Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

HISTORIYA YA IMAMU HUSSEIN (A.S) 14

0 Voti 00.0 / 5

IMAMU HUSSEIN A S

Sehemu ya kumi na nne

Jihadi ya Imamu Hussein bin Ally as 11

IMAMU HUSSEIN AANDAA KABURI LAKE NA WAFUASI WAKE

Kisha Hussein as akanunua Sehemu ambayo sasa ina kaburi lake, alinunua kutoka kwa watu wa Nainawa na Al Ghadhiriya kwa thamani ya dirham sitini elfu na akaitoa sadaka kwao, na akawapa sharti kuwa waonyeshe kaburi lake na wamkaribishe siku tatu yule anayezuru. Na haram ya Hussein aliyoinunua ilikuwa na ukubwa wa mail nne urefu na upana, nayo ni halali kwa watoto wake na wafuasi wake, na ni haramu kwa wasiokuwa wao miongoni mwa waliokhalifu, na humo kuna bwawa. Na Imepokewa kutoka kwa Imamu as Sadiq as kuwa amesema: "Hakika wao hawakutekeleza masharti."

(Na hapa kuna funzo kwetu kuwa ni vizuri kuaanda Sehemu ya makazi yako ya kudumu na siyo vizuri ukasubiri hadi ukafariki na ukatupwa popote ambapo wanazuoni wa fiqihi wanapendekeza kuanda hata sanda yako na ukawa unaiangalia mara kwa Mara na kuifuta vumbi kwani itakukumbusha Mauti kwa hiyo utatenda matendo yako kwa tahadhari)

Hurr akatuma barua kwa Ibn Ziyad akimpa habari kuteremka kwa Hussein as hapo Karbala, Ibn Ziyad akaandika barua kwa Hussein as: "Ama baad: Ewe Hussein nimepata habari ya kuteremka kwako Karbala, na Amirul Muumini (feki) Yazid ameniandikia barua kuwa nisilalie mto na kujifunika, wala nisile nikashiba, isipokuwa ima nikukutanishe na Mola mjuzi (nikuuwe) au uwe chini ya hukumu yangu na hukumu ya Yazid, wasalaam وسلام."

Hussein as aliposoma barua aliitupa toka mikononi mwake na akasema: "Haitafaulu kaumu iliyonunua radhi ya kiumbe kwa hasira ya Muumba." Mjumbe akamtaka atoe jawabu, akasema: "Hana jibu kwangu kwa sababu limestahili kwake neno la adhabu." Ibn Ziyad akamwamuru Umar bin Saad kwenda Karbala, alikuwa amepiga kambi katika Sehemu ya Hammam A'uyun akiwa na askari elfu nne 4000 ili aende nao Dastabiny, kwa sababu watu wa ad Daylam walikuwa wameshindwa. Ibn Ziyad akamwandikia hati ya ugavana wa Ray (Khurasan) na vitongoji vya Dastabiny na ad Daylam, Ibn Saad akamuomba amsamehe katika hilo lakini alipotaka kupokonywa hati alimuomba Ibn Ziyad ampe muda wa usiku mmoja ili atafakari.

Umar bin Saad alikusanya washauri wake, wakamkataza kwenda kumpiga vita Hussein as, mtoto wa dada yake, Hamza bin Mughira Bin Shu'uba alimwambia. "Nakushauri kwa ajili ya Mwenyezi Mungu usiende kumpiga vita Hussein as hatimaye ukakata udugu wako, Wallaahi kama utatoka katika dunia yako bila mali ni bora kwako kuliko kukutana na Mwenyezi Mungu huku una dhambi ya damu ya Hussain as". Ibn Saad akasema: "Nitafanya hivyo." Akalala katika usiku wake hali Akifikiri katika jambo lake na alisikika akisema:

      "Je? Niache ufalme wa Ray na Ray ni matamanio yangu,

       au nirejee na Hali ni mwenye kulaumiwa kwa kumuuwa Hussein.

         Na katika kumuuwa kuna moto ambao hauna kizuizi

       Lakini ufalme wa Ray ni burudisho la macho yangu."

Ilipowadia asubuhi alimwendea Ibn Ziyad na akasema: "Hakika wewe umenipa kazi hii na watu wamesikia, niepushe nayo na badala yangu mtume kwa Hussein mtu ambaye mimi sio mjuzi katika vita kuliko yeye." Na akamtajia watu miongoni mwa wakubwa wa Kufah. Ibn Ziyad akasema: "kama utakwenda na askari wetu sitakuamrisha kuwa Kiongozi kwa ambaye nataka kumtuma, vinginevyo ulete hati yetu." Alipoona ametilia mkazo akasema: "Nitakwenda." Umar bin Saad akamwita Qurat bin Qays al Hadhiliy ili amuulize Hussein as, ni kwa nini amekuja Iraq.

Alipomfikishia barua ya Ibn Saad, Abu Abdillah as akasema: "Hakika watu wa mji wenu wameniandikia barua, njoo kwetu, lakini kama mmechukia basi nitaondoka kwenu." Akarejea na jibu hilo kwa Ibn Saad, ndipo akamwandikia barua Ibn Ziyad akimweleza anayosema Hussein as, jibu lake likamjia: "Ama baad: Mweleze Hussein na wafuasi wake, watoe kiapo cha utii kwa Yazid, kama atafanya hivyo tutabadili rai yetu."

Wanajeshi wakawa wengi Karbala mpaka inasemekana kuwa walifikia laki moja, na wamesema ni zaidi ya idadi hiyo. Ibn Saad akapiga kambi katika mto Furati, wakazingira maji na wakazuia maji yasimfikie Bwana wa Mashahidi as na wafuasi wake wa Hussein as, wakazuia njia ya kwenda kwenye maji mpaka kiu ikawadhuru, na hiyo ilikuwa ni kuanzia siku ya saba Muharram 61 hijiria. Hussein as akachukua shoka na akatembea nyuma ya mahema ya wanawake hatua kumi na sita upande wa kibla, akachimba ikatoka chemchem ya maji matamu, wakanywa kisha ikakauka na haikuonekana tena athari. Ibn Ziyad akatuma ujumbe kwa Ibn Saad:

"Imenifikia habari kuwa Hussein as anachimba visima na anapata maji, anakunywa yeye na wafuasi wake, kuwa mwangalifu! Ikikufikia barua yangu wakataze kuchimba visima kadiri uwezavyo na uwabane sana." Akatuma wakati huo huo Amru bin Al Hajjaj na askari mia tano 500, wakateremkia eneo la as Shai'ah, na hiyo ilikuwa kabla ya kifo cha Hussein as kwa siku tatu.

Fuatilia darasa zetu Sehemu ya kumi na tano na zinazo fuata ujifunze zaidi kuliko kuwafuata viongozi kibubusa

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini