Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

WITO KWA WAISLAMU KUUENDEA UKWELI (SEHEMU YA KWANZA)

0 Voti 00.0 / 5

WITO KWA WAISLAMU KUUENDEA UKWELI (SEHEMU YA KWANZA)
MTUME MUHAMMAD ALIMTEUA IMAM ALI KUWA KHALIFA BAADA YAKE MAKALA NO. 1
BISMIHI TA'ALA
"NA KATIKA HAYA IMEKUJIA HAKI NA MAUIDHA NA UKUMBUSHO KWA WALE WANAOAMINI."(SURATUL HUD 11:120)
UTANGULIZI
Tofauti kubwa iliyopo baina ya Waislamu wa Kishia na Waislamu wa Kisunni ni juu ya imani ya Ukhalifa na Uimamu baada ya kuondoka kwa Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w). Sisi waislamu wa Kishia tunaamini kuwa Imam Ali bin Abi Talib (a.s) ni khalifa na Imam wa kwanza baada ya Mtume (s.a.w.w.) ambapo ndugu zetu Waislamu wa Kisunni wanaamini kwamba Seyidina Abubakar (r.a.) alikuwa ni khalifa wa kwanza.
Ingawa kuna tofauti nyingine ndogo ndogo zilizopo baina ya madhehebu makubwa ya Uislamu (Shia na Sunni) kwa mfano katika sheria (Fiqh) kama vile kukunja mikono wakati wa kusali au kuinyoosha n.k. lakini hizi ni tofauti ndogo ndogo sana ambazo zinaweza hata kupatikana ndani ya madhehebu manne ya Kisunni (Imam Shafi, Maliki, Hanafi na Hanbali ). Masuala haya tutayajadili hapo baadaye InshaAllah.
Mbali na tofauti hiyo kubwa kuna mambo yanayofanana katika imani za Waislamu wa Shia Ithna Ashariya na Waislamu wa Kisunni. La kwanza ni nguzo tano za Uislamu, yaani :
(a) Shahaada - Laa Ilaaha Illallah - Muhammadur Rasuulullah - Hakuna mungu apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah - na Muhammad ni Mtume wa mwisho wa Allah.
(b) Sala tano za kila siku
(c) Kufunga mwezi wa Ramadhan
(d) Kuhiji katika nyumba takatifu ya Kaa'ba
(e) Zakat kwa ajili ya maskini
Kwa pamoja Shia Ithna Asheriyya na Sunni wanaamini juu ya kitabu cha mwisho cha Allah Qur'an kuwa bado kipo vile vile bila mapunguzo au maongezo, na wanajaribu kufuata maamrisho yake bila kubakiza.
Kwa pamoja Shia Ithna Asheriya na Sunni wanaichukulia Sunnah na Siira ya Mtume kuwa ni muongozo kwa Waislamu katika maisha yao ya kila siku na wanajaribu kuifuata kwa uangalifu mkubwa ili wapate kuokoka hapa duniani na Akhera.
Ingawa wapo watu waharibifu katika jamii ambao kwa makosa wanatushutumu sisi Shia Ithna Asheriya kwa madai mbalimbali ya uongo kama vile kudai kuwa Shia wana Qur'an yao au madai kuwa eti Shia wanaamini juu ya Utume wa Imam Ali bin Abitalib, n.k. Wale wote wanaoutafuta ukweli, wanatakiwa kuyatupilia mbali madai (shutuma) haya maovu dhidi yetu na tunawaomba watembelee misikiti na madrasah zetu ambazo mara zote zipo wazi kwa Mwislamu yeyote kuja kuthibitisha imani zetu.
Kuna Shia zaidi ya millioni 250 duniani kote ambao wanaamini kuwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) ni Mtume wa mwisho na wanafuata maamrisho ya Qur'an na Sunna za Mtume (s.a.w.w.) katika maisha yao ya kila siku. Katika manispaa ya Dodoma peke yake, sisi Shia tuna misikiti miwili; Khoja Shia Masjid na Masjid Imam Mahdi (a.s) na tunawaalika waumini wote wa Kiislamu kututembelea katika misikiti hii ili kupata ushahidi kwa macho yao kuhusiana na imani na matendo yetu kabla ya kuangukia katika mtego wa waharibifu wanaotuzulia habari za uongo.
KWA NINI SHIA WANAAMINI KUWA IMAM ALI NI KHALIFA WA KWANZA BAADA YA MTUME ?
Shia Ithna Ashariya wanaamini kuwa Imam Ali bin Abitalib ni Khalifa na Imam wa kwanza baada ya Mtume (s.a.w.w.) kwa kuzingatia sababu moja rahisi sana na iliyo wazi. Sababu hii ni kuwa; "Imam Ali bin Abitalib (a.s) aliteuliwa kwa amri ya Mwenyezi Mungu kuwa Khalifa wa kwanza wa Waislamu na Mtume mwenyewe kwa amri ya Mwenyezi Mungu (s.wt). Hii ndio sababu na hakuna sababu nyingine.
Katika Qur'an tukufu (59: 7) Mwenyezi Mungu anasema: "-----Na anachokupeni Mtume basi pokeeni na anachokukatazeni jiepusheni nacho". Qur'an (33:36):
"Na haiwi kwa wanamume aliyeamini wala kwa mwanamke aliyeamini, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapokata shauri, wawe na hiari katika shauri lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hakika amepotea upotevu ulio wazi".
Shia wanaamini kwamba maadamu Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe kwa amri ya Mwenyezi Mungu alimteua Imam Ali (a.s) kuwa Khalifa, Waislamu hawana hiari yoyote isipokuwa kutii amri hii.
MITUME NA MAIMAMU HUTEULIWA NA MWENYEZI MUNGU TU NA SI VINGINEVYO
Shia wanaamini kuwa ni Mwenyezi Mungu (Allah) tu ndiye anayeweza kumteua mrithi wa Mtume na Imam wa Waislamu, na kwamba Ummah wa Kiislamu hauna hiari yoyote katika jambo hili.
USHAHIDI KUTOKA KATIKA QUR'AN
Aya za Qur'an zifuatazo zina thibitisha kuwa Mitume wote na Maimamu waliteuliwa na Allah Mwenyewe.
1) "Na Mola wako huumba atakavyo na huchagua; Hawana hiari ya kuchagua". (Qasas 28:68)
2) "Mimi nitaleta khalifa katika ardhi". (Baqara 3:30)
3) "Ewe Daud! Hakika tumekujaalia kuwa khalifa katika ardhi…… ".
(Saad 38 :26)
4) "(Allah) alisema kwa hakika nitakufanya wewe (Ibrahimu ) kuwa Imam wa watu (Ibrahimu); alisema Je, na katika kizazi changu pia? Akasema (Ndio lakini) ahadi yangu haitawafikia waovu (madhalimu)". (Baqara 2:124)
5) "Na tukawajaalia kuwa Maimamu wanaoongoza kwa amri Yetu".
(Anbiya 21:73)
6) "Na Unifanyie Waziri (msaidizi) katika jamaa zangu ........... ndugu yangu Haruni .......... Mwenyezi Mungu Akasema: Hakika umepewa maombi yako, ewe Musa".
(Taha 20: 29 - 36)
7) "Na hakika Mwenyezi Mungu alimchagua Adamu na Nuhu na kizazi cha Ibrahimu na kizazi cha Imrani juu ya walimwengu wote. Ni kizazi cha wao kwa wao; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenyekujua".
(Ale Imran 3:33 - 34).
8) "Mwenyezi Mungu amemchagua (Taluti) juu yenu na amemzidishia wasaa wa elimu na kiwiliwili, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mwenye kujua". (Baqara 2:247)
9) "Akasema (Allah) : Ewe Musa! Mimi nimekuchagua juu ya watu wote kwa ujumbe wangu na kwa kusema nawe kwangu, basi pokea haya niliyokupa na uwe miongoni mwa wanao shukuru". (A'raaf 7:144)
10) "Na tukawafanya miongoni mwao Maimamu wanaoongoza kwa amri yetu, waliposubiri na walikuwa wakiyakinisha aya zetu". (Sajdah 32: 24).
Aya zote za Qur'an zilizotajwa hapo juu na nyingine nyingi ambazo hatukuzitaja zinathibitisha kwamba Mitume wote na warithi wao waliteuliwa moja kwa moja na Mwenyezi Mungu bila hiari ya Ummah.
USHAHIDI / UTHIBITISHO WA KIAKILI NA KIHISTORIA
1) Ada Ya Mitume Waliotangulia: Ada ya Mitume wote ilikuwa ni kuteua warithi wao kwa amri ya Allah bila kuingiliwa na Ummah. Historia ya Mitume hawa haitoi mfano hata mmoja wa mrithi wa Mitume aliyechaguliwa kwa kura za wafuasi wake. Hakuna sababu kwa nini linapokuja suala la mrithi wa Mtume wa Mwisho, Muhammad (s.a.w.w.) sheria na kanuni hii ya Mwenyezi Mungu ibadilishwe.
Mwenyezi Mungu anasema: "Wala hutapata mabadiliko katika kawaida ya Mwenyezi Mungu (Mwendo Wake)". (Ahzab 33: 62)
2) Mifano Wa Warithi Wa Mitume Waliopita: Baadhi ya mifano ya warithi wa mitume walioteuliwa na Mitume waliopita kwa amri ya Mwenyezi Mungu (s.w.t).
a) Nabii Adamu alimteua Shiith
b) Nabii Ibrahim alimteua Ismail
c) Nabii Ya'qub alimteua Yusuf
d) Nabii Musa alimteua Yusho' bin Nuun
e) Nabii Issa alimteua Sham'uun
f) Nabii Muhammad (s.a.w.w.) alimteua Imam Ali Ibn Abi Talib
Qur'an inasema: "Na wakumbuke waja wetu Ibrahim na Is-haq na Ya'qkub waliokuwa wenye nguvu na busara. Hakika sisi tuliwachagua kwa lile jambo zuri kabisa la kuikumbuka Akhera. Na bila shaka walikuwa mbele yetu ni miongoni wa watu bora waliochaguliwa. Na mkumbuke Ismaili na Al-Yasaa na Dhulkifli; na hao wote walikwa miongoni mwa watu bora". (Saad 38:45 - 48).
Qur'an inasema: "Na hizi ndizo hoja zetu tulizompa Ibrahim juu ya watu wake. Tunamnyanyua katika vyeo yule tumtakaye. Hakika mola wako ndiye Mwenye hikima na ndiye ajuaye, Na tukampa (Ibrahim) Is-haq na Ya'quub, wote tukawaongoa. Na Nuhu tulimwongoa zamani. Na katika kizazi chake Daudi na Suleimani na Ayyub na Yusuf na Musa na Haruni. Na hivi ndivyo tuwalipavyo wafanyao mema. Na tukamwongoza Zakaria na Yahya na Issa na Ilyasi wote (walikuwa) miongoni mwa watu wema. Na (tukamwongoza) Ismail na Al-Yasaa (Ilisha) na Yunusi na Luti. Na wote tukawafadhilisha juu ya walimwengu. Na (tukawaongoa) baadhi ya baba zao na vizazi vyao na ndugu zao. Na tukawachagua na kuwaongoza katika njia iliyonyooka. Huu ni uongozi wa Mwenyezi Mungu. Kwa huo humwongoza amtakaye katika watu wake". (An-aam 6:83 - 88).
3) Mtume Hakufariki Kabla Ya Kumteua Mrithi Wake (Wasii Wake): Mitume wote waliopita pamoja na Mtume Muhammad (s.a.w.w.) hawakupata kuziacha Ummah zao japo kwa muda mfupi bila kuacha watu watakaoshika mahala pao (warithi). Hata walipokuwa wanatoka kwa safari fupi walikuwa wanaacha watu wa kushika mahala pao (warithi). Je, inawezekana kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) kuondoka na kuuacha Ummah wake bila Wasiy (Mrithi).
Mtume Muhammad alikuwa anajua kuwa muda wake wa kuondoka duniani umekaribia, alijua kuwepo kwa wanafiki katika jamii ya waislam, alijua kuwepo kwa watu walioendekeza tamaa ya madaraka katika mioyo yao, hivyo asingeweza kuuacha Ummah wake bila wasii (mtu atakayeshika mahala pake). Alimteua Imam Ali bin Abitalib kwa amri ya Mwenyezi Mungu kuwa mrithi na mtu atakayeshika mahala pake baada ya kuondoka kwake hapa Duniani.
4) Sababu zinazofanya ulazima wa Mitume kuteuliwa na Mwenyezi Mungu ni hizo hizo zinazofanya ulazima wa Wasii, Imamu na Khalifa kuteuliwa na Mwenyezi Mungu kwa sababu wote wanateuliwa kufanya kazi za Allah.
5) Ikiwa Imam au Khalifa atateuliwa au kuchaguliwa na watu, utii wake wa kwanza hautakuwa kwa Mwenyezi Mungu bali kwa watu waliomchagua. Kwa sababu msingi wa mamlaka yake itakuwa ni watu, mara zote atajaribu kuwaridhisha watu, vinginevyo ikiwa watapoteza imani juu yake, atapoteza nafasi yake. Mtu wa aina hii hataweza kutekeleza majukumu ya dini bila woga au upendeleo, na macho yake daima yatakuwa katika mtazamo wa kisiasa.
6) Historia ya Uislamu ina mifano tele ya maovu yaliyofanywa na makhalifa walioteuliwa na wanadamu. Mfano bora kabisa ni ule wa Yazid bin Muawiya bin Abu Sufiyan ambaye waziwazi kabisa alizipuuza sheria, alikunywa pombe kweupe, alimuua mjukuu wa Mtume Imam Husayn (a.s) na alituma jeshi Makka ambalo liliichoma nyumba tukufu ya Al-Ka'aba na kufanya maovu mengine mengi. (Tazama Taarikhul Khulafaa na Suyuti).
7) Pia ni Mwenyezi Mungu tu ndiye anayejua hisia na mawazo ya ndani ya wanaadamu, hakuna mwingine anayeweza kujua undani wa mtu mwingine. Wakati fulani anaweza kujifanya ni mcha Mungu na mwenye kumuogopa Mwenyezi Mungu ili tu kuwaonyesha wenzake au ili apate umaarufu ili achaguliwe na wenzake kuwa kiongozi kwa manufaa ya kiulimwengu.
Mifano ya aina hii si haba katika historia. Tuchukue mfano wa Khalifa Abdul Malik bin Marwan ambaye alikuwa anamaliza siku nzima msikitini akisali na kusoma Qur'an. Siku moja aliarifiwa juu ya kifo cha baba yake na kwamba watu walikuwa wanamsubiri ili watoe kiapo cha utii kwake. Aliifunika Qur'an na kusema : "Huku ndio kuachana kwangu mimi na wewe (Qur'an)". (Yaani kupata Ukhalifa ndio mwisho wa kusoma Qur'an). (Tazama Taarikhul Khulafaa ya Suyuti, Ukurasa 217). Sifa muhimu za Imam ni Mwenyezi Mungu tu ndiye anayezijua.
8) Ma'asum - Kwa mujibu wa Shia, Maimamu na Makhalifa lazima wawe Ma'asum - yaani waliotakasika kutokana na madhambi na uchafu. Hivyo Maimamu wote 12 walioteuliwa na Mtume Muhammad (s.a.w.w.)walikuwa Ma'asum (wasio na madhambi), na historia ya Uislamu inashuhudia uma'asumu, ucha Mungu, elimu na tabia njema za Maimamu 12 wa Shia Ithna Ashariyah, wa kwanza wao akiwa Imam Ali bin Abitalib (a.s). Mada hii itajadili zaidi katika makala yajayo.
Ismah (kutakasika kutokana na madhambi ) ni sifa kutoka kwa Mungu ambayo haiwezi kupatikana kwa jitihada ya mtu tu bila ridhaa ya Allah, hivyo Maimamu wanatakiwa wateuliwe na Allah tu. Sababu zote zinazothibitisha kuwa Mitume lazima wawe Ma'asum pia hizo hizo zinathibitisha kuwa Maimamu ni Ma'asum. Maelezo zaidi yatafuatia.
9) Miujiza - Kwa mujibu wa Shia, Maimamu walioteuliwa na Allah lazima wawe na uwezo kutoka kwa Allah wa kuonyesha miujiza kila itakapohitajika ili kuthibisha Uimamu wao kama walivyokuwa wakifanya Mitume. Historia ya Uislamu inathibitisha tena kuwa Maimamu 12 walioteuliwa na Allah walionyesha miujiza na waliwashinda maadui zao katika swala la ukweli (haki). Makhalifa walioteuliwa na watu huwa hawana uwezo wa kuonyesha miujiza, jambo ambalo ni muhimu sana kwa Mitume na Maimamu.
10) Ubora - Shia wanaamini kuwa, kama ilivyo kwa Mtume, Imamu lazima awazidi wale wote anaowaongoza katika sifa bora kama vile elimu, Ushujaa, Ujasiri, Ucha Mungu, na Ukarimu. Lazima awe na elimu kamili ya sheria za Mwenyezi Mungu. Hapa pia, sifa hizi hazipatikani kwa Khalifa yeyote aliyechaguliwa au kuteuliwa na watu isipokuwa kwa Maimamu 12 wa Shia Ithna Ashariya walioteuliwa na Allah. Soma makala yatakayofuata kwa maelezo zaidi.
Pointi zote hizi zinathibitisha waziwazi kuwa warithi, Makhalifa na Maimamu wa Mitume wote lazima wateuliwe na Allah tu. Maovu yote, kutokuwepo kwa Umoja, Ujinga, Uvunjaji wa sheria za kiislamu n.k. yote haya yanatokana na makhalifa waliochaguliwa na watu waliopinga amri ya Allah kupitia kwa Mitume wake kuhusiana na suala la ukhalifa.
Ili kupata uokovu, ukweli na utukufu waislamu wanatakiwa warudi na kufuata amri ya Allah (s.w.t) kuhusiana na suala la Imam baada ya Mtume, tunawaita katika ukweli na haki. Lakini ni lini Mtume Muhammad (s.a.w.w.) alimteua Imam Ali bin Abi Talib (a.s) kuwa Khalifa na Imam? Je, kuna ushahidi wowote katika Qur'an tukufu, Sunnah na historia ya Uislamu unaothibitisha uteuzi huu?
Ili kupata majibu ya maswali haya soma makala Na. 2.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini