Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

MUHAMMAD MTUME WA ALLAH 1

1 Voti 01.0 / 5

MUHAMMAD MTUME WA ALLAH 1
KIDOKEZO KIFUPI CHA WASIFA
KUZALIWA MPAKA KUANZA KWA WAHYI
Muhammad al-Mustafa, Mtume wa mwisho wa Allah, alizaliwa Makkah, Arabia mnamo mwezi 17 Rabi al-Awaal, mwaka wa kwanza wa tembo (Amul Fiil) 570 A.D.
Mtume Muhammad (s.a.w.) alizaliwa katika ukoo wa Bani Hashim, wa kabila la Quraishi, ambao walikuwa ndio walioheshimiwa sana katika familia za Kiarabu. Bani Hashim walikuwa ni kizazi cha Ismail, mwana wa Nabii Ibrahim.
Babu yake Mtukufu Mtume, Mzee Abdul Muttalib alikuwa ndiye Mkuu wa Bani Hashim na vile vile alikuwa ndio mlezi wa al- Kaaba. Baba yake yeye Mtume, alikuwa anaitwa Abdullah na mama yake aliitwa Amina. Baba yake alifariki miezi michache kabla ya kuzaliwa kwake. Akiwa na umri wa miaka sita, Mtume akampoteza mama yake pia na yeye akawekwa chini ya uangalizi wa babu yake, Abdul Muttalib. Lakini babu yake naye akafariki baada ya miaka minne; na safari hii, ami yake Mtume, Abu Talib alichukua dhima juu yake na akawa mlezi wake, akimchukua kuishi naye nyumbani kwake mwenyewe. Hivyo Mtukufu Mtume (s.a.w.) kwa kiasi kikubwa alikulia nyumbani kwa ami yake na hata kabla ya kufikia umri wa balehe alikuwa akifuatana na ami yake kwenye safari za kibiashara kwa misafara.
Mtukufu Mtume hakuenda shule yoyote, hata hivyo, baada ya kufikia umri wa utu uzima alikuwa maarufu kwa hekima zake, ushauri, uaminifu na ukweli wake. Mara akawa anajulikana kama “as-sadiq al-amin” – mkweli, mwaminifu. Ami yake, Abu Talib alikuwa kila mara akisema “Hatujasikia uwongo wowote kutoka kwa Muhammad, wala kuwa na tabia mbaya au kufanya uharibifu. Kamwe hacheki ovyo ovyo wala kuzungumza wakati usiofaa.”
Kwa matokeo ya busara na uaminifu wake, Khadija bint Khuwaylid, bibi wa kikuraishi maarufu kwa utajiri wake, akamteua yeye kama meneja wa biahsara zake na akaacha jukumu la kuendesha shughuli zake za kichuuzi mikononi mwake. Mtume safari moja alikwenda Damascus na bidhaa za Khadija na kutokana na uwezo wake akatengeneza faida kubwa ya kuvutia. Haukupita muda mrefu yeye Khadija akamuomba awe mke wake naye Mtume akalikubali ombi lake hilo. Baada ya ndoa yao, akiwa na umri wa miaka ishirini na tano, Mtukufu Mtume akaanza maisha ya kuwa meneja wa mali za mke wake. Alipofikia umri wa miaka arobaini, alijipatia sifa njema ya kuheshimika iliyoenea sana kwa sababu ya busara na uaminifu wake.
Alikataa kuabudu masanamu, kama ilivyokuwa ndio desturi ya kidini ya Waarabu wa wakati huo. Mara kwa mara alifanya faragha za kiroho kwenye pango la Hira nje kidogo ya Makkah, ambamo alifanya maombi na kuzungumza kwa siri na Allah.
KUANZA KWA UJUMBE
Kwenye umri wa miaka arobaini, wakati Mtume alipokuwa kwenye faragha ya kiroho ndani ya pango la Hira, humo alipokea wahyi wa kwanza kutoka kwa Mwenyezi Mungu s.w.t. kupitia kwa Malaika Mkuu Jibril: Huu ulikuwa ndio mwanzo wa kazi ya kutangaza dini hiyo mpya. Katika muda huo zile aya tano za mwanzo za Sura ya 96 ya Qur’an Tukufu zilishushwa kwake. (Tukio hili linajulikana kama Bi’that – kusimamishwa ili kutangaza ujumbe wa Allah)
Siku ile ile aliueleza Wahyi huo kwa binamu yake, Ali Ibn Abi Talib ambaye alitangaza kuikubali kwake dini hiyo. Baada ya Mtume kurudi nyumbani na kumueleza mke wake juu ya Wahyi huo, kadhalika na yeye aliukubali Uislamu. Mara tu, baadaye, Zayd bin Haritha (mtumwa mwaminifu ambaye alimfanya kama mwanawe mwenyewe) vile vile akasilimu na kuwa naye Muislamu.
Mara ya kwaza kabisa wakati Mtukufu Mtume alipokuwa akiwalingania watu kuukubali ujumbe wa Uislamu, alikumbana na upinzai wa kuhuzunisha na mkali sana. Kwa sababu ya umuhimu kwa hiyo, alilazimika kutangaza ujumbe wake kuanzia hapo kwa siri kwa muda wa miaka mitatu hadi yeye alipoagizwa tena na Allah (s.w.t.) kuwaita ndugu zake wa karibu kabisa ili kuukubali ujumbe wake. Aliandaa karamu ya ndugu na akawaalika takriban watu arobaini wa ukoo wake.
Katika mkusanyiko huo, Muhammad aliwauliza kama waliwahi kamwe kumuona akidanganya au kusema uongo? Majibu ya jumla yakawa: “Hatujakuona wewe ukisema uwongo.” Kisha akauliza: “Kama ingekuwa niwaambie kwamba maadui zenu wamejikusanya nyuma ya vile vilima vya mchanga, tayari kwa kuwashambulia, je mtaniamini?” Wao wakajibu, ‘Ndio.’ Halafu akasema:
“Simjui mtu yeyote katika Bara Arabu ambaye anaweza kuwapa ndugu zake kitu bora zaidi hasa kuliko ninavyofanya sasa. Mimi ninakupeni furaha ya maisha yote; ya dunia hii na yale ya kesho Akhera. Mwenyezi Mungu ameniagiza mimi kuwaiteni ninyi kwake. Ni nani kwa hiyo, miongoni mwenu atakayenisaidia katika hili, ili awe ni ndugu yangu, mrithi wangu na khalifa wangu?
Lakini wito huu ulikuwa pia haukuzaa matunda na hakuna aliyeutilia maanani isipokuwa Ali Ibn Abi Talib ambaye kwa hali yoyote ile yeye alikuwa ameikubali dini hiyo. Kwa mujibu wa nyaraka za kumbukumbu za kihistoria na mashairi yaliyotungwa na Abu Talib ambayo yanapatikana hadi sasa, Abu Talib pia aliukubali Uislam; hata hivyo, kwa kuwa alikuwa ndiye mlinzi pekee wa Mtume aliificha imani yake kwa watu ili kuhifadhi ile nguvu yake ya nje aliyokuwa nayo miongoni mwa watu wa Makkah.
Baada ya kipindi hiki, kwa mujibu wa maelekezo ya ki-mungu, Mtume akaanza kulingania ujumbe wake kwa uwazi kabisa. Kwa kuanza kwa kutangazwa kwa wazi kwa ujumbe wake, watu wa Makkah walikuja juu kwa nguvu sana kwa sababu ya ule ujumbe wenyewe wa uislamu – wa kuabudu Mungu mmoja na usawa miongoni mwa waumini bila ya kujali tofauti yoyote ya utaifa, rangi au utajiri – walihofia kabisa dhidi ya hali zao kama zilivyokuwa. Maumivu makali sana na mateso yalifanywa juu ya Mtume na wale walioingia kwenye dini hiyo.
Kwa mfano, Bilal, mtumwa wa kihabeshi ambaye alikuwa ameukubali Uislam, alifungwa kwenye mchanga unaochoma wa jangwa la Arabia na jiwe kubwa sana likawekwa juu ya kifua chake pamoja na maonyo kutoka kwa miliki wake Umayya kwamba angeendelea kubakia katika hali hiyo mpaka atakapoukana Uislam. Lakini sauti pekee ambayo ilisikika ikitoka kwenye midomo ya Bilal ilikuwa ni “Ahad! Ahad! Ahad!” (Mungu Mmoja! Mungu Mmoja!
Makuraishi waliwafanyia waumini ukatili sana kiasi kwamba kikundi cha takriban Waislam 100, chini ya uongozi wa Ja’far bin Abi Talib waliziacha nyumba zao na mali zao, na wakahamia Abyssinia (Ethiopia ya sasa). Waliambiwa na Mtume kwamba watamkuta huyo mfalme wa Abyssinia kuwa ni mtawala mwadilifu. Wakiwa na nia ya kukwamisha kule kuenea kwa Uislamu, Makuraishi waliwafuata mpaka huko Abyssinia wakitafuta kurejeshwa kwao nyumbani ili waje kuhukumiwa kama wahalifu. Lakini Ja’far, kwa ufasaha sana aliliwasilisha suala la Waislam kwa mfalme wa Abyssinia na maombi ya Makuraishi yakakataliwa. Ja’far akasema:
“Ewe Mfalme! Sisi tulikuwa tumezama kwenye kina cha ujahiliya na ushenzi; tuliabudu masanamu, tuliishi maisha machafu tulikula mizoga na tulizungumza lugha ya machukizo; tuliipuuza kila hisia ya ubinadamu na shughuli zote za ukarimu na ujirani; tulikuwa hatuna wala hatujui sheria yoyote bali ile ya wenye nguvu —wakati Mwenyezi Mungu alipotunyanyulia mtu miongoni mwetu, ambaye uzao wake mtukufu, ukweli wake, uaminifu na usafi wake, vyote tunavitambua; na ametuita kwenye Upweke wa Allah (Tawheed) na akatufundisha tusimshirikishe Yeye na kitu chochote; ametukataza tusiabudu masanamu; alituagiza sisi tuseme kweli, kuwa waaminifu kwenye amana zetu, kuwa wenye huruma na kuwajali haki za majirani; ametukataza tusiwaongelee wanawake kwa uovu au kula mali ya mayatima; alituagiza kuepukana na tabia mbaya na kujizuia na maovu; tusali, tutoe zakat na kufunga.
Tumemwamini yeye, tumeyakubali mafundisho yake na amri zake za kumuabudu Mungu na tusishirikishe chochote pamoja Naye.
Kwa sababu hii tu, watu wetu wamechachamaa dhidi yetu, wametutesa ili tuachane na ibada ya Mungu na turudi kwenye kuabudu masanamu ya mawe na magogo ya miti na machukizo mengineyo. Walitutesa na kutuumiza, mpaka tukawa tumekosa usalama tukiwa miongoni mwao, tumekuja kwenye nchi yako nasi tunategemea kwamba utatulinda kutokana na uonevu wao.”
Nyuma, huko Makkah, vikwazo vya kiuchumi na kijamii viliwekwa dhidi ya Mtume na familia yake. Kwa hiyo, Mtume na ami yake, Abu Talib, pamoja a ndugu zao kutoka ukoo wa Bani Hashim walikimbilia kujihifadhi mafichoni kwa muda wa miaka mitatu huko kwenye “korongo la njia ya mlimani” – lililoitwa ‘Shi’b Abu Talib’ ngome moja iliyokuwa kwenye moja ya mabonde ya Makkah. Hakuna aliyefanya uhusiano au kushughulika nao na wala wao hawakuthubutu kuiondoka hiyo sehemu yao ya hifadhi.
Ingawa hapo mwanzoni waabudu masanamu wa Makkah walifikiria kuwafanyia aina zote za mashinikizo na mateso kama vile kuwachapa na kuwapiga, kuwatukana, dhihaka na kashfa kwa Mtume, mara kwa mara wao walionyesha upole pia na ushari kwake ili kuweza kumfanya aiwache kazi ile ya ujumbe wake. Waliweza kumuahidi viwango vikubwa vya fedha au uongozi na utawala wa kikabila. Lakini kwa Mtume, ahadi zao za vitisho vyao viliishia tu katika uongezekaji wa nia na dhamira yake ya kuitekeleza kazi ya ujumbe wake. Wakati mmoja, wao walipokuja kwa Mtume wakimuahidi utajiri a mamlaka, Mtume, akitumia lugha ya kiistiari aliwaambia, kwamba kama ingekuwa waliweke jua kwenye kiganja cha mkono wake wa kulia na mwezi kwenye kiganja cha mkono wa kushoto, yeye asingegeuka nyuma katika kumtii Mungu Mmoja ama kujiepusha na kufanya kazi ya ujumbe wake.

ITAENDELEA KATIKA MAKALA IJAYO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini