Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

KUANGAMIZWA KWA WATU WA NABII SALEH A.S

1 Voti 04.0 / 5

BSMILAHI AR-RAHMANI AR-RAHIIMI

KUANGAMIZWA KWA WATU WA NABII SALEH A.S

Kaumu ya Nabii Saleh A.S. iliangamizwa kwa sababu ya kumuuwa ngamia wa Mwenyezi Mungu na ilhali kabla ya hapo Mtume wao aliwaonya kwa onyo kali la kushukiwa na adhabu ya haraka kabisa ikiwa watamuuwa yule ngamia jike. Ingawa walionywa kwa hilo onyo kali lakini hata hivyo watu wabaya hawakumsikia wala kumjali Mtume wao.

Siku ya Jumatano wakamfukuza yule ngamia wa Mwenyezi Mungu na alipopita karibu ya Masda`a akamrushia mshale, na alipofika karibu na kijana aliyeitwa Qaddaar bin Saalif akamuuwa ngamia kwa upanga kwa amri ya wenzake. Kisha wakamchinja wakagawana nyama yake wakaila. Lakini mtoto wa ngamia aliwahi kukimbilia jabalini, na inasemekana aliingia jabalini akapotea humo. Kama ilivyobainika katika Suratil Qamar aya ya 29, "

فَنَادَوْا صَاحِبَهُمْ فَتَعَاطَى فَعَقَرَ

Maana yake, "Basi wakamwita rafiki yao (Qaddaar naye kashika upanga) akamchinja (yule ngamia wa Mwenyezi Mungu wakamla)." Na pia Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Surat Sh-shams aya ya 14,

فَكَذَّبُوهُ فَعَقَرُوهَا فَدَمْدَمَ عَلَيْهِمْ رَبُّهُمْ بِذَنْبِهِمْ فَسَوَّاهَا

Maana yake, "Lakini walimkadhibisha (Mtume wao) na wakamchinja ngamia (wa Mwenyezi Mungu), kwa hivyo Mola wao aliwaangamiza kwa sababu ya dhambi zao na akawafuta kabisa (duniani)."

Basi khabari zile zilipomfikia Nabii Saleh aliwaambiya: "Nakutahadharisheni kukushukieni ile adhabu ya Mwenyezi Mungu niliyokuahidini kutoka mbinguni." Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Huud aya ya 65, "

فَعَقَرُوهَا فَقَالَ تَمَتَّعُوا فِي دَارِكُمْ ثَلاثَةَ أَيَّامٍ ذَلِكَ وَعْدٌ غَيْرُ مَكْذُوبٍ

Maana yake, "Wakamchinja. Basi (Nabii Saleh) akasema "Stareheni katika mji wenu ( huu, muda wa) siku tatu. Hiyo ni ahadi isiyokuwa ya uwongo." Baada ya kumuuwa yule ngamia wa Mwenyezi Mungu S.W.T. ambayo siku ile ilikuwa ni siku ya Jumatano, wakati wa usiku wake wale watu tisa wakaazimia na wakapanga mipango yao ya kutaka kumuuwa Mtume wao wakasema: Ikiwa kama kasema kweli kuwa itatujia adhabu basi sisi tumwahi kabla hatujawahiwa. Na ikiwa kama ni muongo tutakuwa tumemuuwa yeye na ngamia wake. Hivyo wakamwendea Nabii Saleh wakiifuata ile njia anayopitia wakati anapokwenda zake kusali Msikitini majira ya usiku, mara tu walipomkaribia, Mwenyezi Mungu S.W.T. akawarushia mawe wakafa wote kwa pamoja na vile vitimbi vyao vikenda patupu. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratin Naml kuanzia aya ya 49 hadi 51, "

قَالُوا تَقَاسَمُوا بِاللَّهِ لَنُبَيِّتَنَّهُ وَأَهْلَهُ ثُمَّ لَنَقُولَنَّ لِوَلِيِّهِ مَا شَهِدْنَا مَهْلِكَ أَهْلِهِ وَإِنَّا لَصَادِقُونَ * وَمَكَرُوا مَكْرًا وَمَكَرْنَا مَكْرًا وَهُمْ لا يَشْعُرُونَ * فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ مَكْرِهِمْ أَنَّا دَمَّرْنَاهُمْ وَقَوْمَهُمْ أَجْمَعِينَ

Maana yake, ""(Wale watu tisa) wakasema: "Apishaneni kwa Mwenyezi Mungu (ya kwamba) tutamshambulia usiku yeye (Saleh) na ahli zake, kisha tutamwambia mrithi wake: "Sisi hatukuona maangamizo (yake wala) ya watu wake na sisi bila shaka tunasema kweli. Basi wakapanga mipango yao, na Sisi tukapanga mipango yetu (tukapangua vitimbi vyao) na wao hawatambui. Basi angalia ulivyokuwa mwisho wa vitimbi vyao, tuliwaangamiza pamoja na watu wao wote."

Ilipofika siku ya kwanza asubuhi ambayo ndio ilikuwa ni siku ya Alkhamisi, na ndio siku ambayo waliahidiwa na Nabii Saleh kushukiwa na ile adhabu, mara nyuso zao zikabadilika rangi ya manjano, na siku ya pili ambayo ilikuwa ni siku ya Ijumaa nyuso zao zikawa na rangi nyekundu. Na siku ya tatu ambayo ilikuwa ni siku ya Jumammosi nyuso zao zikawa na rangi nyeusi, hata ikapita mchana wakafikiri kwamba wameokoka na ile adhabu.

Lakini wapi! Ilipowapambazukia asubuhi ya siku ya nne ambayo ilikuwa ni siku ya Jumapili wakakaa wakiingojea ile adhabu ambayo hawakuijua ni adhabu gani, wala hawakujua itatokea mahali gani na wala hawakujua nini la kufanya. Ghafla tu lilipochomoza jua ikawaijia ile adhabu ya Mwenyezi Mungu S.W.T. kwa ukelele mmoja tu uliotoka mbinguni uliopigwa na Malaika Jibril A.S. ukawanyakuwa roho zao kisha ukafuatia mtetemeko mkali wa kutoka ardhini uliowatetemesha kwa nguvu kabisa mpaka wakafa wote katika nyumba zao wala hakuokoka hata mmoja wao. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat A`araaf aya ya 78,

فَأَخَذَتْهُمْ الرَّجْفَةُ فَأَصْبَحُوا فِي دَارِهِمْ جَاثِمِينَ

Maana yake, "Basi tetemeko la ardhi likawanyakuwa (roho zao), na kulipokucha wakawa majumbani mwao kifudifudi wamekwishakufa."
Na pia kama alivyosema Mola Mtukufu katika Suratil Qamar aya ya 31,

إِنَّا أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ صَيْحَةً وَاحِدَةً فَكَانُوا كَهَشِيمِ الْمُحْتَظِرِ

Maana yake, "Kwa yakini tuliwapelekea ukelele mmoja tu, wakawa kama mabuwa ya kujenga uwa." Lakini Mwenyezi Mungu S.W.T. akamuokoa Mtume Wake pamoja na wale watu waliouamini ujumbe wake kama ilivyodhihirika katika Suratin Naml aya ya 53,

وَأَنجَيْنَا الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ

Maana yake, "Na tukawaokoa wale walioamini na waliokuwa wakimcha (Mungu)."

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini