Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

SWALA NI NGUZO YA DINI (SEHEMU YA KWANZA)

0 Voti 00.0 / 5

SWALA NI NGUZO YA DINI (SEHEMU YA KWANZA)
SWALA: Ni matendo na maneno ambayo hujenga mahusiano kati ya Muumba na kiumbe, hivyo mja akiikata, basi mawasiliano yake na Mola wake hukatika.
Allah Mtukufu anasema: “Kwa hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu hakuna aabudiwaye ila Mimi tu, basi niabudu na simamisha Swala kwa kunitaja.”1
THAMANI YA SWALA NDANI YA UISILAMU:
Swala huchukuliwa kuwa miongoni mwa mambo ya dharura zaidi ya Uisilamu na nguzo zake. Imepokewa kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kuwa alisema:
“Swala ni nguzo ya dini, ikikubaliwa matendo mengine hukubaliwa, na ikikataliwa na matendo mengine hukataliwa”2
Daraja hii kubwa ya sala ndiyo tunayoiona katika Aya za Qur’an na Hadithi Tukufu, ikiwemo:
I. KUDUMISHA SWALA NI MIONGONI MWA SIFA MUHIMU ZA WAUMINI:
“Hakika wamefuzu wenye kuamini. Ambao ni wanyenyekevu katika Swala zao”.3
“Na ambao Swala zao wanazihifadhi.”4
II. KUTEKELEZA SWALA NI MIONGONI MWA SABABU ZA UDUGU WA KIISLAMU:
“Na kama wakitubu na wakasimamisha Swala na wakatoa Zaka, basi ni ndugu zenu katika dini …”5
III. KUSIMAMISHA SWALA NI MIONGONI MWA SIFA ZA JAMII BORA:
“Wale ambao tukiwapa madaraka katika nchi husimamisha Swala na hutoa Zaka na huamrisha yaliyo mema na hukataza yaliyo mabaya, na kwa Mwenyezi Mungu ndiko mwisho wa mambo”.6
IV. SWALA NI NYENZO YA MAFANIKIO:
“Hakika amekwishafaulu aliyejitakasa. Na akakumbuka jina la Mola wake na akaswali.”7
V. KUWAELIMISHA WATOTO SWALA NI KATIKA MAJUKUMU YA WAZAZI:
“Na waamrishe watu wako kuswali, na uendelee kwa hayo, hatukuombi riziki bali Sisi tunakuruzuku, na mwisho mwema ni kwa mcha Mungu.”8
VI. SWALA NI KATIKA NGUZO ZA DINI:
“Wala hawakuamrishwa ila kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtaka- sia yeye dini, hali wameshikamana na haki, na wanasimamisha Swala na kutoa Zaka, na hiyo ndiyo dini madhubuti.”9
VII. SWALA NI SHUKURANI KWA MNEEMESHAJI:
“Hakika Sisi tumekupa kheri nyingi.* Basi sali kwa ajili ya Mola wako, na uchinje.* Hakika adui yako ndiye aliyekatikiwa kizazi”10
ATHARI ZA SWALA NA SIRI ZAKE:
I. HULETA UTULIVU WA NAFSI
“Kwa hakika binadamu ameumbwa hali ya kuwa mwenye pupa.* Inapomgusa shari huwa mwenye fazaa.* Na inapomgusa kheri huwa anaizuilia.* Ila wanaosali.”11
II. NI KINGA YA MUUMINI
“Na ombeni msaada kwa subira na Swala na kwa hakika jambo hilo ni gumu isipokuwa kwa wanyenyekevu.”12
III. SWALA NI NJIA YA MAFANIKIO NA UKAMILIFU
“Na simamisha Swala katika sehemu mbili za mchana na nyakati za usiku hakika mema huyaondoa maovu, huo ndio ukumbusho kwa wenye kukumbuka.”13
“…Bila shaka Swala huzuia mambo machafu na maovu…”14
IV. SWALA HUMFUNDISHA BINADAMU MIPANGO NA NIDHAMU KATIKA MAISHA
“…Hakika Swala kwa wenye kuamini ni faradhi iliyo na wakati maalumu.”15
HUKUMU ZA SWALA
Ili kutekeleza Swala ambayo humaanisha kuhudhuria mbele ya Mungu wa ulimwengu na kudhihirisha utumwa na utii kwake, ni lazima vikamilike vitangulizi ambavyo ni lazima kuvitimiza kabla ya sala na ndani yake, huku ukiviambatanisha na mambo ya wajibu, na muda huohuo ukijiepusha na vibatilishi vyake.
VITANGULIZI VYA SWALA
Tohara: Hali hii imegawanyika sehemu mbili:
a) Tohara dhidi ya najisi: Nayo ni hali ya mwili na mavazi ya mwenye kusali kuwa tohara dhidi ya najisi.
b) Tohara dhidi ya hadathi: Nayo ni hali ya mwenye kusali kuwa na tohara yakimaana (ya ndani) huku akikusudia kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kupitia udhu au kuoga au tayammam.
Tohara hii ya pili ina hali mbili:
Ya kwanza: Wakati wa kupatikana maji: Wakati huo inawezekana kupata tohara kwa moja kati ya mambo mawili:
a. Udhu.
b. Kuoga kunakotosheleza udhu (Kama vile kuoga janaba).
Ya pili: Wakati wa kukosekana maji: Wakati huo inawezekana kupata tohara kwa njia ya kutayammamu (badala ya udhu na josho).
Mavazi ya mwenye kusali: Ni vile ambavyo mwenye kusali kuvitumia kuusitiri mwili wake na utupu wake wakati wa kusali.
Mahali pa kusalia: Ni mahali pa kutekelezea sala, ambapo ni sharti pawe pa halali. Vilevile mahali pa kusujudia pawe tohara.
Nyakati za Swala: Nazo ni zile nyakati zilizoainishwa na sharia kwa kila Swala ya faradhi.
Kibla: Ni upande wa Al-Kaaba tukufu ambayo mwenye kusali anataki- wa aelekeze uso wake na mwili wake wakati wa kusali.
•    1. Sura Twaha: 14.
•    2. Biharul-An'war, Juz. 47 Uk. 2.
•    3. Sura Al-Muuminun: 1 - 2.
•    4. Sura Al-Muuminun: 9.
•    5. Sura At-Tawba: 11.
•    6. Sura Al-Haji: 41.
•    7. Sura Al-Aaala: 14 - 15.
•    8. Sura Twaha: 132.
•    9. Sura Al-Bayyinah: 5.
•    10. Sura Al-Kawthar.
•    11. Sura Al-Maarij: 19 - 22.
•    12. Sura Al-Baqarah: 45.
•    13. Sura Hud: 114.
•    14. Sura Al-Ankabut: 45.
•    15. Sura An-Nisai: 103.
ITAENDELEA KATIKA MAKALA IJAYO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini