokwambia, basi wewe na rafiki yako Tariq, hamtakuwa mnafanya makosa.”
KUBADILISHANA MABINTI
Katika kipindi cha kabla ya Uislamu, Uarabuni kulikuwa na aina ya ndoa iliyokuwa ikipendwa ikijulikana kama ndoa ya Shighar (kubadilishana mabinti) ambayo ilikuwa ni dhihirisho la mamlaka yasiyo na kikomo ya akina baba juu ya binti zao. Mwanaume alikuwa akimuoza binti yake kwa mwanaume mwingine kwa matarajio ya yeye pia kupewa binti wa huyo mwanaume kama mke. Katika ndoa za aina hii, hakuna mke yeyote katika hawa wawili aliyepata mahari. Uislamu ulipiga marufuku ndoa za aina hii. Inafaa kuzingatiwa kuwa Mtume (s.a.w.w.) alimpa uhuru kamili binti yake Fatimah Zahra (a.s) katika kuchagua mume.
Aliwaoza pia binti zake wengine wengi, lakini hakuwanyima uhuru wao. Imam Ali bin Abi Talib (a.s) alimwendea Mtume (s.a.w.w) na kueleza nia yake ya kumposa Fatima (a.s), Mtume alisema wanaume wengi walimwendea Mtume, na yeye akafikisha ujumbe kwa Fatimah, lakini aligeuza uso wake pembeni, kama ishara ya kukataa. Mtume alimhakikishia Ali kuwa angefikisha ujumbe wake pia.
Mtume alikwenda kwa Fatimah na kumweleza binti yake mpendwa alichotaka Ali. Safari hii hakugeuza uso wake, lakini alinyamaza kimya na hivyo alielezea ridhaa yake. Mtume alipotoka nje, alikuwa na furaha, akasema, “Mungu ni Mkubwa!”
HARAKATI ZA KIISLAMU JUU YA HAKI ZA WANAWAKE
Uislamu umewafanyia wanawake mambo makubwa. Sio tu kwamba ulikomesha udhibiti usio na mipaka wa akina baba, lakini pia uliwapa wanawake uhuru, haiba na uhuru wa kufikiri na kutoa maoni.
Uislamu kirasmi kabisa ulizitambua haki zake za asili. Hata hivyo, kuna tofauti mbili za msingi kati ya hatua zilizochukuliwa na Uislamu na kile kinachotokea katika nchi za Magharibi na zinazofuatwa na wengine.
Tofauti ya kwanza inahusiana na saikolojia ya mwanaume na mwanamke. Uislamu umefanya na kufunua maajabu katika hili. Tutalijadili hili baadaye katika sura zinazofuatia.
Tofauti ya pili ni kuwa, japo Uislamu uliwafanya wanawake wazijue haki zao na ukawapa utambulisho, haiba na uhuru, haukuwachochea kuasi na kuwafanyia uovu wanaume zao.
Harakati za Kiislamu, za ukombozi wa wanawake zilikuwa nyeupe. Hazikuwa nyeusi wala nyekundu, hazikuwa bluu wala urujuani. Hazikukomesha heshima ya mabinti waliyokuwa nayo kwa baba zao wala ya wake kwa waume zao. Hazikuvuruga msingi wa maisha ya familia na hazikuwafanya wanawake wayatilie mashaka majukumu yao kwa baba zao na waume zao. Hazikutoa mwanga kwa wanaume ambao hawajaoa ambao mara zote huwa wanatafuta mwanya wa kuwalaghai wanawake.
Haukuwapokonya wanawake kutoka kwa waume zao na mabinti kutoka kwa wazazi wao na kuwakabidhi fisi wa ngono na wenye mivuto ya kilaghai ya pesa. Harakati za Kiislamu hazikufanya yale yaliyosababisha makelele na vilio katika mabahari kiasi cha mfumo wa familia kuvunjika vipande vipande. Huko ulinzi wa akina baba umetoweka.
Hakuna anayejua cha kufanya juu ya ufisadi na uchafu wa maadili uliokomaa na kuenea, juu ya uuaji wa watoto wachanga na utoaji wa mimba, juu ya asilimia 40 ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa na juu ya wale watoto wachanga ambao baba zao hawajulikani na ambao mama zao hawataki kuhusishwa na lolote juu ya watoto hao, kwa sababu hawakuzaliwa ndani ya ndoa.
Akina mama wa watoto hao wanachokifanya ni kuwakabidhi watoto hao katika taasisi au mashirika ya kijamii na kamwe hawarudi tena kuwaulizia watoto wao.
Hapana shaka kwamba katika nchi yetu tunahitaji harakati za ukombozi wa wanawake, lakini tunazozihitaji ni harakati safi za Kiislamu na sio harakati za muundo wa Ulaya wenye madoa meusi. Tunataka harakati ambazo wavulana wenye ashiki watakuwa na nafasi ndogo na ambazo zinatakiwa zitokane na mafundisho bora ya Uislamu na yawe yamejengwa juu ya uelewa wa ndani na wa kimantiki wa jamii ya Kiislamu.
RUHUSA YA BABA
Suala linalotakiwa kuchunguzwa kutokana na mamlaka waliyonayo akina baba juu ya binti zao, ni iwapo idhini ya baba ni ya lazima kwa ndoa ya kwanza ya binti yake.
Kwa mtazamo wa Uislamu baadhi ya mambo hayana ubishi.
Mvulana na msichana wote wana uhuru wa kiuchumi. Kila mtu mzima mwenye akili timamu anapaswa kuwa na mamlaka ya mali zake ikiwa anao uwezo wa kuzidhibiti. Baba, mama, mume au kaka hawana mamlaka ya usimamizi au uingiliaji kati katika hili.
Nukta nyingine ambayo haina ubishi ni juu ya ndoa. Watu wazima na wavulana waliokwishakua wana uhuru kamili juu ya jambo hili na hakuna mtu mwingine mwenye haki ya kuingilia. Hali hiyo iko hivi hivi pia kwa mwanamke ambaye amewahi kuolewa lakini sasa hana mume. Lakini kuna tofauti kidogo juu ya mwali ambaye anataka kuolewa kwa mara ya kwanza.
Hapana shaka kuwa baba hawezi kumlazimisha binti yake kuolewa na mtu ambaye yeye binti hajamridhia. Tayari tunajua Mtume alichomwambia yule binti ambaye baba yake alikuwa amemwozehsa bila idhini ya huyo binti. Mtume alisema ikiwa hakuridhika, anaweza kuolewa na mtu mwingine. Lakini kuna tofauti ya maoni ya wanazuoni juu ya iwapo binti anaweza kufunga ndoa bila idhini ya baba yake au iwapo idhini ya baba ni ya lazima.
Kuna nukta moja ambayo haina ubishi kabisa. Ikiwa baba atakataa kutoa idhini bila sababu ya maana, anapoteza haki yake. Mafakihi wamekubaliana kuwa katika hali hiyo binti ana uhuru wa kuolewa na yeyote anayempenda.
Lakini vinginevyo, ni kama tulivyosema, kuwa mafakihi wanatofautiana juu ya nukta hii, iwapo uthabiti wa ndoa ya binti inategemea idhini ya baba au la. Wanavyuoni wengi, hasa wa siku hizi wana maoni kuwa idhini sio lazima. Lakini kuna baadhi ambao wana maoni kuwa idhini ni ya lazima.
Kwa sababu nukta hii inabishaniwa haiwezi kujadiliwa kwa mtazamo wa Kiislamu lakini inaweza kujadiliwa kwa mtazamo wa kijamii.

MWISHOA

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini