Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

BIBI FATIMA (A.S) KIIGIZO CHEMA KWA WANAWAKE 3

0 Voti 00.0 / 5

BIBI FATIMA (A.S) KIIGIZO CHEMA KWA WANAWAKE

Sehemu ya tatu

Bibi Fatima (A.S) Kiigizo Chema Kwa Wanawake

Bibi Fatimah (a.s.) ni mwanamke anayezingatiwa kuwa ni mwanamke wa kutolea mfano katika dini ya kiislamu, na pia ni kiigizo chema kwa kila mwanamke anayetafuta mafanikio katika maisha yake. Bibi Fatimah binti Muhammad (s.a.w.w) ndiye mwanamke bora ulimwenguni aliyezaliwa na kupata malezi katika nyumba iliyokuwa ikishuka ndani yake Wahyi kutoka mbinguni.

Si hivyo tu bali Bibi Fatimah alihitimu mafunzo ya Uislamu katika madrasa ya Utume, na kutokana na mafunzo hayo aliweza kufikia daraja ya juu na tukufu. Katika kuthibitisha ubora wa Bibi Fatimah, Mtume (s.a.w.w) amepata kusema, "Hakika Mwenyezi Mungu huwa radhi kwa radhi ya Fatimah, na huchukia kutokana na kuchukia kwa Fatimah[1]."

Kwa ajili ya daraja kubwa aliyonayo Bibi Fatimah katika Umma wa Nabii Muhammad (s.a.w.w) imekuwa ni wajibu kwa kila mwanamke duniani kuiga mwenendo wa Bibi huyu katika maisha yake, ajing'arishe kwa nuru yake nzuri na afuate nyayo zake ambazo zitamuelekeza kwenye mafanikio na utukufu. Hakika Bibi Fatimah (a.s), ni mfano wa kila utukufu na kila jema. Mwanamke yeyote atafanikiwa iwapo ataamua kufuata mwenendo wa Bibi Fatmah (a.s.), na kinyume chake ni kuwa, kila mwanamke ataangamia iwapo ataamua kujichagulia mwenendo wake au kuiga usiyokuwa mwenendo wa Bibi Fatimah. Pia Fatimah (a.s.) alikuwa Mchaji Mungu na mwenye kutekeleza vilivyo maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Pia ile maana nzima ya Hijabu aliifahamu vema na kuitekeleza kama ilivyoamriwa na Mwenyezi Mungu.

Hivyo utekelezaji wake katika maamrisho ya Mwenyezi Mungu ulikuwa wa hali ya juu, kwani hakupata kutoka nje ila huwa amevaa vazi la kumsitiri mwili wake wote tangu kichwani hadi miguuni. Isitoshe alikuwa akiichukia mno tabia ya wanawake kutoka majumbani mwao bila kujisitiri kisheria. Bibi Fatimah alichukizwa na tabia hiyo kwa sababu Mwenyezi Mungu pia anaichukia tabia ya kutokujisitiri na hasa kwa kuwa kukosa sitara ya kishera kwa wanawake ni ufunguo wa kuyaendea maovu na ni miongoni mwa vitangulizi vinavyosababisha watu kuteleza, bali wanaaanguka kabisa.

Sasa hivi tunawaletea baadhi ya mafundisho kuhusu Hijabu na tutaona pia utukufu wa Bibi Fatimah katika mafunzo hayo.

Ni Kitu Gani Kilicho Bora Kwa Mwanamke?

Inasimuliwa katika historia kwamba, Mtume (s.a.w.w) siku moja aliwauliza Masahaba suali lifuatalo: "Je! ni kitu gani kilicho bora kwa mwanamke?" Masahaba walinyamaza kwa kuwa jibu la mkato na sahihi hawakulifahamu, ikawa kama kwamba akili zao zinahangaika baina ya kuwa kilicho bora kwa mwanamke ni mali, uzuri wake, kuolewa au kitu gani? Kipindi chote hiki Bibi Fatimah alikwisha lisikia swali hilo, na baada ya kimya cha kukosekana jibu, Bibi Fatimah alimtuma mtu aende kwa Mtume (s.a.w.w) akatoe jibu sahihi la swali hili nalo ilikuwa: "Kilicho bora kwa mwanamke ni yeye mwanamke asimuone mwanaume na mwanaume naye asimuone mwanamke[2]."

Baada ya jibu la bibi Fatimah Masahaba walikuwa wakisubiri jibu la Mtume atasema nini kuhusu jawabu alilotoa Binti yake. Mtume (s.a.w.w) akasema "Amesema kweli Fatimah." Na akaongeza kusema, "Fatimah ni sehemu iliyotokana na mwili wangu." Maana ya maneno ya Mtume yalimaanisha kwamba hilo ndilo jawabu sahihi na hiyo ndiyo imani.

Kutokana na jawabu hili, Bwana Mtume (s.a.w.w.) akawa ameitangazia dunia nzima kwamba: Utu, heshima, utukufu, na wema wa mwanamke unapatikana ndani ya Hijabu, na kinyume chake ni uovu na shari, isitoshe hasara humfika mwanamke anapoitupa Hijabu.

Mazungumzo Ya Kustaajabisha

Historia inaendelea kutufahamisha kwamba Bibi Fatimah (a.s.) alikuwa amekaa na baba yake ambaye ndiye Mtume (s.a.w.w), mara alibisha hodi Sahaba Abdalla ibn Ummi Maktum ambaye alikuwa kipofu. Kabla Sahaba huyu hajaingia Bibi Fatimah (a.s.) alisimama akaondoka mahali hapo. Baada ya kwisha mazungumzo baina ya Mtume na Sahaba huyu, Sahaba Abdallah ibn Ummi Maktum aliondoka. Bibi Fatima alirudi na akaendelea kuzungumza na Mtume (s.a.w.w.) Bwana Mtume (s.a.w).wakamuuliza Binti yake sababu ya kuondoka wakati alipoingia Sahaba Abdallah ibn Ummi Maktum hali kuwa anafahamu kabisa kwamba yule ni kipofu haoni[3]

Bibi Fatimah alijibu kama ifuatavyo."Ikiwa yeye hanioni basi mimi namuona na yeye ananusa harufu ya wanawake.

Mtume (s.a.w.w) alifurahishwa mno na jawabu la Binti yake ambalo linaonyesha kipimo cha Uchamungu na utukufu unaotoka kwa Binti yake Mwenye hekima. Isitoshe kwa jawabu hilo, Bwana Mtume hakumlaumu binti yake kutokana na mkazo huu mkali unaohusu Hijabu, bali furaha ya Mtume iliendelea kwa upeo mkubwa na akaunga mkono kwa dhati kabisa kisha akasema: "Nashuhudia kwamba wewe ni sehemu iliyotokana nami[4]".

 

 


[1]. Mustadrak Alhakim juz 3 uk , Al isabah ya Ibn Hajar Al asqalani juz 4 uk.

[2]. Hapana shaka makusudio yaliyomo ndani ya jawabu la bibi Fatimah (a.s.) ni kwamba, wawili hawa yaani mwanamke na mwanaume ni wale wasiokuwa na uhsiano wa kisheria. Watu wenye uhusiano kisheria ni kama hawa wafuatao: Mama, dada, shangazi na au Baba, kaka, mjomba na wengine ambao wametajwa katika vitabu vinavyohusika na sheria. Ama mume na mke, wawili hawa uhusiano kati yao hauna haja ya kutolewa maelezo. Mtarjumi.

[3]. Ni vyema ikaeleweka wazi kwamba Bwana Mtume (s.a.w.w) alimuuliza Binti yake suali hilo hali ya kuwa yeye mwenyewe anajua wazi kuwa Sahaba yule alikuwa haoni, lakini lengo la Bwana Mtume (s.a.w) kuuliza suali hilo alitaka aone namna Binti yake atakavyo toa jawabu la suali hilo ili historia ipate kusajili mazungumzo haya ya kiimani na ubakie kuwa ni mfano mzuri wa kuigwa siku zote.

[4]. Mustadrak Al-Wasail Kitabun-Nikah. Biharul-An-Waar juz 104 uk 38.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini