Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

HISTORIYA YA IMAMU HUSSEIN (A.S) 9

0 Voti 00.0 / 5

IMAMU HUSSEIN (A.S)

Sehemu ya tisa

JIHADI YA IMAMU HUSSEIN BIN ALIY (A.S) 6

WAIRAQI WAGEUKA MUSLIM AUAWA

Asubuhi ilipofika yule mkuu wa jeshi alimjulisha Ibn Ziyad sehemu alipo Muslim (a.s), akamtuma Ibn al Ash'ath na watu Sabini miongoni mwa mashujaa ili wamkamate,. Muslim aliposikia vishindo vya nyayo za Farasi akajua kwamba anaendewa akaharakisha Dua'a yake aliyokuwa akiiomba baada ya swala ya asubuhi, kisha akavaa vazi la vita na akamwambia Twau'ah: Umeshatimiza wajibu wako miongoni mwa wema na umeshachukua hisa yako katika shufaa ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, na jana nilimuona ami yangu Amirul Muuminina Aliy (a.s) katika ndoto naye ananiambia, wewe kesho utakuwa nami.

Muslim aliwatokea akiwa amenyanyua upanga wake na walishamvamia ndani ya Nyumba, akawatoa humo kisha wakarejea kwake tena akawashambulia na kuwatoa huku akisoma beti zisemazo:

"Ni mauti, basi fanya na litakuwa utakalolifanya.

Bila shaka kikombe cha mauti utakunywa.

Hivyo fanya subira katika jambo la Mwenyezi Mungu Mtukufu, Hukumu ya Mwenyezi Mungu kwa viumbe ni yenye kuwa.

Akauawa watu Arubaini na moja miongoni mwao, na kutokana na nguvu zake alikuwa anamshika mtu na kumtupa juu ya Nyumba. Ibn al Ash'ath alituma ujumbe kwa Ibn Ziyad akimtaka msaada wa wanaume basi akamtumia ujumbe akimlaumu, ndipo Ash'ath akamtumia ujumbe: "Unadhani kwamba umenituma kwa muuza kibanda miongoni mwa wauza vibanda wa Kufah au mkokota mikokoteni miongoni mwa wakokota mikokoteni wa Haira? Hakika umenituma kwa shujaa miongoni mwa mashujaa wa Muhammad bin Abdullah hivyo nizidishie askari.

Mapigano yakawa baina ya Muslim na Bakiri bin Hamran al Ahmariy, Bakiri alimpiga Muslim mdomoni na akaukata mdomo wa juu, ukaanguka chini na akaangusha meno mawili ya juu, Muslim akampiga pigo kali juu ya kichwa chake na jingine juu ya bega lake hadi upanga ulikaribia kutokea tumboni, na hivyo akafa.

Kisha washambuliaji walimshambulia wakiwa juu ya Nyumba, wakamtupia mawe na wakawa wanawasha vijinga vya moto na kumtupia, akawakabili kwa kuwapiga katika vichochoro huku akikariri:

"Nimeapa sitauliwa isipokuwa nikiwa huru, Hata kama nayaona mauti kuwa ni mabaya.

Kila mtu leo atapata Shari, Naogopa kudanganywa au kuhadaiwa."

Majeraha yakamzidi na kumchosha huku akivuja damu, hivyo akaegemea kwenye kisusi cha nyumba, wakamshambulia kwa kumtupia mishale na mawe, naye akasema: Vipi mnanitupia mawe kama wanavyotupiwa makafiri na hali mimi ni katika AhIul Bait wa Nabii mwema, je hamjali haki ya Mtume wa Mwenyezi Mungu Katika kizazi chake?

Ibn al Ash'ath akamwambia: Usiuwe nafsi yako na wewe uko katika dhima yangu. Muslim akasema: Nitekwe ningali na nguvu, hapana Wallahi haiwi hivyo katu. Akamshambulia Ibun al Ash'ath hadi akakimbia, kisha wakamshambulia kutoka kila upande hali amezidiwa na kiu, mwanaume mmoja akamchoma kwa upanga wa nyuma, akaanguka na akatekwa. Na inasemekana kwamba walichimba shimo na wakalifunika kwa udongo kisha wakasogea mbali mpaka alipoangukia wakaja wakamteka.

Ndipo akapelekwa kwa Ibn Ziyad l.a, alipofika aliona mtungi wa maji karibu na mlango wa Kasri, akasema ninywesheni maji kutoka kwenye haya maji. Muslim bin Amru al Bahiliy akamwambia: Hutaonja tone mpaka uonje maji ya moto katika Jahanamu. Muslim bin Aqiil akasema: Wewe nani? Akasema: Mimi ni ambaye nimetambua haki ulipoipinga na akamsihi Imamu ulipomdanganya. Ibn Aqiil akamwambia: Mama Yako anahasara, uko mgumu na Muovu Kiasi Gani? Wewe mtoto wa Bahiliy ndio unastahili zaidi kuingia Motoni. Kisha akaegemea ukuta wa Kasri.

Amarah bin Uqba bin Abi Mu'it akamtuma kijana wake anayeitwa Qays akamletea maji, na kila alipotaka kunywa, kikombe kilijaa damu. Na katika mara ya tatu alikwenda ili anywe lakini kikombe kikajaa damu na meno yake yakadondokea humo, hapo akayaacha na akasema: Kama yangekuwa katika riziki iliyopangiwa ningekunywa. Kijana wa Ibn Ziyad akatoka na kumuingiza kwake, hakusalimia, Mlinzi akamwambia humsalimii Amiri? Ibn Aqiil akamwambia: Nyamaza yeye siyo kiongozi wangu. Na inasemekana kwamba alisema :. Amani kwa Mwenye kufuata uongofu, akaogopa mwisho mbaya na kumtii Mwenyezi Mungu.

Ibn Ziyad l.a akacheka na akasema: Usalimie usisalimie hakika wewe ni mwenye kuuliwa.

Muslim bin Aqiil akasema: Kama utaniuwa basi alishamuuwa mbaya kuliko wewe aliye mwema kuliko mimi (Abdurrahmaan bin Muljamu, alimuuwa Ally bin Abi Twalib as), hakika wewe hutaacha kuuwa vibaya wala kutesa vibaya, dhamira mbaya wala kulaumiwa sana, na hakuna yeyote anayestahili kwayo kuliko wewe.

Ibn Ziyad I.a akasema: Umeshatoka dhidi ya Imamu wako na umevunja umoja wa waislamu na umeleta fitina. Muslim bin Aqiil (a.s) akasema: Umesema uongo hakika aliyevunja ni Muawiyyah na mtoto wake Yazeed l.a na fitina ameipanda baba yako, na mimi natarajia Mwenyezi Mungu ataniruzuku shahada katika mkono wa aliye Muovu kati ya viumbe vyake.

Kisha Muslim bin Aqiil (a.s) akataka atoe Wosia kwa baadhi ya kaumu yake, akamruhusu, akawatazama waliokaa akamuona Umar bin Saad, akamwambia :. Baina yangu na yako kuna uhusiano, na mimi nina haja kwako na ni wajibu wako kuikidhi, nayo ni siri. Lakini Umar akakataa. In Ziyad l.a akasema usikatae kukidhi haja ya mtoto wa ami yako. Umar akaenda naye mahali ambapo Ibn Ziyad I.a anawaona, Muslim bin Aqiil (a.s) Akamuusia alipe kutokana na thamani ya upanga wake na ngao yake deni alilokopa tangu aingie Kufah linalofikia diriham mia Sita, na achukue kiwiliwili chake toka kwa Ibn Ziyad I.a na akizike kisha amwandikie barua Hussein (a.s) juu ya habari yake. Umar bin Saad akasimama na akatangaza siri yote kwa Ibn Ziyad I.a.

Ibn Ziyad l.a akasema :. Hakufanyii hiyana ni mwaminifu lakini huenda akaaminiwa mwenye hiyana. Kisha Ibn Ziyad I.a akamgeukia Muslim na akasema :. Ewe Ibn Aqiil, umewakuta watu wako pamoja kisha ukawagawanya. Akasema :. Hapana sikujua kwako hilo lakini watu wa mji wamedai kwamba baba yako Ameuawa wema wao, amemwaga damu zao, na akafanya kwao vitendo vya Kisra na Kaiser, hivyo tukawajia ili tuimarishe uadilifu na kulingania katika hukumu ya Kitabu.

Ibn Ziyad I.a akasema: Una nini wewe na hao, je hatukuwa tunafanya uadilifu kwao? Muslim bin Aqiil (a.s) akasema: Hakika Mwenyezi Mungu anajua wewe siyo mkweli na kwamba wewe unauwa kwa ghadhabu, kwa uadui na dhana mbaya. Ndipo Ibn Ziyad I.a akaanza kutoa kashifa kwa Amirul Muuminina Aliy bin Abi Talib as kwa Aqiil (a.s) na Hussein (a.s). Muslim bin Aqiil (a.s) akasema: Wewe na baba yako mnafaa zaidi kwa kashifa hizo, basi hukumu utakavyohukumu ewe adui wa Mwenyezi Mungu.

Ibn Ziyad I.a akamuamuru Shamiy apande naye juu ya Kasri na akate shingo yake na atupe mwili wake na kichwa chake ardhini, akampandisha juu ya Kasri huku Muslim bin Aqiil (a.s) akimsabahi Mwenyezi Mungu, akisoma tahalili na takibira

سبحان الله و الحمد لله ولاإله إلاالله والله أكبر.

Huku akisema: Ewe Mwenyezi Mungu hukumu baina yetu na kaumu iliyotudanganya wakatufedhehesha na kutudanganya. Akaelekea upande wa Madina na akamsalimia Imamu Hussein (a.s)

السلام عليك يا ابا عبد الله الحسين.

Shamiy akamsogelea karibu na nyayo, akakata shingo yake na akatupa kichwa chake na mwili wake ardhini, akateremka akiwa dhalili. Ibn Ziyad I.a akamwambia una nini? Akasema: Nilimuona mtu mweusi na mbaya mbele yangu akiuma vidole vyake wakati wa kumuuwa, basi nikamuogopa. Ibn Ziyad I.a akasema: Huenda ulishikwa na bumbuwazi. Na kisha wakamuua Hani bin Urwa.

Na Ibn Ziyad l.a akaamua Muslim na Hani kufungwa kamba miguuni mwao na kuburutwa hadi sokoni na kusulubiwa katika kanisa kichwa chini miguu juu, na akapeleka vichwa viwili kwa Yazeed l.a naye akaviweka katika njia ya Damascus.

ألا لعنة الله على الظالمين وسيعلم الذين ظلموا أي منقلب ينقلبون .

Laana za Mwenyezi Mungu Ziwe Juu ya madhalimu.... ".

Fuatana nami sehemu ya kumi historia ya Maasum Hussein bin Aliy (a.s)

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini