Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

BIBI FATIMA (A.S) KIIGIZO CHEMA KWA WANAWAKE 1

0 Voti 00.0 / 5

BIBI FATIMA (A.S) KIIGIZO CHEMA KWA WANAWAKE

Sehemu ya kwanza

Bismillahi Rahmani Rahimi.

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu ndani ya kitabu chake kitukufu: "Na mnapowauliza kitu (wakeze Mtume) waulizeni nyuma ya pazia"[1]

Baada ya kauli hii ya Mwenyezi Mungu, ni wajibu wetu kuufahamisha ulimwengu mzima ya kwamba, Mwanamke ni kiungo muhimu katika jamii, na anayo haki na heshima kama mtu mwingine yeyote anayeishi katika dunia. Siyo kweli kwamba yeye ni kiumbe tofauti, au ni kiumbe kigeni katika suala zima la maisha ya kila siku, bali yuko katikati ya mazingira na matukio yake daima. Kwa kuwa Uislamu ni dini inayoshughulikia hali ya maisha ya wanadamu kwa kila nyanja, imetoa umuhimu wa pekee katika kulinda na kutetea utu, heshima, pamoja na haki za mwanamke. Kwa sababu hiyo basi, Uislamu umemuwekea mwanamke kanuni za sheria zitakazomfaa kulingana na mazingira yake kimaisha, iwe katika maisha yake peke yake au katika ndoa, na au ndani ya familia na jamii yote kwa ujumla.

Kadhalika Uislamu umempa mwanamke nafasi ya kushughulikia masuala yanayomhusu katika dunia na pia akhera, kama yalivyoelekezwa kisheria. Nafasi hii inaweza kumfikisha katika safu za Malaika na kumfanya kuwa kiumbe kitakatifu hapa duniani na akhera.

Kutokana na umuhimu wa mwanamke katika jamii ya wanadamu, Quran inayo sura nzima inayoitwa Sura An-nisaa, ambayo inataja baadhi ya masuala yanayowahusu wanawake.

Isitoshe ndani ya Quran zimo Aya nyingi zinazozungumzia miongozo mbali mbali juu ya mwanamke, ikiwemo namna ya mienendo na mavazi yake ndani ya jamii, halikadhalika na haki zake. Yote haya lengo lake ni kuonesha umuhimu wa mwanamke na kumtakia mafanikio na usalama wake.

Maumbile ya mwanamke yanapoangaliwa kwa makini sana, hapana shaka yoyote yanaonekana kwamba, yanatofautiana mno na maumbile ya mwanaume, kisaikolojia na katika sehemu fulani ya mazingira ya kijamii. Kutokana na tofauti hii, ilibidi pia kuwe na tofauti kati ya mwanamke na mwanaume katika baadhi ya hukumu za kisheria na kanuni. Tofauti hii imekuja kutokana na hali halisi ya maumbile ya mwanamke. Kwa hiyo basi, kanuni na sheria nazo zikaja katika baadhi ya nyakati kufuatia hali na maumbile ya mwanamke. Siyo kweli kwamba tofauti hii ni kwa ajili eti ya kumdhalilisha na kumfanya mwanamke kuwa ni kiumbe pungufu, kama wanavyodai maadui wa Uislamu.

Katika moja ya kanuni muhimu za sheria ya kiislamu iliyotiliwa mkazo, na kumlazimisha mwanamke kutoachana nayo ni Hijabu. Kanuni ya Hijabu haikuja isipokuwa ni kwa ajili ya kuhifadhi na kulinda mafanikio ya mwanamke, bila kusahau heshima yake na utu wake. Kanuni hii inazingatiwa kuwa ni miongoni mwa kanuni muhimu sana ndani ya Uislamu.

Kutokana na umuhimu wake, Mwenyezi Mungu ameitaja katika Aya nyingi za Qur'an, na wala hakutosheka kuitaja katika Aya moja au nusu ya Aya, kama ambavyo kuna kanuni ambazo Mwenyezi Mungu amezitaja mara moja katika Aya moja au hata nusu ya Aya. Tutaonesha umuhimu wa kanuni hii ndani ya kitabu hiki kwa mujibu wa Aya nyingi za Qur'an zilizoitaja kanuni hii.

Mwenyezi Mungu amelikariri mara nyingi suala la Hijabu katika Qur'an ili kuonesha umuhimu wake ndani ya jamii na maisha ya wanadamu. Je ni kwa nini basi Waislamu inawapasa kuliangalia suala la Hijabu kwa makini, na pia kutumia muda mwingi kulitafakari na kuzinduana? Jawabu lake ni kwa sababu upinzani na uchochezi wa kutia dosari Hijabu, na kuitolea tafsiri ambazo siyo maana halisi iliyokusudiwa katika vazi hili, umeongezeka na unazidi kuongezeka. Upinzani na uchochezi huu unakuja kutoka kwa maadui wa Uislamu na watu wapenda maovu. Na kwa kutumia kalamu zao na kelele zao, siku zote wamekuwa wakijaribu kuonesha ubaya wa Hijabu, na kwamba eti inarudisha nyuma maendeleo. Pia hupata wakadai, "Ati Hijabu ni kumdhalilisha mwanamke na ni kumtesa." Hayo ni pamoja na uzushi mwingineo wanaouona kuwa unaweza kuwasaidia katika kampeni yao hii dhidi ya Hijabu. Kwa masikitiko makubwa, ziko baadhi ya serikali zinaonesha msimamo wa wazi kabisa katika kupinga Hijabu, bali zinatumia kila aina ya uwezo walionao kusambaza upinzani huo kwa kuwataka wanawake wa kiislamu waache kujisitiri kwa mujibu wa sheria ya dini yao[2].

Mambo haya hayafanyiki kwa siri, kwani mara kwa mara tunasoma magazetini na au kusikia kwenye vyombo vya habari vingine kwamba serikali fulani imetoa agizo kuwazuwia mabinti wa kiIslamu wasiendelee na masomo ya sekondari au chuo kikuu kwa sababu tu ya wao kuvaa Hijabu. Na kuna baaadhi ya serikali zinatoa maagizo kuwa, miongoni mwa masharti ya kujiunga na vyuo vikuu vya nchi hizo, mwanamke anatakiwa asivaae Hijabu!!

Mpenzi msomaji, ukirejea nyuma kidogo tu katika historia ya nchi ya Iran utakuta kwamba, mwanzoni mwa utawala wa mfalme Shah aliyepinduliwa, lilipitishwa azimio rasmi la kuzuia kabisa uvaaji wa Hijabu kwa wanawake wa kiislamu nchi nzima.

Askari walitawanywa njiani, sokoni mpaka katika njia za majangwani kwa ajili tu ya kuwazuia kuvaa na kuwavua wanawake wanaoonekana kuwa wamevaa Hijabu. Kutokana na unyama huu, wanawake wengi wa kiislamu waliona ni bora wabakie majumbani mwao kwa muda wa miaka mingi kutokana na hofu ya kunyanyaswa na askari wa serikali.

Enyi watu nyie! Ni ya nini vita hii munayoineza dhidi ya Hijabu? Ni kwani nini hampambani na umalaya na maovu yaliyokithiri ndani ya jamii yetu na badala yake mnaelekeza mapambano yenu kwa wanawake wanaolinda heshima ya mwanamke, heshima ya jamii bali pia wanalinda utu wetu?[3].

Ni kwa nini mapambano hayo msiyaelekeze kwenye madanguro ambayo tuna hakika kwamba yanajulikana fika? Kwa nini hampambani na ulevi unaotishia familia zetu? Kwa nini hampambani na madawa ya kulevya yanayoziangamiza nchi zetu na kizazi chetu, bali pia yanaangusha uchumi wa nchi zetu? Kwa nini hampambani na umaskini uliokithiri ndani ya jamii yetu? Mbona hampambani na vibaka wanaotishia usalama wa raia kila kukicha? Mwenyezi Mungu anasema:

وَإِذَا تَوَلَّىٰ سَعَىٰ فِي الْأَرْضِ لِيُفْسِدَ فِيهَا وَيُهْلِكَ الْحَرْثَ وَالنَّسْلَ ۗ وَاللَّهُ لَا يُحِبُّ الْفَسَادَ.

"Na anapotawala hujitahidi kufanya uharibifu katika nchi na kuteketeza mimea na viumbe. Na Mwenyezi Mungu hawapendi watu waharibifu[4].

Siyo ajabu watu hawa kusema hayo wayasemayo hasa tunapozingatia kwamba, wao wanaelewa vizuri na kutambua hekima zilizomo ndani ya kanuni hii na falsafa zake, mambo ambayo yanakubalika kiakili na kimaumbile. Kwa upande mwingine wanakuta Hijabu ndiyo kizuizi kikubwa na madhubuti dhidi ya matendo yao machafu ndani ya jamii safi ya Waislamu. Ndiyo maana wakawa wanaipinga kanuni hii ya kiislamu kwa njia mbali mbali kupitia maonesho ya Television, Redio, Magazeti, Majarida, Sinema n.k. Nia yao ni kumuondeshea aibu na haya mwanamke wa kiislamu, pia kumvua vazi la utamaduni wake kama Mwislamu, na baadaye asiwe na haya wala aibu kisha wamtelekeze na kumsukumiza katika janga la maovu na uchafu mwingineo.

Maadamu mambo yako katika hali hii, yaani vita inaendeshwa dhidi ya mwanamke wa kiislamu, basi hana budi mwanamke huyu wa kiislamu ashikamane na vazi hili la Hijabu. Inampasa pia asimamie kwa uwezo wake wote kueneza mafunzo na hekima za Hijabu baina ya wanawake, wasichana walioko mashuleni na majumbani, na asisitize uvaaji wa vazi hili la Hijabu. Wajibu huu ni kwa mwanamke kwa upande wake na pia kwa Waislamu wote.

Halikadhalika Waislamu wasikubali kutoa nafasi kwa maadui hawa kutekeleza malengo yao ya kishetani, ambayo yanaudhuru Uislamu na Waislamu. Nataraji kitabu hiki kitakuwa ni chenye kuongeza hamasa ya kuimarisha kanuni ya Hijabu na kuivaa. Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kufanikisha na ndiye msaidizi.

 


[1].Qur'an 33:33.

[2].Wakati tunafanya tarjuma ya kitabu hiki, habari kutoka Ufaransa zinasema kuwa: "Serekali ya Ufaransa imepiga marufuku vazi la Hijabu kwa wanawake wa kiislamu nchini humo." Kwa bahati mbaya sana Mufti wa Misri Sheikh Tantawi ameonesha udhaifu mkubwa kwa kusema kuwa: "Wanawake wa kiislamu nchini Ufaransa wanaweza kuvua hijabu iwapo watalazimishwa kufanya hivyo." Habari kamili ya tukio hili tumeichapisha mwishoni mwa kitabu hiki kama tulivyoipata katika mtandao wa Internet. Mtarjumi.

[3]. Kwa hakika ni jambo la kuhuzunisha sana kuwaona wanawake wanaotambua nini maana ya mwanamke wanaishi kwa hofu na mashaka nchini mwao kwa sababu tu wanafuata maagizo ya dini yao. Iko haja tufahamu kwamba, wanawake hawa wanafahamu maana ya kuwa mwanamke na thamani yake katika jamii yoyote ile na si ya kiislamu peke yake. Wanawake hawa wanatambua vyema kwamba umbile la mwanamke linastahiki vazi gani ili kuibakisha heshima ya mwanamke ndani ya jamii. Lakini kwa huzuni na masikitiko makubwa wanawake hawa na utamaduni wao ndiyo maadui wakubwa ndani ya jamii yetu na kwa mawazo ya watu wengi wanastahiki kupigwa vita mpaka wazivue hizo Hijabu zao.

Enyi watu nyie: na hasa wanawake! Hamuoni namna utu na heshima ya mwanamke ivyopoteza thamani yake? Hivi kweli nia yenu ni kuisaidia jamii iondokane na majanga ya ukimwi, watoto wa mitaani na umalaya uliokithiri nchini mwetu? Tazameni mabinti zenu namna wanavyovaa, hivi kweli mnatufunza nini sisi watoto wa kiume? Nashindwa kuizuia kalamu isiandike kwamba, hata watoto wadogo katika zama hizi kwa namna mnavyojidhalilisha wanafahamu maumbile ya wanawake yakoje. Je, huu ndio uhuru? Je, hizi ndizo haki za binaadamu mnazozipigania? Je, haya ndiyo maendeleo ya nchi yetu? Kwa upande wa serikali yetu hivi kweli mmeshindwa kuiongoza jamii kwenye maadili ya kibinaadamu? Hivi kweli wasichana wetu na wanawake wetu wamekushindeni kuwadhibiti kiasi cha kuwa tunaona mambo ambayo hayastahiki konekana hadharani? Mbona hakuna hatua zozote mnazochukua dhidi ya matendo haya yanayofanyika hadharani? Mtarjumi

[4]. Qur'an 2: 205. Makusudio ya Aya hii ni kuonesha kwamba watawala wanapopewa madaraka, badala ya kushughulikia matatizo na maslaha ya raia zao, wao hufanya kila juhudi kueneza uovu, machafu na uharibifu mwingineo ikiwemo ule wa mazingira ya nchi na hatimaye kuziacha nchi hizo zikiwa ni mateka wa maovu, ujinga na umasikini mkubwa. Mtarjumi.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini