Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

BIBI FATIMAH ZAHARA (A.S) 6

0 Voti 00.0 / 5

HISTORIA YA MASUMIN AS.

MA'ASUMAH WA PILI

BIBI FATIMAH ZAHARA (A.S)

Sehemu ya saba.

FATIMAH NI BIBI MBORA WA WANAWAKE WA ULIMWENGUNI

Fatimah Zahara as katika mwanzo wa kujenga jamii ya Kiislamu Madina alikuwa ni mdogo kwa umri, bado hajafikia miaka minane ila alikuwa anafaham na utambuzi wa elimu ya kiuchamungu, ya kidini na umaasumu kamili, kiasi kwamba alitekeleza jukumu muhimu katika ukuaji wa jamii Mpya ya Kiislamu, alisifika kwa ikhilasi yake, kufuatilia kwake Matukio na uelewa wake wa ujumbe wa mbinguni, pamoja na kuwepo wanawake wengine katika nyumba ya Mtukufu Mtume saww, lakini yeye alipata cheo cha juu kitukufu kwa Mwenyezi Mungu, ikhilasi yake na uvumilivu wake katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Alitekeleza majukumu aliyokuwa nayo kwa njia nzuri mno, hivyo akastahiki kuwa ni Bibi mbora wa wanawake wa ulimwengu kwa wa mwanzo na wa Mwisho. Katika hadithi iliyopokewa kutoka kwa Fadhili alisema :. Nilimwambia Abu Abdillah as nieleze juu ya kauli ya Mtukufu Mtume wa Mwenyezi Mungu kuwa yeye ni Bibi mbora wa wanawake, je, ni wa ulimwengu wake tu? Akasema : "Huyo ni Mariamu, yeye alikuwa ni Bibi mbora wa wanawake wa ulimwengu wake tu. Lakini Fatimah ni bibi mbora wa wanawake wa ulimwengu kwa waliotangulia, waliopo na wajao.

Hivyo Fatimah Zahara as amestahiki kwa kuwepo kwake ni sharti la kupatikana Mtume saww na Amirul Muuminina Aliy as kama ilivyo kuja katika hadithi al Quds, ambapo yeye alikuwa na jukumu la kukamilisha na kutimiza katika kujenga jamii ya Kiislamu, na kutimiza lengo la Kuumbwa wanadamu na Mtume Mtukufu, ambapo lau si Fatimah Maimamu wasingeumbwa kutoka katika kizazi cha Mtukufu Mtume wa Mwenyezi Mungu saww katika ulimwengu huu.

Na kukosekana kwa Maimamu ina maana ya kubatilika kuwepo kwa Nabii, na kubatilika kuwepo kwa Uislamu  kwa pamoja, na haya mawili kwa umuhimu wake yanasababisha kubatilika kuwepo wanadamu vile vile... Hivyo basi kama siyo Fatimah as kusingepatikana mwendelezo wa kazi ya Nabii na kuifanya idumu, hivyo yeye as ndio siri ya uimamu tukiongezea yaliyotangulia katika kusimama kwake dhidi ya njama ambazo zilitokea baada ya Nabii saww.

UKARIMU WA  BIBI FATIMAH (A.S)

Katika sifa zingine alizokuwa nazo Fatimah Zahara as na ambazo zinapasa Ziwe ni funzo katika jamii na ummah wowote unaotaka kuendelea ni zuhudi, Ukarimu, kutoa kwa wingi, subira na tabia nzuri iliyotukuka. Kisa cha kulisha chakula ambacho kimepokewa katika Qur-an tukufu katika suratud Dahri ni ushahidi mzuri juu ya hilo ambapo walitoa chakula chao pekee na ambacho ni vipande vya mikate tu kwa watu watatu, kwa siku tatu mfululizo wakabaki na njaa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Na hiyo ni Ibada ya kuweka nadhiri ya kufunga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu wakipona Hassan na Hussein as kutokana na maradhi waliyougua, walipokaa tayari kwa kufuturu mlango uligongwa na masikini, wakatoa vipande vya mikate yao kwa masikini na wakalala njaa, vivyo hivyo walifanya siku ya pili kumfanyia Yatima na katika siku ya tatu mambo yalijirudia kwa mfungwa wa kivita (mateka).

Hivyo Mwenyezi Mungu akateremsha sura kamili kwa ajili yao nayo ni suratud Dahri, na miongoni mwayo ni aya hii :

ويطعمون الطعام على حبه، مسكينا ويتيما وأسيرا

"Na wanawalisha chakula masikini, Yatima, na mateka hali ya kuwa wao wanakihitajia. Insaan :76:8.

MIONGONI MWA IBADA ZA FATIMAH ZAHARA  (a.s)

Vilevile Fatimah Zahara anamcha Mwenyezi Mungu kwa ikhilasi na imani ya juu ambapo moyo wake ulikuwa ni chemchem yenye kububujika kwa kumjua Mwenyezi Mungu na kufungamana naye. Amesema Imamu Hassan as "Nilimuona mama yangu hali akiwa amesimama kwenye mswala wake usiku wa ijumaa basi aliendelea kurukuu na kusujudu hadi yakakaribia mapambazuko ya asubuhi, na nilimsikia anawaombea waumini kwa Kuwataja majina yao na kuwaombea dua kwa wingi na wala haombei nafsi yake chochote.... Nikamwambia : "Ewe mama yangu kwa nini huombei nafsi yako kama unavyowaombea wengine?" Akasema : "Ewe mwanangu jirani kwanza kisha nyumbani."

Kutoka kwa Hassan Busuriy anasema :. Hakujawahi kutokea katika ummah huu mwenye kumuabudu (Mwenyezi Mungu) kumshinda Fatimah as alikuwa akisimama katika sala za usiku hadi miguu inafura.

Huyu ndiye bibi Fatimah as yeye kwa kila upande ni Shule.

Fuatana nami sehemu ya nane historia ya Maasumah Fatimah bint Muhammad saww.

Rejea:

 Ma'anil Akhbar UK 107.

Tafsir Ruhul Maani Jz 90 UK 157

Fatimah Zahara as fiyl Qur-an UK 313.

I'lalus Shara'u UK 181

Biharul anuwari Jz 43 UK 22.

Biharul anuwari Jz 43 UK 84.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini