Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

NI NANI AHLULBAYT (A.S) 3

0 Voti 00.0 / 5

AHLUBAYT WA MTUME KILUGHA NI WENGI SANA KISHERIA NI WATU MAALUM WASIOZIDI KUMI NA NNE  AMBAO NI CHAGUO LA MWENYEZI MUNGU NA WALIOTOHARISHWA 

Kwa mujibu wa Qur'an na hadithi za Mtukufu Mtume s.a.w.w

Wanazuoni wakubwa wakubwa wa Ahlisuna wamekiri na kuandika vitabuni mwao.

kwa maana hiyo Ahlisuna na shi'ah hawatofautiani kuhusu kuwatambulisha Ahlubaiti Rasul.

Sunnah na Nyumba ya Mtume saww, Ahlul Bayt.

Ni nani hao wanaounda Nyumba ya Mtume saww?

HOJA YA TATU:

Mtukufu Mtume saww mwenyewe ameeleza wazi ni nini kinachomaanishwa na Ahlul Bayt wake au al Itrah. Hili linaakisiwa katika hadithi zifuatazo zinazo patikana katika Vyanzo vikuu vya Ahlisuna vinavyo kubalika.

Muslim anasimulia kutoka kwa Aisha :

Mtukufu Mtume alitoka nje akiwa amevaa shuka jeusi la manyoya, wakati Hassan mtoto wa Ally alipokuja, basi Mtume alimruhusu Hassan kuingia ndani pamoja naye akiwa amemfunika kwenye shuka lake. Kisha akaja Hussein na yeye pia akaingia ndani. Halafu akafuata Fatimah. Yeye aliingia ndani vile vile. Kisha Ally naye akaja. Yeye pia aliingia chini ya shuka, kiasi kwamba shuka lilimfunika Mtume, Ally, Fatimah, Hassan na Hussein. Ndipo Mtukufu Mtume akasoma :. Hakika si mengineyo Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, Enyi watu wa Nyumba ya Mtume, na kuwatakasa kabisa kabisa. "33:33

Imamu Ahmad bin Hanbal anasimulia kutoka kwa Umar bin Maymuna kwamba yeye alisema :" tulikuwa tumekaa karibu na ibn Abbas, binamu yake Mtukufu Mtume saww na mwanachuoni mkubwa. Kikundi cha watu tisa kilimjia na kumuomba waondoke naye ama wale watu walikuwapo pale wawapishe. Ibn Abbas akaondoka pale pamoja nao. Baada ya muda kiasi, Ibn Abbas alirudi akiwa amechukia sana kutokana na maneno mabaya aliyoyasikia kutoka kwao kuhusu Ally a.s. Msimliaji anaongeza kwa kusema kwamba, kisha Ibn Abbas akaanza kuelezea nafasi ya Ally a.s mbele ya macho ya Mtukufu Mtume saww na baadhi ya sifa zake. Alitaja muhanga wa Ally pale Khaybar, wakati maswahaba wote walikimbizwa yeye alikuwa imara na shupavu hadi akazifungua ngome nzito za wayahudi, na kabla ya hapo Mtume saww alimtangaza kuwa ni mtu anayependwa ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake naye anampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Sifa nyingine ni kutangazwa kwa ufunuo (wahyi) wa Surat al Tawbah kwa washirikina kulikofanywa ni Ally a.s. Katika msimu wa hijja mwa wa tisa hijiria. Abu Bakr aliye kuwa katumwa kwanza akaambiwa rudi wewe si mustahiki. Halafu akataja tukio jingine ambamo Mtukufu Mtume saww alizungumza na mabinamu zake na kuuliza :. Ni nani miongoni mwenu ambaye yuko tayari kuniamini na kunifuata katika ulimwengu huu na ule wa Akhera? Imam Ahmad bin Hanbal anasema kwamba mabinamu wote wa Mtukufu Mtume walikataa kutoa majibu ya kukubali. Kulikuwa na jibu moja tu la kukubali na hilo lilitoka kwa Imamu Aliy as. Swali hili na jibu lake vilirudiwa kwa mara nyingine katika kikao hicho hicho. Mwishowe Mtukufu Mtume akasema :. Wewe (Ally) ni wasii wangu (mshika makamu) ndugu na Khalifa baada yangu katika dunia hii na Akhera. "Ibn Abbas vile vile alieleza kwamba Ally alikuwa ndiye mtu wa kwanza kusilimu.

Tukio jingine ambalo Ibn Abbas alilieleza na ambalo ni lenye kufaa sana kwenye mjadala wetu hapa ni kwamba Mtukufu Mtume alichukua shuka lake, akamfunika nalo Fatimah, Ally, Hassan na Hussein na kusoma aya hii :

إنما يريد الله ليذهب عنكم الرجس أهل البيت ويطهركم تطهيرا.

Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni (kukukingeni na) uchafu, Enyi watu wa Nyumba ya Mtume, na kuwatakasa kabisa kabisa. " 33:33

Tukio jingine Ibn Abbas alielezea kadhia ya Laylat al Mabit, wakati Ally alipolala sehemu ya hatari kwenye nyumba ya Mtukufu Mtume saww nje kumezingirwa ni vijana zaidi ya Arubaini wakiwa na silaha kali. Lakini yeye hakujali kwa ajili ya kuutumikia uislamu na Mtukufu Mtume wa Mwenyezi Mungu alilala ili kuwafanya wapagani hao wadhanie kwamba Mtukufu Mtume alikuwa bado yuko nyumbani kwake akiwa amelala, ambapo kwa kweli alikuwa anahama kwenda Madina. Ibn Abbas anaeleza kwamba wakati Mtukufu Mtume saww alipokuwa anataka kwenda Tabuuk, alimuacha, Imamu Aliy kuchukua nafasi yake hapo Madina (kuwa Khalifa wake). Ibn Abbas anaeleza kwamba Mtume saww alifunga milango yote binafsi iliyoelekea msikitini isipokuwa mlango wa Ally a.s, hivyo ni yeye peke yake aliye kuwa anastahiki na ana uwezo wa kuingia msikitini moja kwa moja kutoka nyumbani kwake.

Imamu Ahmad bin Hanbal anasimulia kutoka kwa Anas bin Malik kwamba wakati ile aya ya Utakaso imeteremshwa, kwa muda wa miezi sita mfululizo Mtukufu Mtume saww alikuwa akipita nyumbani kwa Ally na bi Fatumah kila asubuhi akiwa njiani kuelekea msikitini kwa ajili ya swala ya al Fajr na huku akiita kwa sauti ya juu : "Swala, Enyi watu wa Nyumba!

Ziko hadithi nyingi sana katika vitabu vya ahlisuna vinavyo kubalika zinazoonyesha watu wanaounda nyumba ya Mtume s.a.w.w pia na aya za Qur-an zipo nyingi sana na zimetafsiriwa na wanazuoni wa ahlisuna wakubwa wakubwa wote kuwa zinathibitisha kuwa Ahlul Bayt wa Mtume saww ni watu maalumu ambao ni Aliy, Fatimah, Hassan na Hussein a.s na Maimamu tisa katika kizazi cha Hussen as. Miongoni mwa aya hizo ni aya ya al Qurba (watu wa karibu zaidi), pale Mtukufu Mtume saww alipoagizwa asiombe malipo yoyote kwa kazi ya kufundisha kwake bali tu kwamba watu wapaswa kuwapenda Qurba wake 42:23.

Zamakhashari, Mwanachuoni mkubwa wa Ahlulisuna na Mfasiri wa Quran amesema kwamba wakati aya hii ilipoteremshwa, Mtukufu Mtume saww aliulizwa kwamba ni akina nani waliolengwa na aya hii. Mtukufu Mtume saww Alijibu : "Hao ni Ally, Fatimah, na watoto wao wawili wa kiume Hassan na Hussein a.s

Rejea

MWISHO wa chanzo cha pili cha itikadi za Shi'ah. Fuatana nami kujua chanzo cha tatu ambacho ni Akili.

REJEA:

  1. Sahihi Muslim Jz 4 UK 1883, hadithi ya 2424. Kitabu Fadha'ili al Sahaba, babu Fadha'ili Ahlul Bayt, mfululizo wa Sakhar namba 4450.
  2. Musnad Ahmad bin Hanbal, Musnad ya Bani Hashim namba 2903.
  3. Musnad Ahmad bin Hanbal.
  4. Musnad Ahmad bin Hanbal, Sakhar namba 13231, Sunan Al Tirmidhi, Sakhar namba 3130.
  5. Al Kashshaf ya Zamakhashari, Jz 3 UK 467.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini