Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

HISTORIYA YA IMAMU HUSSEIN (A.S) 3

0 Voti 00.0 / 5

IMAMU HUSSEIN A.S

Sehemu ya tatu

BAADA YA KUFARIKI MTUME (s.a.w.w)

Wakati Imamu Hussein (a.s) alipofikisha umri wa miaka Sita babu yake Mtume Muhammad (s.a.w.w) alifariki dunia, na baada ya miezi sita alifariki dunia mama yake mzazi Fatimah Zahara (a.s). Kipindi cha miaka ishirini na mitano kilichofuatia ambacho Imamu Aliy (a.s) alipinduliwa na kundi la waasi na Ukhalifa ukashikwa na wanamapinduzi, Imamu aliishi maisha ya kujitenga. Na kuanzia hapo Imamu Hussein (a.s) alipata muda wa kutosha kujifunza tabia ya baba yake.

Mafunzo haya yalichukua muda wa ujana wake na alipokuwa na umri wa miaka thalathini na moja baba yake alirudi kwenye Ukhalifa. Imamu Hussein (a.s) na kaka yake Hassan (a.s) walifuatana na baba yao katika vita vya Jamal, Siffin na Nahrawaan kuwapiga waasi waliokuwa wakiitwa Naqithuuna, Qasituuna na Mariquuna.

Katika mwaka wa Arubaini hijiria Amirul Muuminina Aliy bin Abi Talib (a.s) alikufa kishahidi katika msikiti wa Kufa nchini Iraq na Imamu Hassan (a.s) alilazimika kuzishika kazi za Ukhalifa.

Imamu Hussein (a.s) akiwa ndugu mtiifu. Alimsaidia Imamu Hassan (a.s) na Imamu Hassan (a.s) alipofanya mapatano na Muawiyyah l.a ili kuziokoa haki za uislamu. Imamu Hussein (a.s) nae aliishi maisha ya kujitenga kama alivyofanya Imamu Hassan (a.s).

Imamu Hussein (a.s) alitumikia Uislamu kimya kimya kwa muda wa miaka ishirini. Miaka kumi chini ya kaka yake Imamu Hassan (a.s) na miaka kumi baada ya kifo cha Imamu Hassan (a.s).

Lakini katu Muawiyyah l.a hakuyatimiza masharti ya mapatano aliyoyafanya na Imamu Hassan (a.s). Muawiyyah alimuua Imamu Hassan (a.s) kwa kumtilia sumu na akawasumbua sana wafuasi wa Imamu Aliy (a.s) na akawafunga jela, akawakata vichwa na hata kuwasulubisha.

Mwishoni kabisa Muawiyyah l.a alimalizia kuvunja masharti ya mapatano yaliyobaki ambapo hukutakiwa kuteua mrithi wa Ufalme bali aurudishe kwa Imamu ambaye alikuwepo enzi hizo ambaye ni Imamu Hussein (a.s). Muawiyyah l.a akavunja sharti hili kwa kumchagua mwanawe Yazeed kuwa mrithi wake na alitumia kila aina ya nguvu na Propaganda ili kuungwa mkono na waislamu alikuwa na silaha mbili kali, hongo na upanga.

TABIA ZA IMAMU HUSSEIN (a.s)

Imamu Hussein (a.s) alikuwa Imamu (Khalifa) wa tatu na alikuwa mchamungu na mnyoofu. Hata maadui wake waliukubali ukarimu wake na sifa zake nzuri. Alikuwa akienda Sajida elfu moja katika muda wa masaa ishirini na manne. Alikwenda Hijja mara ishirini na tano kwa miguu. Mtukufu Mtume (s.a.w.w) yeye mwenyewe alisema: Hussein (a.s) ana ushupavu na ukarimu wangu ". Mlangoni pake kila wakati palikuwa na masikini na kila mara nyumba yake ilijaa wageni na hakuna mtu yeyote yule aliyerudi kutoka nyumbani kwa Imamu Hussein (a.s) bila ya kuridhika.

Kwa sababu alikuwa akijulikana kwa jina la" "Baba wa masikini". Alikuwa na kawaida ya kuchukua mikungu ya tende na mikate wakati wa usiku kwenda kuwapa watu fukara na masikini. Na kazi hizi za usiku ziliweka alama katika mgongo wake.

Shu'aybu bin Abdurrahmaan al Khuza'iy amesema: ilikutwa athari juu ya mgongo wa Hussain bin Aliy (a.s) siku ya Karbala, ndipo wakamuuliza Zainul Abidina (a.s) kuhusu athari hiyo, Imamu Sajjad akasema: Hii ni alama iliyoachwa na kitendo cha kubeba magunia ya chakula juu ya mgongo wake kupeleka kwenye makazi ya wajane, mayatima na masikini.[1]

Alikuwa akisema kila mara, "Kama akikuijia masikini yeyote yule kutaka msaada, ina maana kuwa masikini huyo kakuuzia heshima yake na sasa ni wajibu wako kutomrudisha akiwa na wazo baya kuhusu heshima yako.

Jinsi alivyokuwa akiwatendea watumwa na watumishi wake ilikuwa ni kama vile atendavyo baba mwenye huruma kwa watoto wake. Kila mara alikuwa akitafuta nafasi ya kuwapatia uhuru.

Watu wote wa wakati wake waliitambua vizuri elimu yake bora. Katika kila tatizo la kidini aliendewa na kutakiwa alitatue tatizo hilo. Mkusanyiko wa sala (Dua'a) zake unaitwa "Sahifah Husseiniah" (kitabu cha Hussein a.s) upo hadi sasa.

Alikuwa na huruma sana kiasi ambacho aliwaonea huruma hata maadui zake. Kila mara aliwashughulikia sana masikini wa watu wengine kabla ya Wale masikini wake. Imamu Hussein (a.s) akiwa na sifa zote hizi nzuri. Alikuwa mpole na mnyenyekevu sana kiasi ambacho siku moja alipokuwa akipita mahali fulani masikini walimkaribisha kula chakula pamoja nao. Imamu Hussein (a.s) alikwenda kukaa pamoja nao ingawa hakuweza kula nao kwa kuwa sio halali kwa watu wa Nyumba ya Mtume saww kutumia Chochote kilichotolewa sadaka.

Imamu Hussein (a.s) alikuwa msamehevu kwa yeyote aliyemkosea. Imamu Zainul Abidina (a.s) amesema: Nilimsikia Hussein (a.s) akisema: Lau mtu atanitukana katika sikio hili la kulia na akaniomba samahani katika sikio la kushoto, nitamkubalia. Hiyo ni kwa sababu Amirul Muuminina Aliy bin Abi Talib (a.s) alinisimulia kwamba alimsikia babu yangu Mtume (s.a.w.w) akisema: Hatoingia kwenye Hodhi yule asiyekubali samahani kutoka kwa aliye katika haki au aliye katika makosa..[2]

Matokeo yake yalikuwa kila awapo, watu hawakuweza kumtazama. Aliheshimiwa sana kiasi ambacho hakuna mtu yeyote yule aliyezikataa sifa zake nzuri, hata lile kabila lililokuwa adui kwa ukoo wake.

Siku moja alimwandikia barua kali sana Muawiyyah l.a alipoisoma barua hiyo alichomwa sana moyoni. Wafuasi wa Muawiyyah l.a walimshauri amuandikie Imamu Hussein (a.s) barua kama hiyo. Muawiyyah Alijibu:, Kama nikiandika mambo yasiyo ya kweli katika barua hiyo basi barua hiyo haitatimiza lengo lake, na kama nikijaribu kutafuta upungufu wowote ule katika tabia zake Imamu Hussein (a.s) Wallahi, nashindwa kupata upungufu wowote ule.

Masaibu ya Karbala yanaonyesha Sura ya ushujaa, ukweli, nia nzuri, uvumilivu, ustahimilivu na amani. Hakuzilegeza juhudi zake katika kufanya mapatano hadi mwisho. Lakini hakukubali kugeuka japo inchi moja kutoka kwenye njia yake ya wajibu wake na aliridhika kufa kuliko kufanya hivyo.

Aliishi akiwa chini ya baba yake Ally bin Abi Twalib (a.s) na akiwa ndugu mdogo wa Imamu Hassan (a.s) na aliwatii kwa kuwa ilikuwa haki kwake kufanya hivyo. Huko Karbala aliwaongoza watu wake vizuri sana kama alivyowatii wakubwa wake.

Imamu Hussein (a.s) ni mnara wa taa ya Uongofu, jahazi ya uokovu kwa wanadamu wote.[3]

Fuatana nami sehemu ya nne historia ya Maasum Hussein (a.s).

 

 


[1].  Al Manaqibul Ibn Shahri Ashub Jz 4 UK 66

[2]. Ihqaqul Haqi Jz 11 UK 431.

[3]. Uyunu Akhbarir Ridhaa Jz 1 UK 59 hadithi 29.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini