Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

HISTORIYA YA IMAMU HUSSEIN (A.S) 11

0 Voti 00.0 / 5

IMAMU HUSSEIN BIN ALLY (a.s)

Sehemu ya kumi na moja

JIHADI YA IMAMU HUSSEIN (a.s)

IMAMU HUSSEIN AKUTANA NA FARAZDAQ BIN GHALIBU, MSHAIRI

Hussein (a.s) alikutana na Farazdaq Bin Ghalib mshairi, akamuuliza habari za watu alikotoka, Farazdaq akasema: "Nyoyo zao ziko pamoja na wewe na panga zao ziko pamoja na Bani Umayyah na hukumu inateremka kutoka mbinguni."

Abu Abdillah akasema: "Umesema kweli, amri ni ya Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu anafanya anachokitaka na kila siku Mola wetu yuko katika jambo, Kama hukumu itateremka kama tunavyotaka tutamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema zake, naye ni mwenye kuombwa msaada katika kutekeleza shukrani, na kama hukumu itakuwa kinyume cha matarajio yetu, basi hakuvuka mpaka ambaye nia yake ilikuwa ni haki, na uchamungu ni dhamira yake." Kisha Farazdaq akamuuliza juu ya nadhiri na ibada ya Hijja, kisha wakaagana.

      Abu Abdillah aliondoka bila ya kumwangalia yeyote, akukutana na Bashir bin Ghalib katika eneo liitwalo Dhat Iraqi, akamuuliza kuhusu watu wa Kufah, akasema:  "Panga ziko pamoja na Bani Umayyah na nyoyo ziko pamoja na wewe." Akasema (a.s)  "Umesema kweli."

Alikaa eneo la Al Khuzaimah mchana na usiku moja na kulipokucha dada yake Zainabu (a.s) alifika kwake na kumwambia: "Hakika mimi nimesikia sauti ikisema: "Ewe jicho la sherehekea kwa bidii, nani atawalilia Mashahidi baada yangu, watu wanafuatwa na mauti kwa kadiri ya kutekeleza ahadi yangu." Hussein (a.s) akasema: "Ewe dada yangu yote yaliyohukumiwa basi yatakuwa."

Alipoteremka (a.s) Sehemu inayoitwa Zurud aliteremka karibu na Zuheiri Bin Al Qayni Al Bajaliy na hakuwa ameandamana naye, na hakupendezwa na kitendo cha kuteremka pamoja naye lakini maji yaliwakusanya katika Sehemu moja, hivyo pindi Zuheiri na jamaa zake walipokuwa kwenye mlo aliowaandalia,  aliwasili mjumbe wa Hussein (a.s) akimwita Zuheiri kwenda kwa bwana wake Abu Abdillah (a.s) , Zuheiri akakataa kuitika wito, isipokuwa mkewe "Dalham bint Amru" alimhimiza kwenda kusikiliza maneno yake.

Zuheiri alikwenda kwa Hussein (a.s) na upesi alirudi kwa jamaa zake akiwa na furaha, uso wake ukiwa wa njano, akaamuru aletewe virago na mizigo yake, akaipeleka katika upande wa bwana wa vijana wa watu wa peponi na akamwambia mke wake, nenda kwa watu wako hakika mimi sipendi upate tabu kwa sababu yangu isipokuwa kheri. Kisha akawaeleza waliokuwa pamoja naye: "Anayetaka miongoni mwenu kumnusuru mtoto wa Mtume s.a.w.w anifuate, vinginevyo haya ni maagano ya mwisho."

Kisha akawaeleza yale aliyoyasisitiza Salman Alfarisy katika tukio hili, akasema: "Tulishambulia Najar tukaifungua na tukapata ngawira na tukafurahi kwa hilo, Salman Alfarisy alipoona furaha tuliyonayo, alisema: "Kama mtawakuta vijana wa kizazi Cha Muhammad s.a.w.w basi kuweni na furaha sana kwa Kupigana kwenu pamoja nao kwa yale mliyoyapata, yale yanayoshinda ngawira, lakini mimi nawaageni.""" Mke wake akasema: "Mwenyezi Mungu akujaalie kheri na nakuomba unikumbuke siku ya kiyamah mbele ya babu wa Hussein (a.s)

Na katika Sehemu ya Zurud alipewa habari za kuuliwa Muslim bin Aqili (a.s) na Haniy Bin Urwah, Hussein (a.s) akasema: "Hakika sisi sote ni wa Mwenyezi Mungu, na hakika kwake yeye tutarejea."

إنا لله و انا اليه راجعون.

Na akawatakia rehema kwa wingi, akalia na wakalia pamoja naye Bani Hashim, na mayowe ya wanawake yakawa mengi Sehemu hiyo ikatikisika kwa kifo cha Muslim bin Aqili, na machozi yakamtoka kila mtu.

Abdillah Bin Salim na Mundhir Bin Al Mushmaala Al Asadiyan wakamwambia: "Tunakushauri ewe mtoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu ungeondoka katika Sehemu yako hii hakika huna wa kumnusuru huko Kufah." Familia ya Aqili ikasimama na kusema: "Hatuondoki mpaka tulipize kisasi au tuonje aliyoyaonja ndugu yetu." Hussein akawatazama na akasema: "Hakuna kheri katika maisha baada ya hawa."

     Na katika Sehemu ya Shaququ, Hussein (a.s) alimuona mwanaume anakuja kutoka Kufah, akamuuliza juu ya watu wa Iraq, akamwambia wamekusanyika dhidi yake, akasema (a.s) : "Hakika ni maamuzi ya Mwenyezi Mungu anafanya analolitaka na Mola wetu Mtukufu kila siku yuko kwenye jambo." Kisha akasoma beti za mashairi akisema:

                     "Hata kama dunia inahesabiwa kuwa na thamani,

              Lakini makazi ya thawabu za Mwenyezi Mungu Mtukufu yana thamani zaidi.

                      Na ikiwa mali zote ni zenye kuachwa basi vipi chenye kuachwa mtu akifanyie ubakhili.

              Na ikiwa riziki ni zenye kugawiwa na kukadiriwa basi ni nzuri zaidi mtu kutokuipupia katika kuichuma.

                  Na ikiwa miili imeumbwa kwa ajili ya mauti basi mtu kuuliwa kwa upanga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ni bora zaidi.

                Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yenu enyi Aali Ahmad, hakika mimi najiona kuwa ni mwenye kuondoka toka kwenu."

Na hakika Sehemu ya Zabalah alipewa habari za kuuliwa Qays kutoka kwa Mus'hiru as Swaydaniy, akawajulisha watu hilo na akawaruhusu waondoke, basi wakatawanyika kulia na kushoto, akabakia na wafuasi wake ambao walikuja naye kutoka Makkah, na walikuwa wamemfuata wengi miongoni mwa mabedui kwa kudhani kwao kwamba, anakwenda sehemu ambayo watu wake wamemtii Mwenyezi Mungu, hivyo akaona si vizuri kwenda nao isipokuwa baada ya kujua wanachokiendea, na alijua atakapowapa ruhusa ya kuondoka hatamfuata isipokuwa yule anayetaka kumliwaza katika mauti.

Fuatana nami katika Sehemu ya kumi na mbili historia ya Ma'asum Hussein (a.s)

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini