Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

TAWASSULI (SEHEMU YA NNE)

0 Voti 00.0 / 5

TAWASSULI (SEHEMU YA NNE)

MUENDELEZO WA MAKALA ILIYOPITA
MJADALA DHIDI YA WANAOKANUSHA TAWASSULI KURUHUSIWA KISHERIA
Imesemekana haiwezekani kutawasali kupitia mfu, na kitendo hiki ni kibaya kiakili kwa sababu maiti haina uwezo wa kujibu, na kuwa kutawasali kupitia yeye ni kusemesha kisichokuwepo. 1
Dai hili linapingwa na linapingana na Qur’ani tukufu. Ifuatayo ni mifano halisi kutoka ndani ya Aya za Qur’ani tukufu ambazo zinakanusha dai la kuwa maiti ni kisichokuwepo:
i) “Na humo watapata riziki zao asubuhi na jioni.”2
Kundi hili la Aya liliteremka kuzungumzia haki ya waumini, kwani lin- abainisha aina ya umuhimu watakaofanyiwa duniani na Akhera.
Na nyingine ikaweka wazi:
النَّارُ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا غُدُوًّا وَعَشِيًّا ۖ وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ أَدْخِلُوا آلَ فِرْعَوْنَ أَشَدَّ الْعَذَابِ {46}
“Ni moto wanawekewa asubuhi na jioni. Na siku kitakapotokea Kiyama waingizeni watu wa Firauni katika adhabu kali zaidi.”Ghafiru: 46.
Mwenyezi Mungu anabainisha adhabu watakayoipata wenye kuasi na makafiri katika maisha ya Barzakhi, jambo linalojulisha kuwa wao ni hai baada ya kifo na kabla ya Kiyama, kwani kusimama Kiyama kumetajwa baada ya kuwekewa moto Asubuhi na Jioni. Hivyo ikithibiti kuwa kifo si kutoweka bali ni uhai mpya, basi je, inawezekana kuwasiliana na mfu au haiwezekani? Kwa madai kuwa uhai wa Barzakhi unazuia kuwasiliana naye?
Jibu ni: Kuna Aya nyingi ndani ya Qur’ani tukufu - ukiongezea na Sunna tukufu - zinazoonyesha uwezekano wa mwanadamu aliyomo duniani kuwasiliana na mwanadamu hai aliyomo ndani ya ulimwengu wa Barzakhi. Miongoni mwa Aya hizo ni hizi zifuatazo:
Wito wa Nabii Saleh kwa kaumu yake akitaka wamwabudu Mwenyezi Mungu na akaiamuru isiudhuru muujiza wake, na baada ya kumchinja ngamia jike na kuasi amri ya Mola wao Mlezi, Mwenyezi Mungu anasema:
فَأَخَذَتْهُمُ الرَّجْفَةُ فَأَصْبَحُوا فِي دَارِهِمْ جَاثِمِينَ {78}
فَتَوَلَّىٰ عَنْهُمْ وَقَالَ يَا قَوْمِ لَقَدْ أَبْلَغْتُكُمْ رِسَالَةَ رَبِّي وَنَصَحْتُ لَكُمْ وَلَٰكِنْ لَا تُحِبُّونَ النَّاصِحِينَ {79}
“Na tetemeko likawanyakua na wakawa majumbani mwao kifudifudi wamekwishakufa.* Basi akawaacha na akasema: “Enyi kaumu yangu, bila shaka nimekufikishieni ujumbe wa Mola Wangu Mlezi na nimekunasihini lakini nyinyi hamuwapendi wenye kunasihi.”
Al- ‘Aaraf: 78-79.
Tazama jinsi Mwenyezi Mungu anavyotoa habari kwa uhakika na uyakini kuwa tetemeko liliangamiza umma wa Saleh (a.s.) na wakawa majumbani mwao kifudifudi wamekufa. Baada ya hapo anatoa habari kuwa Nabii Saleh (a.s.) aliwaacha kisha akawaambia kwa kusema:
لَقَدْ أَبْلَغْتُكُمْ رِسَالَاتِ رَبِّي وَنَصَحْتُ لَكُمْ ۖ {93}
“Bila shaka nimekufikishieni ujumbe wa Mola wangu Mlezi na nimekunasihini lakini nyinyi hamuwapendi wenye kunasihi.”Al- Aaraf: 93.
Maelezo yaliyotoka kwa Saleh (a.s.) kuiambia kaumu yake yalikuwa ni baada ya kuangamia kwao na kifo chao, kwa ushahidi wa kauli: “Na akawaacha” iliyoanza kwa (Al-Fau) yenye kuhisisha kuwa maelezo yalitoka baada tu ya kaumu kuangamia.
Nabii Shuaybu (a.s.) aliwasemeza watu wake baada ya kuangamia kwao kwa kauli ya Mwenyezi Mungu:
فَتَوَلَّىٰ عَنْهُمْ وَقَالَ يَا قَوْمِ لَقَدْ أَبْلَغْتُكُمْ رِسَالَاتِ رَبِّي وَنَصَحْتُ لَكُمْ ۖ فَكَيْفَ آسَىٰ عَلَىٰ قَوْمٍ كَافِرِينَ {93}
“Basi akawaachilia mbali na akasema: “Enyi kaumu yangu, bila shaka nimekufikishieni ujumbe wa Mola Wangu Mlezi na nimekupeni nasaha, basi vipi nihuzunike juu ya makafiri.” -Al-Aaraf: 93.
Usemi wa Shuaybu kuwaambia kaumu yake umetoka baada ya kuangamia kwao. Hili linahimiza uwezekano wa kuwasiliana nao, kwani laiti walioangamia kwa tetemeko wangelikuwa hawasikii usemi wa Shuaybu (a.s.) na Saleh (a.s.) basi nini maana ya wao wawili kuwasemeza?
Wala haisihi kufasiri kuwa ni maelezo ya kuhuzunika kwa sababu tafsiri hiyo ni kinyume na maana inayojulikana moja kwa moja, na si sahihi kwa mujibu wa misingi ya kitafsiri.
Ama baadhi ya hadithi tukufu ambazo zinaashiria uwezekano wa kuwa na mawasiliano na roho za wafu ni kama zifuatazo:
Imepokewa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kuwa alisimama kwenye Kisima cha Badri na kuwasemeza mushirikina ambao walikuwa wameuawa na miili yao ikiwa imetupwa kwenye Kisima. Kutoka kwa Anas bin Malik amesema: Sahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu walimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu usiku akisema: “Enyi watu wa kisimani, ewe Ut’batu bin Rabia, ewe Umayya bin Khalaf, ewe Abu Jahl bin Hisham...”
Akataja orodha ya waliyokuwemo kisimani. “Je, mmekuta ni kweli aliyowaahidini Mola wenu Mlezi? Kwani mimi nimekuta ni kweli aliyoniahidi Mola Wangu Mlezi.”
Waislamu wakasema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hivi unawaita watu ambao wameshakufa?” Akasema: “Nyinyi hamsikii niyasemayo kuliko wao, lakini wao hawawezi kunijibu.”3
Hakika waislamu bila kujali madhehebu yao humtolea salamu Mtume wa Mwenyezi Mungu ndani ya sala na mwishoni mwake wakisema: “Amani iwe juu yako ewe Nabii na Rehema za Mwenyezi Mungu na Baraka zake.” Na hakika Sunna hiyo ya Mtukufu Mtume imethibiti kwa ajili yake zama za uhai wake na baada ya kifo chake, hivyo mawasiliano yetu na uhusiano wetu na Nabii (s.a.w.w.) havikatiki. Salamu hii haijulishi uwezekano wa kuwasiliana na roho yake (s.a.w.w.) tu, bali zaidi ya hapo inathibitisha kwa yakini kuwa mawasiliano yapo.
Imepokewa kutoka kwake kuwa: “Atakayenizuru baada ya kifo changu na akanitolea salamu nitamrudishia salamu mara kumi na watamzuru Malaika kumi wakimtolea salamu. Na hapana yeyote atakayenisalimia ndani ya nyumba yoyote ile isipokuwa Mwenyezi Mungu hunirudishia roho yangu mpaka nami nimrudishie salamu.4
Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: “Mwenye kunizuru baada ya kufa kwangu ni kama amenizuru wakati wa uhai wangu….5
Ikithibiti kuwa inawezekana kuwasiliana na mtu aliyomo kwenye maisha ya Barzakhi, je inaruhusiwa kumwomba na kutawasali kupitia kwake ili kukidhiwa haja, au kufanya hilo ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu kwa ushahidi wa kauli yake (s.w.t.): “Hakika mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu?”6
Jibu: Hakika mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu na kwa utashi Wake na kwa ridhaa Yake hutokea mambo, isipokuwa hilo halizuii kuthibiti shufaa ya Manabii na Mawalii duniani na Akhera baada ya idhini kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kama linavyoonekana hilo pale ilipothibiti kwa Isa (a.s.) kuumba na kuhuisha wafu na kuponya wagonjwa baada ya idhini kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Na kwa kuwa mambo huenda kwa kufuata Kanuni ya ‘Sababu na Kisababishwa’ ndio maana tunamkuta Musa (a.s.) akisema:
قَالَ هِيَ عَصَايَ أَتَوَكَّأُ عَلَيْهَا وَأَهُشُّ بِهَا عَلَىٰ غَنَمِي وَلِيَ فِيهَا مَآرِبُ أُخْرَىٰ {18}
“Akasema: Hii ni fimbo yangu ninaegemea na ninaangushia majani kwa ajili wanyama wangu; tena ninaitumia kwa matumizi mengine.” Twaha: 18.
Hivyo Manabii pamoja na Utakaso wao lakini wametaka msaada kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, mpaka Mtume wa Mwenyezi Mungu akateremshiwa:
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ حَسْبُكَ اللَّهُ وَمَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ {64}
“Ewe Nabii Mwenyezi Mungu anakutosha wewe na yule aliyekufuata katika waumini.”
Al-Anfali: 64
Maana inayojulikana kutoka kwenye Aya ni Mtume kutaka msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kutoka kwa waumini kama Isa (a.s.) alivyotaka kusaidiwa na wanafunzi wake, akasema:
مَنْ أَنْصَارِي إِلَى اللَّهِ ۖ {52}
“Nani atakuwa msaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu?”Al-Imrani: 52
Na kama Musa (a.s.) alivyotaka kusaidiwa na ndugu yake Haruna (a.s.) na Mwenyezi Mungu akamjibu: “Karibuni tutautia nguvu mkono wako kwa ndugu yako.”7 na 8 Kisha tunamkuta Mwenyezi Mungu ameomba msaada kutoka kwa waja wake akasema:
إِنْ تَنْصُرُوا اللَّهَ يَنْصُرْكُمْ وَيُثَبِّتْ أَقْدَامَكُمْ {7}
“Mkimsaidia Mwenyezi Mungu atawasaidia.”Muhammad: 7.
Na akasema:
وَالَّذِينَ آمَنُوا وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا فِي سَبِيلِ اللَّهِ وَالَّذِينَ آوَوْا وَنَصَرُوا أُولَٰئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا ۚ {74}
“Na wale waliowapa mahala pa kukaa na wakainusuru hao ndio wau- mini wa kweli.”
Al-Anfali: 74.
Hivyo tukikiri kuwa kuomba msaada na kutawasali kupitia asiyekuwa Mwenyezi Mungu ni jambo linaloruhusiwa kwa sababu ni kwa idhini Yake na utashi Wake, na si kwa kujitegemea; basi ni ipi dalili ya kuomba msaa- da kupitia maiti? Ilihali kilichothibiti ni kuomba msaada zama za uhai wake kupitia Mtume (s.a.w.w.) au Walii na si wakati wa ufu wake.
Hakika Sahaba hawajakanusha kutawasali kupitia Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) zama za uhai wake na baada ya kifo chake.
KUTAWASSALI KUPITIA MANABII NA MAWALII BAADA YA VIFO VYAO
Miongoni mwa sera za waislamu ni kutawasali kupitia Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) baada ya kifo chake:
Ndani ya Musnad ya Ahmad mna: “Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi nakuomba kwa haki ya wanaokuomba na ninakuomba kwa haki ya mwendo wangu huu, kwani mimi sikutoka kwa maringo na majivuno wala kujionyesha wala kutaka kusifiwa, nimetoka kwa kuogopa ghad- habu zako na kutafuta radhi zako. Basi ninakuomba uniepushe na moto na unisamehe madhambi yangu kwani hapana anayesamehe madhambi isipokuwa Wewe.”9
Hadithi hii iko wazi mno katika maana yake na inajulisha ruhusa ya kutawasali kupitia Mawalii wao wenyewe na wala si kupitia dua zao. Na ni tamko jumuisho linalojumuisha waombaji wote kutoka kwa Adam mpaka siku ya mwombaji, bali linajumuisha Malaika pia na waumini miongoni mwa Majini. Na wala haiwezekani kuihusisha na waombaji wa siku ya leo tu, au walio hai tu, kwani hakuna dalili inayoelekeza Hadithi kwenye maana hiyo na wala haina kihisishi mahususi kutoka nje.10
ii) Ndani ya An-Nasai na At-Tirmidhi imepokewa: “Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi nakuomba na kutawasali Kwako kupitia Mtume wako Mtume wa Rehema, ewe Muhammad, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu hakika mimi natawasali kwa Mola Wangu Mlezi katika haja yangu kupitia kwako ili ikubaliwe, ewe Mwenyezi Mungu mfanye Muhammad kuwa mwombezi wangu.”
Hizi ni miongoni mwa dua ambazo waislamu wanatawasali kwazo kupitia Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) baada ya kifo chake.
MDAHALO DHIDI YA IBNU TAYMIYYA KUHUSU MWELEKEO WAKE KATIKA DUA HII
Kumetokea tofauti kati ya Ibnu Taymiyya na wafasi wake kuanzia As- Salafiya mpaka Mawahabi juu ya suala la kutawasali kupitia Manabii na Mawalii baada ya vifo vyao. Yeye anaona kuwa hairuhusiwi kutawasali kupitia wafu, na yafuatayo ni maneno yake kisha mdahalo:
“Katika Tawassuli hakuna kuomba kupitia viumbe wala kutaka msaada kupitia kiumbe bali ni kuomba na kutaka msaada kupitia Mwenyezi Mungu. Lakini kuna kuomba kupitia jaha yake kama ilivyo ndani ya Sunan Ibnu Majah kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.) kuwa alisema katika dua ya mtu aliyetoka kuswali aseme: “Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi nakuomba kupitia haki ya waombaji Kwako……. Hadithi.”
Hivyo ndani ya Hadithi hii aliomba kupitia haki ya waombaji kwa Mwenyezi Mungu…. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ameweka juu ya nafsi yake haki…. (mpaka akasema): Na kuna kundi limesema: Katika dua hii hakuna ruhusa ya kutawasali kupitia yeye (s.a.w.w.) baada ya kifo chake na kipindi cha kutokuwepo kwake, bali kuna kutawasali zama za uhai wake na kipindi cha kuwepo kwake……”
Kisha akaanza kutetea rai hii ya mwisho, akasema: “Na hiyo Tawassuli ya kupitia yeye (s.a.w.w.) ni kuwa wao walikuwa wakimwomba awaombee na yeye anawaombea na wanaomba pamoja naye na wanatawasali kupitia shufaa yake na dua yake.”
Akafananisha hilo na Hadithi ya bedui: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu mali zimeangamia na njia zimekatika, tuombee Mwenyezi Mungu azizuie dhidi yetu.”
Akasema: “Huku ndiko kulikuwa kutawasali kwao kupitia yeye (s.a.w.w.) katika kuomba mvua na mfano wake, na Mtume alipofariki walitawasali kupitia Abasi, na pia Muawiya bin Abu Sufiyan aliomba mvua kupitia Yazid bin Al-Aswad Al-Jarashi akasema: “Ewe Mwenyezi Mungu hakika sisi tunaleta maombi kwako kupitia wabora wetu, ewe Yazid inua mikono yako kwa Mwenyezi Mungu……”
Kisha akamalizia kwa kusema: “Hakuna mwanachuoni yeyote aliyesema kuwa inaruhusiwa kisheria kutawasali na kuomba mvua kupitia Mtume na Walii baada ya kifo chake wala kipindi cha kutokuwepo kwake. Na wala hawakulifanya hilo kuwa ni Sunna katika kuomba mvua wala katika kuom- ba msaada wala katika dua za aina nyingine, ilihali dua ndio ubongo wa ibada.”11
Ndani ya maneno haya kuna mgongano na mchanganyo na upotoshi wa maneno waziwazi zaidi ya sehemu moja. Tutaanza kuufichua kabla ya kutoa dalili juu ya maudhui.
1. Amechanganya kati ya kutawasali kupitia Mtume (s.a.w.w.) na kutawasali kupitia jaha. Kuna tofauti kubwa kati ya kauli yake: “Ewe Muhammad, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hakika mimi naelekea kwa Mwenyezi Mungu kupitia kwako.” Na kati ya kusema: “Ewe Mwenyezi Mungu kupitia haki ya waombaji kwako.” Au “Ewe Mwenyezi Mungu kupitia haki ya Muhammad (s.a.w.w.).”
Wa mwanzo ameelekea na kutawasali kupitia yeye (s.a.w.w.) na wa pili kaelekea na kutawasali kupitia haki yake na jaha na cheo chake, hivyo aina mbili hizi za kutawasali za kupitia Manabii na Mawalii zinaingia chini ya kifungu hiki. Na Ibnu Taymiyya amemfasiri wa mwanzo kuwa ni sawa na wa pili, nayo ni tafsiri isiyo sahihi.
2. Hapa amechanganya kama alivyochanganya kabla, kati ya kuelekea kupitia Mtume (s.a.w.w.) na kati ya kuomba akuombee. Kitofautishi kiko wazi na wala haifichiki kuwa amefanya hili ili kupotosha maana na wala si jingine. Na ndio maana utamwona alipotoa dalili kutumia Hadithi ya bedui alileta kipande tu na akaacha kauli yake tuliyoitaja mwanzo “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hakika sisi tunakufanya mwombezi kwa Mwenyezi Mungu.” Ambayo Mtume (s.a.w.w.) aliithibitisha.
3. Amejipinga mwenyewe katika kunukuu kutoka kwa wanachuoni, kisha akakimbilia kwenye kifungu cha dua ya kuomba mvua na kitu kingine ili kupotosha bongo na si jingine, kwa sababu alirudi na kukusanya aina zote za dua “Na wala hawakulifanya hilo kuwa ni Sunna katika kuomba mvua wala katika kuomba msaada wala katika dua aina nyingine.”
Mwanzo amenukuu kutoka kwa wanachuoni kauli yao ikiruhusu kutawasali kupitia Mtume (s.a.w.w.) zama za uhai wake na baada ya kifo chake, kisha akarudi akasema: “Hakuna mwanachuoni yeyote aliyesema inaruhusiwa kisheria kutawasali na kuomba mvua kupitia Mtume na Walii baada ya kifo chake.”
Na hapa tunakuja kwenye yale yanayopingana na haya madai yake kupitia dalili ambazo yeye mwenyewe baadhi yake amekiri kuwa ni sahihi. Tumethibitisha na tunasisitiza kuwa Ibnu Taymiyya hajapata maelezo (ya Qur’ani na Hadithi) yanayoonyesha kukatazwa kutawasali kupitia Mtume (s.a.w.w.), hivyo akakimbilia kutafsiri baadhi ya maelezo kwa maana isiyotafsirika.
Na hapa tutamwona jinsi gani anazungusha mgongo wake dhidi ya maele- zo ambayo yamethibiti kwake kuwa ni sahihi kwa namna isiyo na shaka: Ananukuu kwa njia anazojua kuwa ni sahih kutoka kwa Sahaba Mheshimiwa Uthman bin Hunayf kuwa anawafunza watu kutawasali kupi- tia Mtume (s.a.w.w.) zama za Uthman bin Affan, kisha anamfanya mwombezi kupitia habari zilizowakilishwa kutoka kwa wanachuoni waliotangulia.
Anasema: Al-Bayhaqiyu amepokea kuwa kuna mtu alikuwa akienda mara kwa mara kwa Uthman bin Affan kumwomba haja na Uthman alikuwa hamjali na wala hamtekelezei haja yake, basi mtu huyo akakutana na Uthman bin Hunayf na kumlalamikia hilo, Uthman bin Hunayf akamwambia: “Nenda sehemu ya kutawadhia utawadhe kisha nenda msik- itini na uswali rakaa mbili kisha useme: “Ewe Mwenyezi Mungu, hakika mimi nakuomba na naelekea Kwako kupitia Mtume wetu Muhammad Mtume wa Rehema. Ewe Muhammad hakika mimi naelekea kwa Mola Wangu Mlezi kupitia kwako ili anitimizie haja yangu.” Kisha nenda ili niende pamoja na wewe.”
Mtu yule akaenda na kufanya hayo, kisha baadae akamwendea Uthman bin Affan. Mlinzi akaja na kumshika mkono kisha akamwingiza kwa Uthman na kumketisha huku wakikaa pamoja juu ya busati na akamwambia: “Angalia haja yako uliyonayo.” Akataja haja yake na akamtimizia. Kisha mtu yule akatoka kwake (kwa Uthman bin Affan) na kukutana na Uthman bin Hunayf na kumwambia: “Mwenyezi Mungu akulipe kheri, hakuwa akisikiliza haja yangu wala kunijali mpaka uliponisemeza maneno.”
Uthman bin Hunayf akasema: “Sikuyasema lakini nilimsikia Mtukufu Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) akiwa amejiwa na kipofu na kumlalamikia kupofuka kwa macho yake. Mtume (s.a.w.w.) akamwambia: “Au uvumilie.” Kisha akasimulia Hadithi iliyotangulia.
Al-Bayhaqiyu amesema: “Bado tunaendelea na Ibnu Taymiyya- Ameipokea kwa urefu Ahmad ibnu Shabibu bin Said kutoka kwa baba yake. Na pia ameipokea Hisham Ad-Dastawiyu kutoka kwa Abu Jafar kutoka kwa Abu Umama bin Sahli kutoka kwa ami yake Uthman bin Hunayf.
Kisha Ibnu Taymiyya ametaja njia nyingi za upokezi wa Hadithi hii na kudai ni sahihi mpaka akasema: “Kuna riwaya iliyopokewa kutoka kwa wema waliotangulia kuhusu hilo, mfano riwaya aliyoipokea Ibnu Abu Ad- Dunia kwa njia yake ndani ya kitabu chake (Majani Duai):
Alikwenda mtu kwa Abdul-Malik bin Said bin Abjuru akapima tumbo lake na kumwambia: “Una ugonjwa usiopona.” Mtu yule akasema: “Ni upi?” Akasema: “Majipu ya tumboni.” Yule mtu akabadilika na kusema: Allah, Allah, Allah ndio Mola wangu Mlezi simshirikishi na chochote, ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi naelekea kwako kupitia Mtume Wako Muhammad Mtume wa Rehema, Rehema na Amani ziwe juu yake, ewe Muhammad hakika mimi naelekea kwa Mola Wako na Mola Wangu kupi- tia kwako anirehemu dhidi ya ugonjwa nilio nao.
Akasema: Akapima tumbo lake na kusema: “Umepona hauna ugonjwa.” Ibnu Taymiyya akaongeza kwa kusema: “Dua hii na mfano wake ime- pokewa kuwa waliiomba wema waliyotangulia na
imenukuliwa kutoka kwa Ahmad bin Hambali ndani ya (Mansakul-Marawaziyu)
Tawassuli kupitia Mtume (s.a.w.w.) ndani ya dua.”12
Hivyo ndivyo anavyothibitisha ubatili wa rai yake na kubatilika madai yake yaliyotangulia ya kuwa haijanukuliwa kutoka kwa yeyote miongoni mwa wema waliyotangulia kuwa alitawasali kupitia Mtume (s.a.w.w.) baada ya kifo chake.
Hili ni dai ambalo alilolitamka wazi na kuliweka mbele ya kitabu chake:
At-Tawassulu Wal-Wasilatu.13
Kwa maelezo haya inathibiti kuwa hakuwa na lengo lolote katika madai yake ila ni kung’ang’ania rai batili ambayo dalili thabiti zinathibitisha ubatilifu wake. Na ukweli ni kuwa kilichothibiti kutoka kwa wema waliotangulia ni kingi sana kuliko hayo na wala hawakukomea kutawasali kupitia Mtume (s.a.w.w.) tu baada ya kifo chake, bali walitawasali kupitia mwingine waliyemwona anafaa na kuamini kuwa ana jaha na shufaa mbele ya Mwenyezi Mungu.14
•    1. Rejea Minihajus-Sunna cha Ibnu At-Taymiyya.
•    2. Mariyam: 62.
•    3. Sahih Bukhari 5: 76. Siratu Ibnu Hishami 2: 639, humo imesemekana kuwa aliyehoji ni Umar.
•    4. Rejea Sunanu Abu Dawudi 2: 218. Kanzul-Ummal 10: 38. Twabaqatu Ash- Shafiiyatu cha As-Sabkiyu 3: 406-408.
•    5. Kanzul-Ummal 5: 135, Hadithi ya 12372.
•    6. Al-Imrani: 154.
•    7. Al-Qasas: 35.
•    8. Tazama Al-Barahinu Al-Jaliyatu cha As-Sayyidu Muhammad Hasan Al- Qazwini: 42.
•    9. Musnad Ahmad 3: 21. Sunanu Ibnu Majah 1: 356.
•    10. Rejea Az-Ziyaratu Wat-Tawassulu cha Swaibu Abdul-Hamidi: 142.
•    11. Ziyaratul-Quburi wal-Istinjadi bil-Quburi: 37-43.
•    12. Tazama At-Tawassulu wal-Wasila: 97, 98, 101-103.
•    13. At-Tawassulu wal-Wasila: 18.
•    14. Rejea Az-Ziyaratu Wat-Tawassulu cha Swaibu Abdul-Hamid: 148-152, kili- chotolewa na Markazi Ar-Risala.
MWISHO WA MSURURU WA MAKALA HIZI ZA: TAWASSULI

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini