Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI (SEHEMU YA TISA)

0 Voti 00.0 / 5

KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI (SEHEMU YA TISA)
MLANGO WA 9: KUNYONYESHA
CHAKULA KWA AJILI YA MTOTO ALIYEZALIWA PUNDE
Mwenyezi Mungu Mtukufu ameweka chakula na maji kwa ajili ya mtoto katika mwili wa mama, na ameumba mfumo wa kushangaza wa kumlisha kichanga aliyezaliwa punde kwa njia ambayo ni kamilifu na yenye manufaa sana.
Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.): “Ewe mama wa Is’haaq, usimlishe mtoto kutoka kwenye titi moja tu, bali umlishe kutoka kwenye matiti yote mawili, kwani moja ni badala ya chakula na jingine ni badala ya maji.” 1
Katika riwaya nyingine, imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Allah (s.w.t.). ameweka riziki ya mtoto katika matiti mawili ya mama yake, ndani ya moja ni maji yake na katika jingine ni chakula chake.” 2
Kwa vile sasa tuko kwenye mas’ala ya ulishaji wa mtoto aliyezaliwa punde moja kwa moja kutoka kwa mama yake, ni lazima tena hapa kutaja na kusisitiza umuhimu wa kipato cha halali, ulipaji wa Khums na Zaka, matu- mizi ya chakula safi na halali kwa mama na athari zake kwa mtoto. Mwenyezi Mungu Mtukufu ameeleza umuhimu wa kula chakula halali na kizuri mara nyingi ndani ya Qur’ani Tukufu3 na hadithi zimesisitiza wazi kwamba kukosa kulishikilia hili ni moja ya sababu za chanzo cha tabia (akhlaq) mbaya, ushari na uonevu. Vile vile imeelezwa kama ni chanzo cha kukosa utiifu kulikotolewa kwa Imam Husein (a.s.) kutoka kwa maadui zake na hivyo yakatokea masaibu ya Karbala.
Kufungamana na matokeo ya kula chakula haramu, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesimulia: “Kila wakati tonge la chakula cha haramu linapoingia ndani ya tumbo la mtu, malaika wote wa mbingu na ardhi hutupa laana juu yake, na mpaka wakati ambapo lile tonge haramu limo ndani ya tumbo lake, Mwenyezi Mungu haangalii upande wake aliko. Kila mtu ambaye anakula tonge la chakula haramu anajikusanyia sababu za ghadhabu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu Halafu, iwapo akatubia, Mwenyezi Mungu huipokea toba yake na endapo atafariki dunia bila ya kutubia, basi anastahili moto wa Jahannam.4
MIFANO MITATU
Ili kuweza kusisitiza hayo hapo juu, na kadhalika baadhi ya njia zilizopendekezwa za unyonyeshaji na matokeo yake, mifano mitatu ya maisha ya maulamaa wetu imetajwa hapa chini:
1. Ilisemwa kwa mama yake Sheikh Ansaarii, mmoja wa Ulamaa wa Shi’ah wa kuheshimika: “Mashaallahu, mtoto mzuri kiasi gani uliyemleta kwenye jamii!” Huyo mama akajibu: “Nilikuwa na matumaini makubwa juu ya mwana wangu, kwa sababu nilimnyonyesha kwa miaka miwili na kamwe sikuwa bila ya Wudhuu. Wakati mwanangu alipolia katikati ya usiku na akataka maziwa, mimi niliamka, nikachukua Wudhuu, kisha ndipo nikamnyonyesha mwanangu.”5
2. Aliulizwa pia mama yake Muqaddas Ardabiili kwamba, ni nini chanzo cha hadhi ya hali ya juu ya mwanao? Yeye akajibu akisema: “Mimi sikuwahi kamwe kula kipande cha chakula chenye wasiwasi, na kabla ya kumpa mwanangu maziwa yangu kwanza nilichukua Wudhuu. Kamwe sikumtazama mtu ambaye sio maharim wangu (ambaye kuoana naye kunaruhusiwa), na baada ya kumuachicha kwake kunyonya, nilichunga usafi na utakaso na kumfanya akae na kucheza na watoto wema.”6
3. Haj Sheikh Fadhkullah Nuuri, Mujitahidi anayeenziwa ambaye alinyongwa wakati wa uhai wake, alikuwa na kijana ambaye alikuwa ni aina ya mtu ambaye alijaribu kufanya baba yake anyongwe. Mmoja wa wanavyuoni mashuhuri anasimulia: Nilikwenda kukutana na marehemu Nuuri huko gerezani na nikamuuliza. “Huyu mtoto wako angepaswa kuwa mtoto wa mtu muungwana, na mrithi wako bora. Kwa nini yeye ni duni kiasi hicho kwamba anakuzungumzia vibaya na hata anadiriki kufurahia kuuliwa kwako?”
Marhum Nuuri alijibu: “Ndio, mimi nililijua hili na nilikuwa na hofu hiyo.” Kisha aliendelea akasema: “Mtoto huyu alizaliwa huko Najaf. Alipokuja kwenye ulimwengu huu, mama yake aliugua na hakuweza kum- nyonyesha maziwa yake. Tulilazimika kupata mama mnyonyeshaji wa kuajiriwa ili ampatie maziwa. Baada ya muda kitambo wa kunyonyesha, tuligundua kwamba mwanamke huyu ni dhalim (si mwenye tabia njema), na juu ya hayo, ni adui wa Imam Ali (a.s.) na Ahlul-Bayt wote (a.s.). Kwa wakati ule, kengele za tahadhari zilianza kulia kwa ajili yangu.”
Wakati wa kunyongwa kwa baba huyu, mtoto wake alisimama na kushangilia pamoja na wajinga wengine, na yeye pia hatimaye alitoa mtoto kwenye jamii ambaye si mwingine zaidi ya Nuuruddin Kianuri, kiongozi wa Hizb-e Tude (Chama cha Kikomunisti cha Irani);7 huyu ni mtoto wa kiume wa mtu yule yule aliyepiga makofi kushangilia wakati wa kuny- ongwa baba yake.8
THAWABU ZA KUNYONYESHA
Kuna hadithi nyingi sana zinazosimulia thawabu za kunyonyesha, kama zile ambazo zimesimuliwa katika sehemu ya Umuhimu wa Umama katika Mlango wa tano, ambapo mama anayenyonyesha amefananishwa na mtu anayepigana katika njia ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na endapo anafariki katika wakati huu, anapata thawabu za Shahidi.
UMUHIMU WA MAZIWA YA KIFUANI
Imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Kwa ajili ya mtoto, hakuna maziwa bora zaidi kuliko maziwa ya mama yake.”9 Mtume vile vile amesema kwamba hakuna kinachoweza kuchukua nafasi mbadala ya chakula na maji isipokuwa maziwa.10 Kadhalika, imesimuliwa kutoka kwa Imam Ali (a.s.) kwamba hakuna maziwa yenye baraka zaidi kwa mtoto kuliko yale maziwa ya mama.11
Kunyonyesha sio kumlisha mtoto tu, bali pia ni kubadilishana mapenzi na uimarishaji wa moyo. Wakati mtoto anaponyonya, anaweza kusikia sauti ya moyo wa mama yake na hili linasababisha uburudikaji na utulivu. Watoto walionyonyeshwa huelekea kuwa na afya zaidi na timamu zaidi katika masuala ya afya ya kimwili na kiroho na wanasaikolojia wanaamini kwamba kunyonyesha kunawaweka watoto wenye furaha na kuridhika na pia kuna athari katika Akhlaq zao.
Kunyonyeshwa ni moja ya haki za mtoto na pia inahesabiwa kama ni haki ya mama, na imekokotezwa sana ndani ya Qur’ani na hadithi. Kwa kweli, manufaa yake yanakubalika sana katika ulimwengu wa leo. Kwa hakika, inapasa kuzingatiwa akilini kwamba kunyonyesha kunashauriwa tu endapo kama hakutaleta hatari yoyote kwa mama au mtoto.
FAIDA ZA MAZIWA YA KIFUANI 12
1. Maziwa ya kifuani yana virutubisho vyote muhimu ambavyo mtoto anavihitaji ndani ya miezi 4 – 6 ya mwanzo ya maisha.
2. Maziwa ya kifuani yanazo protini na mafuta yanayofaa kuridhisha mahitaji ya kawaida ya mtoto.
3. Kuna kiasi kikubwa cha laktosi katika maziwa ya kifuani kuliko kwenye aina nyingine za maziwa, kwani hii ndio inayohitajiwa na mtoto.
4. Kuna vitamini za kutosha ndani ya maziwa ya kifuani, zinazohakikisha kwamba hakuna vitamini za ziada ama maji ya matunda yanayohitajika.
5. Madini ya chuma ndani ya maziwa ya kifuani yanatosha kwa ajili ya mtoto. Hata kama viwango vikiwa sio vya juu sana, uwezo wa mtoto wa kunyonya kile kiasi cha lazima ni mzuri sana.
6. Maziwa ya kifuani yana maji ya kutosha kwa ajili ya mtoto, hata kama mtu anaishi katika tabia ya nchi iliyo kavu.
7. Maziwa ya kifuani yana chumvi ya kutosha, kalisi na fosfati kwa ajili ya mtoto.
8. Maziwa ya kifuani yana kimeng’enya kiitwacho lipase kinachomeng’enya mafuta.
9. Mtoto aliyenyonyeshwa sio mwepesi wa kuambukizwa kutokana na kinga iliyoongezeka.
10. Maziwa ya kifuani ndio kinga muhimu dhidi ya sababu mbili kuu za vifo miongoni mwa watoto: magonjwa ya kuhara na maambukizi kwa njia ya hewa.
11. Kunyonyeshwa kunapunguza magonjwa yanayotokana na mizio (aleji) kama vile pumu, ukurutu na kadhalika, na kunasaidia kukinga au kupunguza baadhi ya magonjwa wakati mtoto anapokuwa kwenye umri wa kijana na kuendelea juu zaidi.
12. Kisukari na baadhi ya matatizo ya mmeng’enyo yanakuwa machache kwa watoto walionyonyeshwa.
13. Kunyonyesha kunasaidia watoto wagonjwa kupona haraka zaidi; kwa hiyo ni muhimu sana kwamba kusisimamishwe katika wakati huu.
14. Maziwa ya kifuani ni rahisi na haraka kumeng’enya, kwa hiyo, watoto walionyonyeshwa wanaelekea kushikwa na njaa haraka kuliko watoto walionyonyeshwa maziwa ya aina nyingine.
15. Maziwa ya kifuani wakati wote yako tayari na hayana haja ya mata- yarisho yoyote.
16. Maziwa ya kifuani hayaharibiki kamwe na wala hayawi chachu, hata kama mtoto atakuwa hajanyonya kwa muda wa siku kadhaa chache.
17. Unyonyeshaji wa kawaida, na kunyonyesha wakati mtoto anapohitajia kunazuia ushikaji wa mimba.
18. Mawasiliano ya kawaida kati ya mama na mtoto katika siku za mwan- zoni za maisha yake kunaongeza fungamano la kiroho na la kimwili baina ya wawili hao, kuelekezea kwenye uhusiano mzito na wa upendo na mafunzo na malezi bora ya mtoto huyo.
19. Maziwa ya kifuani hayahitaji gharama yoyote ile.
20. Watoto walionyonyeshwa wanakuwa na umahiri wa uoni, uzungumzaji na utembeaji haraka sana.
21. Kule kunyonya kwa mtoto mara tu baada ya kuzaliwa kunasababisha muamsho wa oksitosini ambako kunaishia katika mnyweo wa tumbo la uzazi, na hivyo kupunguza utokaji wa damu kwa mama huyo.
22. Akina mama wanaonyonyesha wana uwezekano mdogo wa kupata saratani ya matiti au ya tumbo la uzazi.
23. Wanawake wanaonyonyesha wanarejea haraka sana kwenye miili yao ya wakati wa kabla hawajapata mimba kwa vile mafuta yao ya uzazi yanatumika haraka.
24. Maziwa ya kifuani ya mama hubadilika kulingana na mahitaji ya kila siku ya mtoto. Kuna tofauti vile vile kati ya akina mama kutegemeana na mahitaji ya watoto wao, kwa mfano, maziwa ya mama wa mtoto ambaye hajatimiza kipindi (cha ndani ya mimba – kabichi) na maziwa ya mama wa mtoto wa kipindi kamili aliyetimia.
25. Watoto walionyonyeshwa wana maarifa zaidi hata wanapokuwa wachanga kabisa (yaani, zile wiki nne za mwanzo za uhai wao). Utafiti umeonyesha kwamba watoto hawa wanacheza zaidi katika zile wiki mbili za mwanzo na waonyesha mishughuliko mingi kuliko watoto wengineo.
26. Watu wazima ambao waliwahi kunyonyeshwa huelekea kuwa madhubuti zaidi na wepesi kwa tabia.
KIPINDI CHA MUDA ULIOPENDEKEZWA KWA KUNYONYESHA
Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika Suratul-Baqarah, Aya ya 233 kama ifuatavyo:
وَالْوَالِدَاتُ يُرْضِعْنَ أَوْلَادَهُنَّ حَوْلَيْنِ كَامِلَيْنِ ۖ لِمَنْ أَرَادَ أَنْ يُتِمَّ الرَّضَاعَةَ ۚ{233}
“Na wanawake waliozaa wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kamili kwa anayetaka kukamilisha kunyonyesha ………” (Al- Baqarah; 2:233).
Na katika Surat al-Ahqaf, Aya ya 15, Mwenyezi Mungu anasema:
وَحَمْلُهُ وَفِصَالُهُ ثَلَاثُونَ شَهْرًا ۚ{15}
“….. Na kumbeba na kumwachisha ziwa ni miezi thelathini …..” (Al-Ahqaf; 46:15)
Kama ilivyoonyeshwa katika Aya hizo hapo juu, muda ulioshauriwa katika Uislam kwa ajili ya kunyonyesha ni takriban miaka miwili. Ni dhahiri vilevile kutoka kwenye hadithi kwamba muda wa kunyonya wa Imam Husein (a.s.) pia ulikuwa miezi ishirini na nne.13
Ahlul-Bayt (a.s.) wanayo mapendekezo kadhaa juu ya kipindi cha kunyonyesha. Katika baadhi ya hadithi, imesimuliwa kwamba kunyonyesha kwa muda chini ya miezi 21 kunahesabiwa kama ni uonevu na shari dhidi ya mtoto.14 Ndani ya riwaya nyinginezo, kunyonyesha kwa muda wa miezi 21 kunaonekana kama ni muhimu na ni lazima.15 Kadhalika, imesimuliwa katika hadithi kwamba kunyonyesha kwa zaidi ya miaka miwili pia kumekatazwa.16
VITENDO VINAVYOSHAURIWA
1. Mama anapaswa kuwa na uchamungu, na awe mwangalifu kwamba maziwa yasije yakachafuka kutokana na kukosa uchamungu na maadili. Hususan katika kipindi cha kunyonyesha, mtu anapaswa kujitenga na aina zote za dhambi. Matendo mema na ukaribu na Allah yana matokeo na athari njema kwa mtoto.
2. Usome “Bismillah” kabla ya kuanza kunyonyesha. Imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Kila tendo la muhimu na la thamani ambalo linatendeka bila ya utajo wa “Bismillahi Rahmani-Rahim,” litakuwa halikukamilika na halitakuwa na matokeo mema.”
3. Mnyonyeshe mtoto pamoja na kumkumbuka Imam Husein (a.s.), kwani imesimuliwa kutoka kwa Imam huyo: “Enyi Shi’ah wangu, kila wakati mnapokunywa maji yenye siha basi nikumbukeni mimi.”
4. Wakati wa kunyonyesha mwangalie mtoto huyo na uzungumze naye.
Hususan kuzungumza juu ya vifo vya kishahidi na kuzaliwa kwa Ma’asumin (a.s.) kunashauriwa sana; usijali kama mtoto anaelewa au laa. Mama anayetaka kupitisha (kurithisha) utamaduni na desturi ya Ahlul-Bayt (a.s.) kwa mtoto wake anahitajia kuwa na utamaduni wa kidini yeye mwenyewe na alitekeleze hili wakati anapomfundisha na kumnyonyesha mtoto wake.
5. Subira na utulivu, hasira na hali ya kukasirika mawazo mazuri na mabaya, tabia ya ukarimu na huruma na ukaidi na hali ya ulipizaji visasi vyote hivi vina athari kwa mtoto. Ni lazima na muhimu kukumbuka kwam- ba mustakabali wa mtoto uko mikononi mwa vitendo vyako wewe.
6. Kila siku ya wiki, tekeleza majukumu yako ya kila siku kama vile kupika, kufanya usafi, kula na kunyonyesha, huku ikiwa ni pamoja na kumkumbuka Ma’sumin wa siku hiyo, kama ilivyoainishwa katika Mafatihul-Jinan:
Jumamosi: Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w.).
Jumapili: Imam Ali (a.s.) na Hadhrat Fatimah(a.s.).
Jumatatu: Imam Hasan na Imam Husein (a.s.).
Jumanne: Imam Zainul-Abidiin (a.s.), Imam Muhammad al-Baqir na Imam Ja’far as-Sadiq (a.s.).
Jumatano: Imam Musa al-Kadhim, Imam Ali ar-Ridhaa, Imam Muhammad at-Taqii na Imam Ali an-Naqii (a.s.).
Alhamisi: Imam Hasan al-Askarii (a.s.).
Ijumaa: Imam Mahdi (a.s.).
7. Kama ilivyoshauriwa na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), uanze vitendo vyako kwa Qur’ani Tukufu, na kumdhukuru Mwenyezi Mungu na kuwakumbuka Ahlul-Bayt (a.s.) – (Pamoja na Duaul-Faraj kwa ajili ya Imam Mahdi a.s.).
8. Mshukuru na kumtukuza Mwenyezi Mungu Mtukufu baada ya kunyonyesha kwako.
9. Mwishowe kabisa, vifanye vitendo vyako, hususan kunyonyesha, kwa nia ya kutafuta radhi za
Mwenyezi Mungu Mtukufu na ukaribu Naye.
KUMUACHISHA MTOTO ZIWA (KUNYONYA)
Ni17 muhimu kumkumbusha msomaji kwamba ingawa kuna njia nyingi sana za kumuachisha mtoto ziwa, kitabu hiki kinataja chache tu ambazo zimeelezwa katika vyanzo vya Kiislam na Ahlul-Bayt (a.s.):
1. Usiwe mkali kwa mtoto, na ujiepushe mbali na mbinu kama za kupaka viungo vikali kama pilipili,
na kadhalika.
2. Wakati mtoto anaposisitiza katika kunyonya, usimfukuzie mbali na wewe.
3. Kwa kuzingatia ukweli kwamba kunyonyesha sio kwamba ni chanza cha chakula tu, bali kwamba ni chanzo cha ukaribu na utulivu kwa ajili ya mtoto vilevile, ni muhimu kwamba, sambamba na vyakula vingi mbadala, upendo mwingi na wakati mzuri pamoja na mtoto hakikisha vinapatikana pia.
4. Kuchagua wakati muafaka na mahali pazuri kwa ajili ya kuanza na kumalizia kwa vitendo, hususan vile vyenye muhimu na thamani, ni moja ya mbinu za wanavyoni wa Kiislam.
Kwa hiyo, inastahili tu kwamba kwa ajili ya kumkatisha mtoto kutoka kwenye kitendo muhimu kama cha kunyonya, mahali na wakati mzuri vichaguliwe, na kutekelezwa kwa kutiliwa maanani ule utayari wa mtoto na uwasilishaji wa fursa nzuri.
5. Pale inapowezekana, mahali bora zaidi ni kwenye haraam (quba) za Maimam (a.s.) au Imamzade (maquba ya watoto wa Maimam).
6. Ushauri wa mwanachuoni ni kama ufuatao:
Katika miezi ya mwisho ya unyonyeshaji wakati uamuzi unapokuwa umefanyika wa kumsimamisha polepole mtoto kunyonya, chukua wudhuu na uingie kwenye haraam katika hali ya kutakasika. Mara unapoifikia kaburi tukufu (dariih), soma ziarat inayostahili na uombe tawasuli (uombezi mtukufu) wa mtu huyo mtukufu. Halafu chukua komamanga tamu lililomenywa na ukae ukielekea Qiblah. Wakati unaposoma Surat Yaasin, mnyonyeshe mtoto kutoka kwenye matiti yote hadi maziwa yanapokwisha, na upulize kwenye komamanga hilo mara kwa mara.
Mwishoni mwa kisomo hicho, wasilisha thawabu za kisomo hicho ziende kwa roho ya Ali Asghar, mtoto wa miezi sita, na kwa mama yake. Kisha muombe Mwenyezi Mungu akikubalie kipindi hicho cha unyonyeshaji kwa ukarimu Wake, na akujaalie na riziki yenye maana kwa watoto wako kwa kwisha kipindi cha kunyonyesha. Kisha mlishe mtoto hilo komamanga lote (au majimaji yake – juisi).
Angalizo: Utamu wa komamanga umetiliwa mkazo mahsusi hasa. Pia kwa kawaida, ulaji wa komamanga ni wenye manufaa sana, hususan katika siku za Ijumaa, na limehusishwa na utulivu uliozidi kiasi, na kuondoa fadhaa na wasiwasi.
Angalizo: Kama kwenda kwenye Haraam hakuwezekani kwa sababu za kijiogorafia au nyinginezo, inawezekana kufanya nia ya kutembelea Quba na kufanya vitendo vyote vilivyoshauriwa ukiwa nyumbani.
REJEA:
•    1. al-Kafi, Jz. 6, Uk. 40, hadithi ya 2
•    2. Wasa’ilush-Shi’ah, Jz. 21 Uk. 453
•    3. Surat al-Abasa; 80:24, na Surat al-Baqarah; 2:167 na 172
•    4. Thawab al-Amaal, Uk. 566
•    5. Rayhaaney-e Behesht, Uk. 177
•    6. Mafasid Maal wa Luqme Haraam.
•    7. Kianuri alikuwa aina ya mtu ambaye alitekeleza vitendo vya kukiri mwenyewe vya “kijasusi, udanganyifu na uhaini.”
•    8. Tarbeat Farzand az Nazr Islam, Uk.89
•    9. Mustadrak al-Wasa’il, Jz. 15, Uk. 256
•    10. Tibb an-Nabii, Uk. 25
•    11. al-Kafi, Jz. 6, Uk. 40.
•    12. Rayhaaney-e Behesht, Uk. 184-187
•    13. Mustadrak al-Wasa’il, Jz. 15, Uk. 157, hadithi ya 17848
•    14. Tahdhib al-Balaghah, Jz. 8, Uk.106, hadithi ya 6
•    15. Tahdhib al-Balaghah, Jz. 8, Uk.106, hadithi ya 7
•    16. Tahdhib al-Balaghah, Jz. 8, Uk.105, hadithi ya 4
•    17. Rayhaaney-e Behesht, Uk. 212-213
ITAENDELEA KATIKA MAKALA IJAYO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini