Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

HISTORIYA YA MTUKUFU MTUME (S.A.W.W) 2

0 Voti 00.0 / 5

KUZALIWA KWA UISLAMU UPYA CHINI YA UONGOZI WA NABII WA KWANZA KUUMBWA NA NABII WA MWISHO KUTUMWA

MTUKUFU MTUME MUHAMMAD SAWW ATANGAZA UJUMBE WAKE KWA WANADAMU

Wakati Muhammad saww alipokuwa na umri wa miaka 40, aliamriwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kupitia Malaika wake Jibril as, kutangaza Upweke wake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa wanadamu na hasa kwa waabudu masanamu na washirikina wa dunia nzima, na kutoa ujumbe wa amani kwa wanadamu waliokaa kivita.

Kwa mwitiko wa amri hii ya mbinguni, Muhammad saww alianzisha program nzito sana iitwayo Uislamu ambayo ilikuwa ibadili mwisho wa mwanadamu daima.

Kabla ya mwito huo kumjia wa kutangaza Upweke wa Muumba, Muhammad saww alikuwa na tabia ya kutumia muda wake mwingi katika taamuli na tafakuri. Ili kujikinga na kuingiliwa kati na wasiwasi usio na lazima, alikwenda mara kwa mara kwenye pango la mlimani liitwalo Hira, maili tatu Kaskazini Mashariki ya Makkah, na kutumia zile siku nyingi za kiangazi pale pangoni.

Alikuwa huko Hira pale siku moja yule Malaika MKuu Jibril as alipotokea mbele yake, na kumletea zile habari njema kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amemchagua yeye kwa Mtume wake wa mwisho kwa Ulimwengu, na ameweka juu yake jukumu la kuwaongoza wanadamu kutoka kwenye msukosuko wa dhambi, makosa na ujinga, kwenda kwenye mwanga wa uongofu, Haki na ujuzi. Jibril as kisha akamwambia Muhammad saww soma Aya zifuatazo:-

إقرأ باسم ربك الذي خلق. خلق الانسان من علق.  إقرأ وربك اللأكرم.  الذي علم بالقلم.  علم الإنسان ما لم يعلم.

Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba. Amemuumba mwanadamu katika pande la damu!. Soma, na Mola wako ni Mtukufu mno. Ambaye amemfunza (kuandika) kwa kalamu. Amemfunza mwanadamu lile asilolijua. 96:1-5

Aya hizi tano zilikuwa ndiyo wahyi wa mwanzoni kabisa, na zilikuja kwa Muhammad saww katika "Usiku wa cheo" au "Usiku uliobarikiwa" ndani ya mwezi wa Ramadhani (mwezi wa tisa wa kalenda ya Kiislamu) wa mwaka wa 40 wa Tembo. Zipo mwanzoni mwa sura ya 96 ya Qur-ani Tukufu. Jina la Sura hiyo ni Iqra'a (Soma) au A'laq (pande la damu lililoganda).

Huu Usiku wa cheo au Usiku uliobarikiwa hutokea kwa mujibu wa hadithi, wakati wa kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani, ambayo ni mwezi 19, 21 na 23. ya mwezi wa Ramadhani.

Katika mapokezi husika ya mapokezi ya Mtukufu Mtume Muhammad saww ya Wahyi wa kwanza, Waislamu wanasema Mtukufu Mtume Muhammad saww hakushitushwa au kuhofishwa na kutokea kwa Jibril as alimkaribisha kama aliyekuwa akimtarajia. Jibril as alimletea zile habari njema kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amemchagua yeye kuwa Mtume wake wa mwisho kwa wanadamu na akampongeza kwa kuteuliwa kuwa mpokeaji wa heshima kubwa kuliko zote kwa mwanadamu katika dunia hii.

Muhammad saww hakusita katika kuupokea ujumbe wa Utume wala hakuwa na ugumu wowote katika kurudia (kuzisoma) zile Aya za Wahyi (ufunuo) wa mwanzo. Alizisoma au kuzirudia bila ya taabu yoyote, mwenyewe. Jibril as, kwa kweli, hakuwa mgeni kwa Muhammad saww, na alijua pia kwamba sababu ya kuwepo kwake mwenyewe ilikuwa ni kutekeleza ujumbe uliowekwa juu yake na Mwenyezi Mungu Mtukufu kama Mtume wake. Aliyekuwa "mwenye kuuelewa ujumbe" hata kabla ya kufika kwa Jibril as. Yeye Jibril as alimpa tu ishara ya kuanza.

Waislamu wanasema kwamba kitu kimoja ambacho Jibril as hakutakiwa akifanye, kilikuwa ni kutumia nguvu za kimwili juu ya Muhammad saww kusoma. Kama alifanya, itakuwa kwa kweli ni mtindo wa ajabu wa kumpa Muhammad saww huo uwezo wa kusoma - kwa kumminya au kumkaba. Waislamu wanasisitiza zaidi kwamba Muhammad saww hakuazimia kujiua katika wakati wowote wa maisha yake, sio hata katika nyakati za huzuni sana; na kwamba haijawahi kumjia kwamba angeweza kamwe kuguswa na "uovu" au kwamba angeweza "kupotoshwa" au "kuchafuliwa"

Hata hivyo, Muhammad saww alihisi wasiwasi juu ya ukubwa wa jukumu lililo mbele yake. Alitambua kwamba katika utekelezaji wa kazi yake, atakuja kukabiliwa na upinzani mkubwa, mgumu, na uliodhamiriwa wa wapagani wa dunia nzima. Ile hali ya wasiwasi wake ilikuwa karibu kudhihirika. Alikuwa, kwa hiyo, kwenye hali ya uzito wa mawazo alipoondoka pale pangoni kurudi nyumbani. Na alimuomba Khadija, mke wake kumfunika ndani ya blanket wakati akikaa chini kumueleza yale matukio ya kule mlima wa Hira.

Khadija Bint Khuwailid mke wake aliposikia Hadithi aliyomwambia Muhammad saww, alimliwaza na kumpa moyo kwa kusema, "Ewe mwana wa ami yangu, kuwa mwenye furaha nzuri, Mwenyezi Mungu Mtukufu amekuchagua wewe kuwa Mtume wake. Wewe siku zote ni mpole kwa majirani zako, mwenye msaada kwa jamaa zako, mkarimu kwa mayatima, wajane na masikini, na mwenye upendo kwa wageni. Mwenyezi Mungu Mtukufu kamwe hatakuacha wewe peke yako.

Inawezekana kwamba Mtukufu Mtume Muhammad saww alizidiwa kwa muda kidogo na mawazo juu ya uwajibikaji wake kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kuubeba mzigo mzito wa jukumu lake jipya, lakini pale aliposikia maneno ya kuliwaza ya Khadija, mara moja alijisikia zile fadhaa zote ndani yake zikipungua. Alimtuliza na kumpa moyo kwamba pamoja na mkono wa Mwenyezi Mungu Mtukufu juu ya bega lake, atasimama sawia na majukumu yake na ataweza kushinda vikwazo vyote.

Fuatana nami Sehemu ya IFUATAYO historia ya Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini