Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

KUFUNGUA SAFARINI KWA MUJIBU WA KITABU NA SUNNA 2

0 Voti 00.0 / 5

KUFUNGUA SAFARINI KWA MUJIBU WA KITABU NA SUNNAH/HADITHI SAHIHI

Sehemu ya pili

Kwa kufuata Qur-ani Tukufu na Sunnah/Hadithi Sahihi mutawatiri wanavyuoni wameafikiana kuwa ni ruhusa kisheria kufungua safarini kwa hiyari au kwa wajibu, isipokuwa wametofautiana juu ya ulazima na ruhusa ya hiyari. Hii ni kama tofauti iliyopo kuhusu kupunguza swala; je ni ruhusa ya hiyari au ni lazima.

Shi'ah Imamiya Ithna Ashariyya kwa kuwafuata Maimamu wa Ahlubaiti Rasul, wao na Dhahiriya wamesema kuwa kufungua safarini ni lazima. Na Katika Maswahaba hiyo ndiyo kauli ya Abdur Rahman bin Auf, Umar bin Khatabi na mwanae Abdallah, Abu Huraira, Aisha na Ibn Abbasi.

Na kwa waliokuja baada ya Maswahaba (Tabi'ina) hiyo ni Kauli ya Imamu Ally bin Hussein bin Ally bin Abi Twalib as na mwanae Muhammad Al Baqir, Said Bin Musayyab, Atau, Ur'watu Bin Az-Zubairi, Shaabatu,Az-Zahriy, Al Qasim Bin Muhammad bin Abi Bakr na Yunus bin Ubaydu na wafuasi wake.

Wanavyuoni wa Fiqihi wa Ahlisuna/kisunni wakiwemo wa madhehebu nne wamesema kuwa kufungua safarini ni ruhusa ya hiyari, japokuwa wametofautiana kuhusu ni kipi bora kufungua au kufunga.

Al Jasasu amesema: "Swaumu safarini ni bora kuliko kufungua."

Maalik na At Thauriy wamesema: "Kufunga kunapendeza sana kwetu kwa mwenye nguvu ya kufunga."

Imamu Shafii amesema: "Akifunga safarini inatosheleza."

As-Sar'khasiyyu amesema: "Hakika kufunga safarini inaruhusiwa kwa Kauli ya wanavyuoni wa Fiqihi, na hii ndiyo kauli ya Maswahaba wengi, na kwa mujibu wa kauli ya watu wa dhahiri hairuhusiwi- mpaka akasema: "Hakika kufunga safarini ni bora kwetu kuliko kufungua."

Imamu Shafii amesema: "Kufungua safarini ni bora kwa sababu dhahiri ya hadithi tulizozipokea zinaonyesha kuwa kufunga safarini hairuhusiwi, hivyo hata kama dhahiri hii ikiachwa iruhusu funga basi itabaki kuwa kufungua safarini ni bora kuliko kufunga."

Akalinganisha na Swala, hakika kupunguza na kuishia rakaa mbili safarini ni bora kuliko kutimiza, na hivyo ndivyo Swaumu ilivyo kwa sababu safari inazibadili.

Mtukufu Mtume saww amesema: "Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu alimuondolea msafiri nusu ya swala na funga."

Ibn Qudamati Al Muqaddasiy amesema: "Hukumu ya msafiri ni hukumu ya mgonjwa anaruhusiwa kufungua na ni karaha kwake kufunga japokuwa Akifunga inatosheleza. Ruhusa ya kufungua imethibiti kwa maelezo ya (Hadithi au Aya) na Ijma'ai (makubaliano) na wanavyuoni wengi wamesema kuwa iwapo Akifunga inatosheleza- mpaka akasema: "Kufungua safarini ni bora kuliko kufunga.

Al Qurtubi amesema: "Wanavyuoni wametofautiana kuhusu ubora, ni kipi bora safarini, kufunga au kufungua. Maalik na Shafii katika baadhi ya yaliyopokewa toka kwao wamesema: "Swaumu ni bora kwa mwenye nguvu ya kufunga. Madhehebu ya Maalik na Shafii yamefanya kuwa ni hiyari, akasema Shafii na waliomfuata kuwa: Ni hiyari. Na wala hajaboresha, pia ndivyo ilivyo kwa Ibn Aliyatu."

Nukuu hizi na nyinginezo zinaweka wazi makubaliano ya wanavyuoni wote wa Fiqihi kuwa inaruhusiwa kufungua safarini na si ulazima wa kufungua japokuwa Shafii kakiri dhahiri ya dalili ni kuzuwia kufunga safarini akasema:

Kwa sababu dhahiri ya hadithi tulizozipokea zinaonyesha kuwa kufunga safarini hairuhusiwi.

Vyovyote vile ni kuwa kufungua ni kati ya hukumu za safari sawa iwe lazima au ruhusa ya hiyari. Muhimu ni kubainisha dalili zinazoonyesha kuwa kufungua ni lazima au ni ruhusa ya hiyari. Na itakubainikia kuwa kufungua ni lazima inayoonyeshwa na Kitabu na Sunnah/ Hadithi Sahihi.

Fuatana nami Sehemu ya tatu kuona Kitabu kinasemaje kuhusu saumu ya Ramadhani safarini baada ya kuona kauli za wanavyuoni wa Fiqihi.

REJEA:

Al Mahaliy ya Ibn Hazmi Andlusiy Jz 6 UK 258

Ahkamu l Qur-ani Jz 1 UK 215

Al Mabsutu ya Sarkhasiy Jz 3 UK 91-92

As- Sharhu Al Kabiir fi dhaylul Mughuniyi: Jz 3 UK 17-19

Al Jamiu liahkamil Qur-ani Jz 2 UK 280

Al Mabsutu ya Sarkhasiy Jz 3 UK 91.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini