Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

WITO KWA WAISLAMU KUUENDEA UKWELI (SEHEMU YA TATU)

1 Voti 03.0 / 5

WITO KWA WAISLAMU KUUENDEA UKWELI (SEHEMU YA TATU)
MAKALA NO. 3: MTUME MUHAMMAD ALIMTEUA IMAM ALI KUWA KHALIFA BAADA YAKE
BISMIHI TA'ALA
"NA KATIKA HAYA IMEKUJIA HAKI NA MAUIDHA NA UKUMBUSHO KWA WALE WANAOAMINI."(SURATUL HUD 11:120)

Katika makala yetu Na. 2, tulianza kutoa ushahidi kutoka katika Qur'an Tukufu na vitabu vinavyotambulika vya Ahlul Sunnah Wal Jama'ah kuthibitisha kuwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) alimteua Imam Ali bin Abitalib (a.s) kuwa Wasiy na Khalifa baada yake.

Aidha katika makala Na. 2, tulitoa uthibitisho wa aina tatu juu ya hilo, na ushahidi huo ni: (1) Hadithi Indhar au Da'wat Dhul Ashirah. (2) Aya ya Wilayah. (3) Hadithi ya Manzilah. Katika makala hii Na. 3 na zitakazofuatia, tutatoa ushahidi zaidi kuthibitisha Uimamu wa Ali bin Abitalib (a.s).
USHAHIDI NA. 4 - HADITHI YA THAQALAYN QURAN NA AHLUL BAYT

Katika Hadithi hii ya Thaqalain, Mtume Muhammad (s.a.w.w.) ameripotiwa akisema:
"Innii Taarikun Fiikum Al-Thaqalayn: Kitaballahi Wa Itratii Ahlu Baytii, Maa In Tamassaktum Bihimaa Lan Tadhillu Ba'dii Abadan".

"Ninawaachieni vitu viwili vizito, kitabu cha Mwenyezi Mungu (Qur'an Tukufu) na kizazi changu Ahlul Bayt, na ikiwa mtashikamana na hivi vitu viwili, basi kamwe hamtopotea".

Hadithi hii inathibitisha waziwazi kuwa, kabla ya kufariki, Mtume alituachia Ahlul Bayt kama viongozi wetu na Imam Ali (a.s) alikuwa ni kiongozi wa Ahlul Bayt baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.), hivyo Imam Ali ni Khalifa wa Waislamu baada ya Mtume.

Hadithi ya Thaqalayn imesimuliwa na vitabu vyote vikubwa vya Ahlul Sunnah Wal Jama'ah na ambayo inachukuliwa kuwa ni hadithi sahihi kabisa kuliko zote na Maulamaa wote wa Kisunni, peke yake tu ni ushahidi tosha na ni uthibitisho wenye uzito kabisa unaothibitisha Uimamu wa Ali bin Abitalib (a.s) baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.).

Imekubaliwa pia na maulama wa Kisunni kuwa hadithi hii imeelezwa na Mtume, sio mara moja bali katika maeneo na matukio mbalimbali kiasi kwamba hadithi hii imekuwa maarufu na imesimuliwa na mamia ya wanahadithi (wapokezi wa hadithi).

Katika moja ya matukio ambapo Mtume aliitoa hadithi hii ilikuwa ni katika viwanja vya Arafati wakati wa Hajjatul Widaa' (Hijja ya Mwisho ya Mtume), Siku ya Ghadir Khum - Mtume alipokuwa anarudi kutoka katika Hajjatul Widaa', katika siku zake za mwisho za ugonjwa wake, na katika khutba zake katika mji wa Madina, n.k.

Baadhi ya vitabu vikubwa vya Kisunni vilivyopokea hadithi hii ni hivi vifuatavyo:
1) Musnad Ahmad bin Hambal, Jz. 3, Uk.17

2) Sahihi Muslim, Juz. 2, Uk. 237.

3) Kanzul Ummal, Juz. 7, Uk. 112.

4) Sahihi Tirmidhi, Juz. 2, Uk. 308.

5) Mustadrak Al-Hakim, Juz. 3,Uk. 109.

6) Yanaabi ul Mawaddah, Uk. 25.

7) Tafsiir Ibn Kathiir, Juz. 3, Uk. 486.

8) Sawa'iq Al-Muhriqah, Uk. 150.

9) Taarikh Al-Ya'quubi, Juz. 2, Uk. 93

10) Dhakhair Al-Uqba cha Tabari, Uk. 16.

Na vitabu vingenevyo vingi ambavyo hatutavitaja hapa kwa sababu ya uchache wa nafasi.

Imam Suyuti amesimulia katika kitabu chake: Ihyaa'ul Mayyit, kwamba katika maradhi ya mwisho ya Mtume (s.a.w.w.), Mtume aliwahutubia sahaba zake kwa kusema: "Enyi watu, ninakaribia kuondoka duniani kwenda kuonana na Mola wangu Mtukufu, lakini kuweni makini, ninawaachia vitu viwili: Kitabu cha Allah na kizazi changu Ahlul Bayt". Kisha aliunyanyua na mkono wa Imam Ali (a.s) na kusema:

"Haadha Ali Ma'al Qur'an, Wal Qur'anu Ma'a Ali, Laa Yaftariqaani Hattaa Yaridaa Alayyal Hawdh." - "Huyu Ali yuko pamoja na Qur'an na Qur'an iko pamoja na Ali, na kamwe hawatoachana mpaka watakaponikuta katika chemchem (Hawdhi) za Kawthar".

Mtume alituachia Qur'an na Ahlul Bayt ili tuvishikilie vitu hivi viwili kwa nguvu, ili tusipotee na tumkute Mtume Peponi katika chemchem za Kawthar kwa mafanikio. Lakini kwa bahati mbaya baada ya kifo cha Mtume, watu waliwapuuza Ahlul Bayt na wakaiepuka njia iliyonyooka. Najiuliza nini litakuwa jibu lao watakapo kutana na Mtume siku ya Hukumu? Mtume ameiita Qur'an na Ahlul Bayt kama ‘Thaqalayn’ (Vitu viwili muhimu na vizito) lakini watu wamevichukulia kiuepesi tu. Tunamuomba Allah atuepushe kutokana na upotovu na dhulma dhidi ya Ahlul Bayt. Amin.

Na la kushangaza zaidi ni ukweli kwamba ingawa Hadithi hii ya Thaqalayn ipo katika vitabu vyote vya Kisunni vinavyo tambuliwa, lakini bado baadhi ya Maulama wa Kisunni wanajaribu kuuficha kwa sababu wanazozijua wenyewe au ili kuwadanganya wafuasi wao ambao hawajasoma vya kutosha, kuwa hadithi hii inapatikana katika vitabu vya Shia tu.

Kuna kipindi niliwahi kualikwa ili nitoe mada / hotuba juu ya umuhimu wa elimu katika moja ya misikiti ya Sunni, Dodoma. Ili kuonyesha elimu walivyokuwa nayo Ahlul Bayt, niliitoa Hadithi ya Thaqalayn katika hotuba yangu. Baada ya Majlis (Mkutano), ndugu yetu mmoja Mwislamu Sunni alialikwa kufunga kikao kwa dua. Yule ndugu yetu alijifanya kuwa ni mwanazuoni mkubwa na Ahlul Sunnah na badala ya kufunga kikao tu kwa dua' kama alivyotakiwa kufanya, aliuonyesha wazi ujinga wake / kutokujua kwake na alionyesha uadui wake dhidi ya wafuasi wa Ahlul Bayt, kabla ya dua alisema: "Hadithi ya Thaqalayn, vitu vizito viwili: Qur'an na Ahlul Bayt haipo kabisa katika vitabu vya Kisunni na hadithi hii sio sahihi". Uongo gani mkubwa huu dhidi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake!

Baadaye, baada ya kikao nilimfuata na kumwambia kuwa nina vitabu vingi vikubwa vya Kisunni kama Sahihi Muslim, Musnad Ahmad, Riyadhus Swaliheen, n.k. ambamo hadithi imepokelewa na kuandikwa, na nilimwalika aje kwangu ili nimpe ushahidi, lakini hakuthubutu kutokea. Nilitoa vivuli (photocopy) vya kurasa za vitabu hivi ambamo hadithi imetajwa na nikamtumia, lakini hakujibu wala hakuonyesha kujuta kwa kitendo chake cha kuikana hadithi ambayo ipo katika vitabu vyake. Tunamuomba Mwenyezi Mungu amuongoze katika njia iliyonyooka - Amin.
AHLUL BAIT NI AKINA NANI?

Swali muhimu kabisa ambalo tungependa kulijibu sasa ni Ahlul Bait ni akina nani? Au Ahlul Bait ni wepi? Hapa pia tutatoa majibu kutoka katika vitabu vya Sunni tu.

1) Muslim anasimulia katika Sahihi yake kutoka kwa Safiya bint Shaibah ambaye aliripoti kuwa: "Siku moja Aisha bint Abubakar alisema: "Siku moja Mtume wa Allah alikuwa amejifunika Kisaa (blanket kubwa), kisha akaja Imam Hasan (a.s) na Mtume akamuita na kumfunika na Kisaa. Kisha akaja Imam Husayn (a.s) na pia Mtume akamfunika. Kisha akaja Fatima (a.s) na Mtume akamfunika kwa Kisaa. Kisha akaja Imam Ali (a.s) na Mtume pia akamfunika kwa Kisaa. Kisha akasema:

"Innamaa Yuriidullahu Liyudh'hiba Ankumur Rijsa Ahlal Bayti, Wa Yutahhirakum Tat-hiira". - "Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu enyi Ahlul Bayt na anataka kukutakaseni utakaso ulio bora kabisa". (Suratul Ahzab 33:33).

Hadithi hii inaonyesha waziwazi kuwa Ali, Fatima, Hasan na Husayn ndio Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) ambao wameteuliwa na Mtume kuwa viongozi wetu. (Angalia Sahih Muslim, Jz. 5, Uk. 287).

2) Katika Sahihi Muslim imeripotiwa kuwa: "Aya ifuatayo iliposhuka: "Na atakayebishana nawe baada ya kukujia elimu, mwambie: Tuwaite watoto wetu na watoto wenu, wanawake wetu na wanawake wenu, na nafsi zetu na nafsi zenu, na kisha tuombe kwa unyenyekevu laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo (Aya ya Mubahilah, Aali Imran 3:61); Mtume aliwaiita Ali, Fatima, Hasan, Na Husayn na akasema: "Allahumaa Haa'ulaai Ahlii" - Ewe Mwenyezi hawa ndio watu wa nyumbani kwangu, Ahlul Bayt". (Tazama Sahih Muslim, Jz. 5, Uk. 268).

3) Ingawa Mtume alieleza mara nyingi kuwa Ahlul Bayt ni Ali, Fatima, Hasan, na Husayn; na hii imerekodiwa katika vitabu vingi vya Kisunni na wapokeaji thabiti, lakini utakuta baadhi ya wanazuoni wa Kisunni wanajaribu kung'ang'aniza kuwa Ahlul Bayt ni wake za Mtume.

Ukweli ni kwamba wake za Mtume hawamo katika kundi la Ahlul Bayt, kwa sababu Ahlul Bayt kwa mujibu wa Qur'an ni Ma'asumu (hawana madhambi) na walikuwa wametakasika ambapo wake za Mtume hawakuwa Ma'asumu. Mjadala juu ya mada hii utajadiliwa baadaye. Kwa wale wanaoamini kuwa wake za Mtume ni katika Ahlul Bayt wasome hadithi ifuatayo katika Sahih Muslim, Juz.5, Uk. 274.

Muslim amesimulia katika Sahih yake kupitia kwa Zaid bin Arqam ambaye alisema kuwa: "Mtume Muhammad (s.a.w.w.) amesema: "Enyi watu! jueni kwamba mimi ni mwanaadamu na Malaika wa Mauti anaweza kunijia hata mimi pia na lazima niitike wito wake. Enyi watu! ninawaachieni vitu vizito (muhimu) viwili; cha kwanza ni kitabu cha Mwenyezi Mungu, ambapo ndani yake mtapata mwongozo na nuru, hivyo shikamaneni na kitabu cha Mwenyezi Mungu na kamwe msikiache; na kizito cha pili ni Ahlul Bayt wangu, ninawakumbusheni juu ya wajibu wenu kwa Ahlul Bayt --- ninawakumbusheni juu ya wajibu wenu kwa Ahlul Bayt ---- ninawakumbusheni juu ya wajibu wenu kwa Ahlul Bayt (alirudia mara tatu)".

Kisha tuliuliza: "Ahlul Bayt ni akina nani, Je, wake?" Akasema: "Hapana. Ninaapa kwa jina la Allah, kwa hakika mwanamke huishi na mumewe kwa muda, kisha mumewe akimpa talaka, hurudi kwa baba yake na jamii yake, Ahlul Bayt ni watu wake kutoka katika familia yake na ambao kwao sadaka ni haramu baada yake". (Sahih Muslim, Baab Fadhail Ali (a.s), Juz. 5, Uk. 274).

4) Katika Sahih Tirmidhi imeripotiwa kutoka kwa Umru bin Abi Salama ambaye amesema: "Aya hii iliposhuka: "Innama Yuridullahu Liyudh Hiba Ankumur Rijsa Ahlal Bayti Wa Yutahhirukum Tat-Hiira" - "Kwa hakika, Mwenyezi Mungu anataka kuwaondeleeni kila aina ya uchafu, enyi Ahlul Bayt, na kuwatakasani kwa utakaso ulio bora kabisa (33:33)", katika nyumba ya Ummu Salma, Mke wa Mtume; Mtume aliwaita Fatima, Hasan, Husayn na Ali na aliwafunika kwa Kisaa (blanketi); kisha akasema : "Ee Mwenyezi Mungu! hawa ni Ahlul Bayt wangu, hivyo waondolee kila aina ya uchafu na watwaharishe kwa tohara iliyo bora kabisa".

Ummu Salma akasema: "Je, na mimi ni pamoja nao (Ahlul Bait) Ewe Mtume wa Allah?" Mtume alijibu: "Hapana, wewe una nafasi yako na upo katika njia iliyonyooka". Alikataliwa kuingia! Hadithi hii pia imo katika Musnad Ahmad bin Hambal (Juz 6, Uk. 306), na Sahih Tirmidhi (Juz. 2, Uk. 209).

5) Katika aya ya Tathiir: "Innamaa Yuridullahu Liyudh-Hiba Ankumur-Rijsa Ahlal Bayti Wa Yutahhirakum Tat-Hiira (Ahzab 33:33), dhamiri ya Kiarabu iliyotumika kwa Ahlul Bayt ni "Ankum......, Yutahhirukum....". Wakati katika sura hiyo hiyo katika aya zilizotangulia (Ahzab 33:32-34) dhamiri iliyotumika kwa wake za Mtume ni "Kuntunnaa....., Minkunna......., n.k." ambayo ni dhamiri ya kike kwa kiarabu.

Badiliko hili la ghafla la dhamiri kutoka dhamiri ya kike kwenda dhamiri ya kiume katika Aya (Ahzab 33:33), inathibitisha kuwa wake za Mtume hawamo katika Ahlul Bayt ambao wanatakiwa kufuatwa, kwa sababu wakati Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alipotaka kuwazungumzia wake za Mtume alitumia dhamiri ya kike "Kuntunna ....., Minkunna......", lakini alipoanza kuwazungumzia Ahlul Bayt "Ali, Fatima, Hasan na Husayn", dhamiri ilibadilika. Huu ni ushindi dhahiri kwa wale wanaojua sarufi ya lugha ya Kiarabu.

Wapendwa wasomaji, mmeona kwamba hadithi ya Thaqalayn (vizito viwili) : Qur'an na Ahlul Bayt imeripotiwa katika vitabu vingi sana vya Kisunni, lakini umewahi kumsikia mwanazuoni wa Kissuni akiizungumzia hadithi hii - Kushikamana na Qur'an na Ahlul Bayt - ambao ndio ulikuwa wasiyya wa mwisho wa Mtume. Kwanini wanazuoni wa Kisunni wanaupuuza wosia wa mpendwa kiongozi na Mtume wetu? Je, kuna sababu yoyote ya maana ya kuupuza wosia huu (jambo ambalo ni dhambi kubwa) zaidi ya kuwa ni ujinga, ugumu wa mioyo, kujiegemeza upande wa imani zetu ulizonazo, wivu na manufaa yetu binafsi? Tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe tawfiiq ya kushikamana na Qur'an na Ahlul Bayt baada ya Mtume (s.a.w.w.) Amin.
USHAHIDI NA. 5 - HADITHI YA SAFINA / JAHAZI

Katika kitabu cha Kisunni: Mustadrak Sahihein imesimuliwa na Hakim kupitia kwa Hanash Al-Kanani ambaye alisema: Nimemsikia Abudhar Al-Ghafari akisema wakati alikuwa ameushika mlango wa Kaa'ba Tukufu: "Enyi watu, wale wanaojua mimi ni nani wananijua, lakini wale wasionijua na wajue kuwa mimi ni Abudhar (Sahaba wa Mtume). Nimemsikia Mtume (s.a.w.w.) akisema:

"Mathalu Ahlulbaytii Fiikum Mathali Safiinatin Nuuh, Man Rakibaha Najaa, Wa Man Takhallafa Anha Gharika". - "Mfano wa Ahlul Bayt wangu ni kama Safina / Jahazi ya Nuuh (a.s). Kila aliyeipanda aliokoka, na kila aliyejiepusha nayo aligharikishwa". Mwanachuoni wa Kisunni Hakim amesema kwamba hadithi hii ni Sahihi.

Pia hadithi hii ya Safina imesimuliwa na mamia ya wanazuoni wa Kisunni katika vitabu vyao. Umewahi kumsikia mwanazuoni yeyote wa Kisunni akiizungumzia hadithi hii kwenye hotuba yake? Kama hujawahi, basi wanazuoni hao wanaificha. Lakini unaweza kurejea vitabu vifuatavyo vya Kisunni na utaipata hadithi hii:

• Al-Hakim katika Mustadrak yake, Juz. 2, Uk. 343.

• Sawaiq Muhriqah, Uk. 153.

• Faraid Simtein, Juz.4,Uk. 149.

• Mustadrak Sahihein, Juz.3, Uk. 343.

• Nuural Absaar, Uk. 126; na vitabu vingine vingi.

Waislamu waliotaka kunusurika na moto wa Jahannamu siku ya Kiyama waliwafuata AhlulBayt - Imam Ali (a.s), baada ya kuondoka kwa Mtume. Ni sababu gani inayotufanya tusiwafuate Ahlul Bayt baada ya Mtume na hali ya kuwa Ahlul Bayt ni safina ya Nuuh (a.s)?

Kwa hakika, hatutaki kuwa kama mtoto wa Nuuh (a.s) ambaye juu yake Qur'an inasema:

" ---- na Nuuh alimwita mwanae, na alikuwa peke yake. Ewe mwanangu! ingia (ndani ya Safina) uwe pamoja nasi na usiwe miongoni mwa makafiri (wasio amini). Alisema nitakimbilia mlimani, mlima ambao utanilinda dhidi ya maji. Nuuh akasema hakuna mlinzi leo atakayekulinda dhidi ya adhabu ya Mwenyezi Mungu isipokuwa yule mwenyewe kurehemewa. Kisha wimbi likapita kati yao, hivyo akawa ni miongoni mwa waliogharikishwa". (Huud 11:41-43).

Ni nani atakayetuokoa dhidi ya gharika ikiwa hatutoingia katika jahazi / safina ya Ahlul Bayt? Tunamuomba Allah (s.w.t) atunusuru na gharika tusiwe kama alivyokuwa mtoto wa Nuuh. Amin.
USHAHIDI NA. 6 - HADITHI NYINGINE JUU YA AHLUL BAYT

Kuna hadithi nyingi sana za Mtume Muhammad (s.a.w.w.) zinazoonyesha fadhail na uongozi wa Ahlul Bayt (a.s). Tutatoa hadithi chache hapa chini kutoka katika vitabu vya Kisunni ili kuthibitisha nafasi ya Ahlul Bayt baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.):

1) Ibn Abbas amesimulia kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.w.) kasema: "Nyota huwaongoza watu wa dunia ili wasiangamie. Hali kadhalika Ahlul Bayt wangu ni viongozi wa Ummah wangu watakaouepusha ummah wangu kutokana na utengano na kutofautiana (kuhitilafiana); na yeyote miongoni mwa makabila ya kiarabu atakayewapinga, atakuwa ni kutoka katika kundi la Iblis". (Mustadrak Sahihein, Juz .2, Uk. 343; Sawaiq Al-Muhriqah, Uk. 235).

Ingekuwa waqureishi walikubaliana juu ya Uimamu wa Ali bin Abitalib (a.s) na wangekuwa hawakumpinga Mtume (s.a.w.w.) juu ya suala hili, Ummah wa Kiislamu ungekuwa umeepukana na Utengano na Khitilafu. Lakini kwa bahati mbaya ukhalifa wa Ali (a.s) ulinyang'anywa, na Ahlul Bayt walipingwa.

2) Jinsi ya Kumsalia Mtume (s.a.w.w.) - Salawat - Mtume Muhammad (s.a.w.w.) amewaelekeza waislamu kuwajumuisha Ahlul Bayt wake (Aali Muhammad) wakati wa kumtumia salawat, na hairuhusiwi kuiondoa Aali Muhammad kwenye Salawat.

Kwenye Sahih Bukhari, imetajwa kwamba siku moja masahaba walimuuliza Mtume Muhammad (s.a.w.w.): "Ewe Mtume wa Allah, tumeelewa jinsi ya kukusalimia, lakini tufundishe jinsi ya kukutumia salawat (kumsalia Mtume)". Alijibu: "Semeni Allahumma Swalli Alaa Muhammad Wa Alaa Aali Muhammad, Kama Swallayta Alaa Ibrahim Wa Alaa Aali Ibrahim, Innaka Hamidun Majid. (Sahihi Bukhari, Juz.8, Uk. 245).

Swali hili liliulizwa na masahaba baada ya amri ya salawat kuteremka katika Qur'an: "Innallaha Wa Malaaikatahu Yusalluna Alan Nabii. Yaa Ayyuhal Ladhiina Aamanu Swallu Alaihi Wa Sallimu Tasliima" - "Kwa hakika Mwenyezi Mungu na malaika wake wanamtakia rehema Mtume. Enyi mlioamini! Mtakieni rehema Mtume na msalieni". (Ahzab 33:56).

Maulamaa wa Kisunni na wa Kishia wamekubaliana kuwa aya hii ilishuka kwa ajili ya fadhail za Mtume na Ahlul bayt wake. Rejea vitabu vifuatavyo vya Kisunni:

1- Asbabun Nuzul cha Wahidi,Uk. 271.

2- Al-Mustadrak cha Hakim, Juz. 3, Uk. 148.

3- Tafsiir Fakhruddin Raazi, Juz. 25, Uk. 226.

4- Riyadhu Swalihun cha Nawawi, Uk. 4555

5- Jami' Li Ahkamil Qur'an cha Qurtubi, Juz.14, Uk. 233-34.

Imesimuliwa katika Sawaiq Al-Muhriqah cha mwanazuoni wa Kisunni Ibn Hajar (Uk. 144) kwamba: Mtume Muhammad (s.a.w.w.) alisema: "Msiifupishe salawat (salawat Al-Bataraa)". Baada ya kuulizwa nini itakuwa ufupisho wa salawat? Mtume (s.a.w.w.) alijibu: "Mnaposema : Allahuma swalli alaa Muhammad - na mkaishia hapa, hii haitosihi, lazima mseme: Allahumma swalli alaa Muhammad wa Aali Muhammad."

Kwa bahati mbaya ndugu zetu wa Kisunni wanapotuma salawat, wanajiepusha kusema Aali Muhammad, hivyo wanatoa salawat isiyotimia na wanakhalifu maelekezo ya Mtume. Kwa mfano katika mawaidha au majlis, wasikilizaji wa Kisunni, kwa kawaida wanaposikia jina la Mtume humtumia salawat isiyokamili kwa kusema Allahumma Swalli Wa Sallim Alaihi, bila kusema Wa Aalihi. Hata maulamaa wa Kisunni wanapoandika jina la Mtume wanaandika salawat isiyotimia Swallallahu Alaihi Wassallim; wanaondoa "Wa Aalihi". Je, ni ujinga au wivu, au kujiegeamiza upande wao / kujipendelea hata kama sio sahihi au nini, nashangaa?

Katika hadithi nyingine, Mtume Muhammad (s.a.w.w.) alisema: "Yeyote atakaye sali sala na ndani ya sala yake asinisalie mimi na Ahlulbayt wangu, sala yake haitokubaliwa". (Tazama : Shifaa ya Qaadhi Ayadh Maghrabi Juz. 2, Uk. 55; Sawaiq Al-Muhriqa cha Ibn Hajar Uk. 139).

Mwanachuoni wa Kisunni Raazi katika Tafsiri yake (Juz.7, Uk. 391) ametaja Ahlulbayt ni sawa na Mtume katika mambo matano: (1) Salawat (2) Salamu (3) Tahara yaani Ismah (4) Sadaka kwao ni haramu (5) Kuwapenda ni wajibu.

Imam Shafii amesema katika shairi lake maarufu kuwasifu Ahlulbayt: "Ahlulbayt wa Mtume, kuwapenda nyinyi ni wajibu kwa kila mwislamu kama ilivyofunuliwa kwenye Qur'an. Hii ni fadhail kubwa sana kiasi kwamba kwa yeyote ambaye hatowatumia salawat, sala yake inakuwa batili".

3) Aya ya Mawaddah - "Qul Laa As'alukum Alaihi Ajran Illal Mawaddata Fil Qurba". - "Sema siwaombi ujira isipokuwa kuwapenda jamaa zangu wa karibu". (Shura 42:23).

Tafsiri zote na vitabu vya hadithi kwa pamoja vinasema kuwa Ahlulbayt na Qurba hapa ni Ali, Fatima, Hasan na Husayn, na kuwapenda ni wajibu kwa kila mwislamu kwa sababu iliposhuka aya hii Mtume aliulizwa: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni nani hao jamaa zako wa karibu (Qurba) ambao kuwapenda imekuwa ni wajibu kwa kila mwislamu? Mtume alijibu: "Ni Ali, Fatima na watoto wao wawili Hasan na Husayn".

Tazama :
1. Sahih Bukhari, Juz. 6, Uk. 129.
2. Tafsiir Tabari, Juz. 25, Uk. 14.
3. Tafsiir Al-Kasshaf, Juz. 3, Uk. 402.
4, Tafsiir Al-Waadhih , Juz. 25, Uk. 19.

Aya hii ya Mawaddah iliposhuka (42:23), baadhi ya watu walianza kuwaza akilini mwao kuwa Mtume anataka tuwapende Ahlulbayt wake kwa matakwa yake mwenyewe. Hivyo Jibril alikuja na kumwambia Mtume. Baadhi ya watu wanakulaumu kwa upendeleo. Hivyo aya hii ikashuka: "Je mnasema ameitunga Qur'an?" (Shura 42:24).

Alhamdulillah, sisi Shia Ithna Ashariyah tunawapenda Ahlulbayt, na tunawapa nafasi wanayostahili, tunawafanyia Maulid kila mmoja wao, tunafurahia furaha zao na hatuzifurahii huzuni zao, na tunaamini kuwa wao ni viongozi wetu baada ya Mtume (s.a.w.w.). Tunawaita Waislamu wote kujiunga nasi katika kuwafuata Ahlulbayt baada ya Mtume.

Qur'an inasema katika aya hiyo hiyo ya Mawaddah : "Na yeyote atakayechuma wema (kwa kuwapenda Ahlulbayt) tutamzidishia wema, kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye shukrani (Shura 42:23). (Tafsiir Baghawi na Tafsiir Tha'labi). Soma makala Na. 4 kwa ushahidi zaidi juu ya Ukhalifa wa Imam Ali bin Abitalib (a.s).

Wa Billahi Tawfeeq.

MWISHO WA MSURURU WA MAKALA HIZI ZA: WITO KWA WAISLAMU KUUENDEA UKWELI

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini