Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

NABII YUUNUS A.S

0 Voti 00.0 / 5

BSMILAHI AR-RAHMANI AR-RAHIIMI

NABII YUUNUS A.S

Mwenyezi Mungu S.W.T. alimtuma Nabii Yuunus A.S. kwa watu wa mji wa Ninawah ulioko nchi ya Iraq, kwani watu hawa walikuwa wakiabudu masanamu. Nabii Yuunus A.S. alikuwa na sauti nzuri sana hata inasemekana wakati alipokuwa akisoma wanyama wa porini walikuwa wakimsikilza sauti yake, kama alivyokuwa akifanya Nabii Daud A.S. katika zama zake. Alipowaijia watu wake aliwakataza ukafiri na akawalingania katika ibada ya Mungu mmoja. Lakini watu wake walimkadhibisha, na wakakataa wito wake na jambo hili liliendelea kwa muda mrefu. Nabii Yuunus A.S. alipokata tamaa alitoka nje ya mji kwa kukhofia adhabu na huku ameghadhibika akiwaahidi watu wake kushukiwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Alipowaacha watu wake, nyuma yake Mwenyezi Mungu S.W.T. akatia toba na imani katika nyoyo zao kisha wakajuta ubaya waliomfanyia Mtume wao. Na haijatokea mji wa watu wake kamili uliomuamini Mtume wake ila mji wa Nabii Yuunus. Kwani wote walipomuamini Mwenyezi Mungu S.W.T. aliwasamehe na akawaondolea adhabu ambayo ingeliwapata duniani kwa ile kufuru yao kama ilivyowapata kina Adi na Thamuwd na walio mfano na wao. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Yuunus aya ya 98, "

فَلَوْلا كَانَتْ قَرْيَةٌ آمَنَتْ فَنَفَعَهَا إِيمَانُهَا إِلاَّ قَوْمَ يُونُسَ لَمَّا آمَنُوا كَشَفْنَا عَنْهُمْ عَذَابَ الْخِزْيِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَمَتَّعْنَاهُمْ إِلَى حِينٍ

Maana yake, "Kwa nini usiweko mji ulioamini (upesi kabla ya kuadhibiwa), ili imani yake iwafae? Isipokuwa watu wa Yuunus (tu ndio walioamini mara walipohisi kuwa adhabu inakuja. Basi wakaokoka). Walipoamini tuliwaondolea adhabu ya hizya katika maisha ya dunia na tukawastarehesha kwa muda (tuliotaka)."

Nabii Yuunus A.S. alipoondoka alielekea kwenye pwani ya bahari. Pale pwani akapanda jahazi lililokuwapo majini. Jahazi lile likenda katika bahari, ukawaijia upepo mkali baharini, na lile jahazi lilikuwa limeshehena, ikabidi atoswe mmoja wao, wakafanya kura ili kumchagua mtu kati yao atakaetoswa baharini. Kura ikamwangukia mara tatu Nabii Yuunus kwa amri aliyoitaka Mola Mtukufu. Nabii Yuunus hakungojea atoswe bali yeye mwenyewe akajitosa baharini, mara samaki mkubwa alimmeza hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa.

Na kwa amri ya Mwenyezi Mungu S.W.T. samaki yule hakumvunja mifupa yake wala hakula nyama yake. Alibakia katika tumbo lake na huku akimdhukuru kwa wingi Mwenyezi Mungu S.W.T. kwa kusoma dua ifuatayo: "ALLAHUMMA LAA ILAAHA ILLA ANTA SUBHAANAKA INNI KUNTA MINA DHAALIMIIN." Na hayo yaliyompata ni kwa sababu alikuwa asitoke nje ya mji wake bila idhini ya Mola wake. Lakini yeye alitoka nje ya mji kwa ghadhabu ya watu wake. Kwa hivyo ikawa mtihani mkubwa kwake.

Na baada ya siku ambazo hakuna azijuae, samaki yule alimtema na kumtupa kwenye ufuko wa pwani na hali ya kuwa ni mgonjwa. Mwenyezi Mungu S.W.T. akamuoteshea mmea unaofanana na maboga au mmumunya na akawa akila na kunywa mpaka iliporejea afya yake. Alipokuwa na hali nzuri na mwenye afya, Mwenyezi Mungu S.W.T. akamtuma mpaka kwa wale wale watu wake aliowakimbia ambao idadi yao ilikuwa laki moja au zaidi, wakamwamini Nabii Yuunus aliyowaitia. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu akawastarehesha mpaka muda wao wa kufa. Kisa hiki cha Nabii Yuunus kimetolewa katika Surat Ssaaffaat tangu Aya ya 139 hadi ya 148,

"وَإِنَّ يُونُسَ لَمِنْ الْمُرْسَلِينَ * إِذْ أَبَقَ إِلَى الْفُلْكِ الْمَشْحُونِ * فَسَاهَمَ فَكَانَ مِنْ الْمُدْحَضِينَ * فَالْتَقَمَهُ الْحُوتُ وَهُوَ مُلِيمٌ * فَلَوْلاَ أَنَّهُ كَانَ مِنْ الْمُسَبِّحِينَ * لَلَبِثَ فِي بَطْنِهِ إِلَى يَوْمِ يُبْعَثُونَ * فَنَبَذْنَاهُ بِالْعَرَاءِ وَهُوَ سَقِيمٌ * وَأَنْبَتْنَا عَلَيْهِ شَجَرَةً مِنْ يَقْطِينٍ * وَأَرْسَلْنَاهُ إِلَى مِائَةِ أَلْفٍ أَوْ يَزِيدُونَ * فَآمَنُوا فَمَتَّعْنَاهُمْ إِلَى حِينٍ

Maana yake, "Na hakika Yuunus alikuwa miongoni mwa Mitume. (Kumbukeni) alipokimbia kwenye jahazi lililoshehena. Akaingia kupigwa kura akawa miongoni mwa walioshindwa. Samaki akammeza hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa. Na ingelikuwa hakuwa katika wanaomtukuza Mwenyezi Mungu. Bila shaka angelikaa tumboni mwake mpaka siku ya kufufuliwa. Lakini tulimtupa ufukoni hali ya kuwa mgonjwa. Na tukamuoteshea mmea wa maboga. Na tulimpeleka kwa (watu) laki moja au zaidi. Basi wakaamini na tukawastarehesha mpaka muda (wao wa kufa)."

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini