Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

HAJA YA DINI 2

0 Voti 00.0 / 5

HAJA YA DINI 2

MUENDELEZO WA MAKALA NAMBA MOJA

5) HOJA IJULIKANAYO KAMA "HOJA YA PASCAL"

Hadhrat Amiirul Mu'miniin Ali bin Abi Talib alisema:
Wanajimu na waganga husema kuwa wafu hawatafufuliwa kamwe, "Nikasema: Haya shikilieni maoni yenu hayo. Kama oni lenu litakuwa sahihi, sitapata dhara lolote (kutokana na imani yangu, ya kuiammi sika ya Hukumu); lakini iwapo imani yangu itakuwa sahihi basi mtakuwa wakosefu (katika siku hiyo kwa kutoiamini siku ya Hukumu)".

Allama Abu Hamid Al Ghazali (Aliyefariki mnamo mwaka 1111 Masihiya) aliandika katika kitabu chake kiitwacho "Mizanul Aamal" kuwa "Ali (Mwenyezi Mungu amteremshie baraka zake) alimwambia mtu mmoja aliyekuwa akibishana naye sana kuhusu Akhera akisema: Kama ukweli ni huo unaoufikiria (kuwa hakuna maisha ya Akhera); basi ninyi wote mtaokoka; lakini iwapo ukweli ni kama hivi nilivyokwisha kueleza (kuwa kuna maisha ya Baadaye), basi ninyi mtalaaniwa na mimi nitaokolewa." Huo ndio ukweli uliopo. Thibitisho tuzipatazo sisi wenyewe tuvionapo viumbe vilivyomo humu duniani, zaunga mkono imani ya kuwepo Mwenyezi Mungu Muumba, na kuwepo kwa siku ya Hukumu.

Kisha Mwanachuoni huyo, Bwana Al-Ghazali alieleza kuwa, Hadhrat Ali [a] hakuitoa hoja hii ili kuficha mdhihiriko wa kuwepo kwa maisha ya Akhera, ila aliitoa kwa kutaka kuwahakikishia watu jambo hili kwa maelelezo ya kihoja.

Miaka elfu moja, baada ya Hadhrat Ali bin Abi Talib [a] alitokea mtaalamu wa hesabu maarufu sana Bwana Pascal ambaye alifariki mnamo mwaka 1662 Masihiya; pamoja na "Parido Pascal" (Hoja ya Pascal) yake maarufu, ambayo allitumia ili kulihakikishia kundi la watu wa aina hiyo hiyo, jambo hilo hilo.

Hoja yake hiyo, yaweza kuelezwa kwa kifupi zaidi kwa maneno yafuatayo:
"Kama unaamini kuwepo maisha ya Akhera, utapata kila kitu kama kweli maisha hayo yapo kweli, na hutapata hasara yoyote kama maisha hayo hayapo. Hivyo basi ni afadhali kuyakinisha kuwa, hakika siku hiyo ipo." (Habari hizi zinatoka katika UK. 439 wa kitabu kiitwacho "Pascal", kilichoandikwa na Bensees na kutayarishwa Bwana Y. Brunchirey huko Paris - Ufaransa mnamo mwaka 1912 Masihiya).

Je huu ni ulinganifu tu? Au Pascal alipata wazo la (Pari) imani yake kutokana na Uislamu?

Bwana Asin Palalcios anaamini kuwa Bwana Pascal alisoma hoja hizi katika kitabu kiitwacho "Ihya-ul-Uluum" cha Mwanachuoni Al-Ghazali.

Lakini, Bwana Al-Ghazali mwenyewe anaeleza katika kitabu hicho Mizanul-Aamal tulicho kitaja hapo juu kuwa, Hadhrat Ali bin Abi Talib [a] ndiye asili ya hoja hii.

Hivyo basi, inatubidi tuziweke sifa hizi pale zipasikapo kuwapo na kukubali kuwa Bwana Pascal (ingawa yeye binafsi hakutueleza kazipata habari hizi kutoka kwa Hadhrat Ali bin Abi Talib [a].

6) SIFA ZA DINI

Mpaka sasa nimeeleza umuhimu wa dini kwa ujumla.
Sasa hebu ngoja nizitaje sifa za lazima kwa dini kuwa nazo, ili itimize mahitaji ya dini niliyoyataja hapo juu.
1) KWANZA KABISA DINI NI LAZIMA IPATANE NA AKILI NA UDADISI WA MTU.

Hakika zipo dini zenye kuwataka wafuasi wake waamini kwanza kisha ndipo waelewe. Kusema kweli dini kama hizi huzirudisha nyuma fikara za mwanaadamu na ni haki ziitwe (na kwa hakika zinaitwa) dini zisizopatana na fikara za Mwanaadamu.

Uislamu kama unavyofafanuliwa na imani ya madhehebu ya Shia Ithna-sheria, hutoa nafasi ya mbele zaidi kwa akili za binadamu na hoja zake. "Akili" ni moja wa misingi minne ya Sheria ya Shia Ithna-Asheria. Sio hivyo tu, bali vile vile imani hii inahimiza kuwa mafundisho ya dini ni lazima yaeleweke kwa mwenye kuiamini dini hiyo.
2) NI LAZIMA DINI IFUNDISHE NA IFANYE KWA VITENDO, HEKIMA YA MWANAADAMU.

Ziko dini ambazo huwataka wafuasi wake wasujudie picha au sanamu za watu fulani fulani au wanyama fulani fulani au vitu vingine ambavyo havina uhai.

Dini kama hizi hushusha sana heshima za wafuasi wao, na ni haki zilaumiwe kwa jambo hilo. Baadi ya dini hufundisha ubora wa watu wa taifa fulani au kudharau watu wa ukoo mwingine.

Uislamu tu ndio uliokuwa na bado ni kiongozi wa usawa wa binaadamu na ambavyo, kwa mara ya kwanza katika historia ya dini, umefundisha na ukafanya kwa vitendo, udugu, usawa na haki kwa binadamu na ukaonyesha heshima ya Mwanadamu kiasi cha kuweza hata kuyashangaza macho ya watu wote.
3) DINI NI LAZIMA IWE MWONGOZO ULIO KAMILI WA KUMWENDELEZA MWANADAMU KIMWILI, KIAKILI NA KIROHO KWA UJUMLA.

Zipo baadhi ya dini ambazo hutilia mkazo zaidi katika mambo ya kiroho na kuachilia mbali mwili na akili; na zipo nyingine ambazo huzungumzia tu kuhusu maendeleo ya kimwili, au ya kiakili lakini haziyafanyi kimatendo mambo hayo.

Dini za aina hii haziwezi kuwachukua wafuasi wake mbali sana kwa sababu maendeleo yafundishwayo na dini hizo yamekwenda kombo.

Ni Uislamu tu, kama unavyofundisha na Madhehebu ya Shia Ithnaasheria, ambao humwendeleza mtu kimwili, kifikara na kiroho kwa ujumla.
4) NI LAZIMA DINI IWE NA MKUSANYIKO WA SHERIA ZIHUSUZO MAISHA YA BINAADAMU.

Dini ambazo hufundisha tu kuwa "wapende jirani yako" bila ya kuonyesha jinsi ya kufanya hivyo, ni dini zisizo na faida yo yote wakati zikaribiwapo na suala la kulifanya jambo kimatendo.
Uislamu unao mkusanyiko timamu wa sheria za maisha ya mwanaadamu ambazo humwongoza mtu sawa sawa katika maisha yake ya kifamilia, kijamii, kiuchumi, kitabia za kiutu na kiadilifu.
5) NI LAZIMA DINI IAFIKIANE NA ASILI YA MWANAADAMU.

Zipo dini zinazojaribu kuiepuka asili ya mwanaadamu. Kwa mfano, baadhi ya dini zinafundisha utawa. Wanaamua kwa matendo yao (kama si kwa maneno mengi) kuwa Mwenyezi Mungu alikosea alipoumba hamu ya tendo la mke na mume katika mwili wa mwanaadamu. Vile vile wanasahau (au wanajifanya kusahau) kuwa silika za kiasili haziwezi kuharibiwa na kuwa silika hizi zisizo za kiasili zinamwongoza mtu kwenye undanganyifu wa kisiri.

Na sijui, ni nini kingelitokea kuhusu kuwepo kwa mwanaadamu hapa duniani, iwapo watu wote wangelikuwa wafuasi wa kimatendo wa dini hiyo. Hakika watu wote wangelimalizika katika muda wa miaka kati ya arobaini na hamsini hivi.

Bila ya kusema kuwa dini kama hii haiwezi kuwaongoza watu kwenye ustawi, kwa sababu kufuatana na asili yake, dini hii ni kinyume na mdumisho wa kuwepo kwa wanadamu hapa duniani.
6) NI LAZIMA DINI ISITUMIKE KAMA ZANA MIKONONI MWA WADHALIMU, ILI KUUDHULUMU UMMA.

Dini nyingi zinalaaniwa na makafiri kwa kuwa silaha ya makabaila kwa ajili ya kuudhulumu umma unaoonewa na kuzifunika sauti za walalamikaji.

Dini kama hizi, kwa mfano zile zilizofundisha mawazo ya "Kudra". Hivyo basi, umma ulilazimishwa kuamini kuwa matendo yote mabaya, udhalimu, na uovu wa watawala ulikuwa ni Penzi la Mwenyezi Mungu; hivyo basi vitu kama hivi ni lazima vivumiliwe bila ya malalamiko yo yote.

Dini kama hizo hazina nafasi katika karne iliyoendelea kama hii yetu. Ni Uislamu peke yake, kama ulivyoelezwa na madhehebu ya Shia Ithna-asheria ambao ulisema kuwa imani kama hiyo ilikuwa upuuzi mtupu; kuwa kila mtu ana madaraka kamili ya matendo yake na kuwa madaraka yake yasihusishwe na Mwenyezi Mungu.

Itadhihirika wazi, kutokana na kanuni ya hapo juu kuwa, miongoni mwa dini nyingi sana za duniani, ni Uislamu tu (Imani ya Shia Ithna-asheria) ambao Unatimiza mashaiti haya ya lazima ya dini ya kweli, na yenye maarifa mengi.

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini